Hili la kutapisha maji machafu msimu wa mvua linakera sana

06May 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la kutapisha maji machafu msimu wa mvua linakera sana

UMETIMU msimu wa mvua na sasa unaendelea katika baadhi ya mikoa nchini. Nianze kusema ni neema kwa wakulima na sote, maana chakula ni muhimu kwa kila mmoja wetu, wakati huohuo mvua ina umuhimu sana kwa mengi ya kimazingira, pia ‘maji ni uhai.’

Pamoja na mvua hizo kuendelea kunyesha kila mahali, baadhi ya watu wana mapokeo yake katika sura hasi wakitaja ndugu zetu wengi wa mijini na mfumo yao ya vyoo si sahihi.

Mvua zinaponyesha na vyoo vyao kufurika, mbinu wanayotumia ni kujaribu kutiririsha maji hayo machafu mtaani katika namna maarufu kwa jina la ‘kuyatapisha.’

Nafuu hiyo, inazua lingine la uchafu umma jirani unasambaziwa maji hayo yenye vinyesi.

Tahadhari ya afya ambayo ni angalizo la awali, ni kwamba wanaotapisha maji hayo machafu, wajue wazi kuwa wanasababisha kuwapo kwa milipuko ya magonjwa hata ikiwamo watu kuhara ovyo.

Inakera kuona mtu anaona shida kutafuta gari za majitaka ili kunyonya maji hayo, anahamia mbadala wa kuwachukua na kuwalipa fedha kidogo mfano kati ya Sh. 5000 na Sh. 10,000, wamfanyie kazi ya ‘kutapisha choo chake.

Ieleweke kwamba inapofanyika hivyo, kuna maana kwamba wanavyotapisha maji hayo yanaenda mitaani wanakoishi watu wengine wakubwa kwa wadogo, wenye viatu na wasio navyo, wakubwa kwa wadogo baadhi wanayakanyaga na watoto hata kuhusisha na mikono na midomo yao.

Tukumbuke, kuna watoto mitaani wadogo hupenda kuchezea maji hata mvua zikinyesha na kukatika. Sasa hao watoto wanapochezea maji hayo, nao ndio wa kwanza kunaangukia magonjwa hatari ya kuambukiza kama kuhara na kutapika.

Hivyo, muhimu ninaloliona ni kwamba, sote tuwe wastaarabu kuwajali watu wote, kwa kila namna tunavyoweza na mojawapo lipo dhahiri ni hilo la kutasambaza maji machafu kwa makusudi.

Mara zote, magari ya kuchukua maji taka yapo mengi na la busara hapo ni kuwapo utaratibu binafsi au wa kifamilia, kuweza kuyatoa majitaka kwa njia iliyo sahihi na sio kuyafungulia njia, ili yaende kwa wenzako.

Pia ifahamike umma wote unatumia mvua hiyo katika maeneo yao, yakivuka sehemu mbalimbali za mtiririko wake.

Kukabili afya ya mazingira inaanza na namna kila mtu anavyojua miundombinu ya maeneo yako yalivyo, kisha wanayaweka vizuri, ili mvua zikinyesha zisiweze kuleta athari kwa wengine.

Najua kuna taarifa zinazitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa, ikifafanua kila kitu kuhusu ujoo wa mvua na mwenendo wake, hali ya hewa kila juu wa mvua na jinsi ya kujianda au kujihadhari mapema.

Hatua za kuchukua mapema inaanzia pamoja na kuweka vizuri miundombinu, ili mvua zinapoanza kunyesha mtu asipate shida kwenye mwanzo wake.

Cha kushangaza mvua zinaponyesha tu, mtu akiona maji yamejaa kwake, badala ya kufanya utaratibu unaofaa, yeye anachokimbilia ni kuyaelekeza maji yaende katika nyumba ya mwenzake au kwingineko, bila kujali huko kuna umma.

Huyo anayefanya hivyo, anamsababishia mwenzake nyumba yake kujaa maji na aingie gharama za kuyatoa maji tena machafu.

Niseme, kinachotakiwa hapo ni watu waishi kwa upendo na ushirikiano na daima sio busara mtu kuelekeza maji ya mvua kwa makusudi yaingie katika nyumba ya mwenzake asiye na kosa, hali ambayo hata inakinzana na kanuni, sera pia sheria za mazingira.

Kama wewe huyapendi maji hayo yakae kwako, basi nawe usimpelekee mwenzako maji hayo kama tunavyofunzwa kiimani na kijamii, usichopenda kutendewa wewe, usimtendee mwenzako.