Hivi ndugu ilitukosea nini waheshimiwa!

10Jan 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Hivi ndugu ilitukosea nini waheshimiwa!

ENZI za mwishoni mwa ukoloni Tanganyika, tuliokuwa tunasikia na kuelewa na hata tukisikiliza redio za Rising na Phillips, tulizoea kumsikia Mwalimu Julius Nyerere akiita au kuwatambulisha Bwana Edward Twinning au Bwana Richard Turnbull.

Hao walikuwa ni magavana wa mwisho mwisho wa Mkoloni Mwingereza nchini. Lakini hata Nyerere alitambulishwa kama Bwana Julius Nyerere na wenzake au wadogo zake kiwadhifa, alipokuwa mikutanoni na kokote alikotakiwa kutambulishwa.

Nyakati hizo hata wanawake walitambulishwa, kama vile Bibi Titi Mohammed, Bibi Maria Nyerere, Bibi Sophia Kawawa na wanawake wengine maarufu walitambulishwa hivyo tukiona wazee wetu wakikubaliana kabisa na utambulisho huo wa Bwana Fulani au Bibi Fulani.

Baadaye tukaambiwa Bwana ni utambulisho wa mmiliki wa mtumwa, hivyo mtumwa alimwita mmiliki wake Bwana wangu. Kwa kuwa mfumo ulikuwa ni dume, tulisikia Bwana zaidi ya Bibi, huku bibi akibaki kuwa mke wa bwana. Ingawa kwingineko, bibi alikuwa nyanya. Mama wa baba au mama yako.

Kidogokidogo, bibi fulani ikafa, ikabaki mama fulani. Tukaanza kusikia Mama Maria Nyerere, Mama Sophia Kawawa, na kadhalika. Kumbe wenye akili wakawa wanawaza na kuwazua, kuhusu utambulisho huu. Wakauona kama una chembechembe za kikoloni bado. Wakaona kumbe zina chembechembe za kibaguzi pia.

Wenye akili hao, wakaona kuwa kumbe kuitana bwana fulani, kunamaanisha kuwapo utumwa miongoni mwa Watanganyika. Hata baada ya Uhuru mambo yaliendelea hivyo hivyo, bwana na bibi fulani, kabla ya bibi kuwa mama fulani.

Ilipobainika zaidi kwamba kumbe utambulisho huu utatugawa, ikaonekana bora tuitane waheshimiwa. Yaani kiongozi aitwe mheshimiwa fulani bila sasa kujali ni bwana au bibi. Mheshimiwa Julius Nyerere, Mheshimiwa Rashidi Kawawa, Mheshimiwa ikawa mheshimiwa kila mahali. Majaji na mahakimu wakawa waheshimiwa.

Wabunge na madiwani nao wakataka wawe waheshimiwa, kwa kuwa wanatunga sheria za nchi na maeneo, michakato ikafanyika, wakawa waheshimiwa. Mwananchi wa kawaida akabaki mwananchi wa kawaida. Aitwe mheshimiwa kivipi wakati hana cheo wala wadhifa!

Hiyo nayo ikaonekana inaleta utengamano badala ya utangamano. Wenye vichwa vyao wakakaa na kutafakari, wakaona umoja wetu ulioleta uhuru kwa kuunganishwa na Kiswahili, utaparaganyika kama nchi itakuwa ya waheshimiwa na wasioheshimiwa, wakati Katiba inasema kila mtu ana haki ya kuheshimiwa na hivyo ni mheshimiwa, kwa nini sasa wawe wachache nchini. Tunagawanyika ohoo!

Mwalimu Nyerere akaliona hilo, akashauriana na wenzake, wakajiuliza kwa nini tusiitane ndugu? Mbona hilo halina ubaguzi, kwa kuwa sisi ni ndugu na tunaapa kuwa Afrika ni moja na kila mtu ni ndugu yangu! Ikakubalika tuitane ndugu, bila kujali umri, kabila, dini au rangi ya mtu.

Ndugu ikatuunganisha, ikatuheshimisha na kututambulisha kimataifa. Rais wa Tanzania, Ndugu Julius Nyerere, Waziri Mkuu, Ndugu Rashid Kawawa. Ikawa hivyo, mpaka majirani zetu nao tukaanza kuwaita ndugu. Rais wa Kenya, Ndugu Jomo Kenyatta, Rais wa Uganda, Ndugu Milton Obotte.

Kwa kweli Nyerere akaipenda sana, akiitumia sana kila alikohitaji kutambulisha au kuhutubia, isipokuwa kwa viongozi wa dini, Baba Askofu au Shekhe Mkuu. Huko hakutumia ndugu hata kidogo. Alikuwa mnyenyekevu kuliko kawaida.

Ilibaki kidogo tu ndugu iwe utambulisho wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa sababu ilionekana inatuunganisha na kutuheshimisha. Iliishia wapi? Mungu mwenyewe anajua, kwa kuwa tulikuwa na Kiswahili wenzetu wakiwa na makabila.

Mara he, ndugu ikajifia tena, tukasikia wabunge wanataka waitwe waheshimiwa, kama majaji, mahakimu, na madiwani nao wakafuata nyayo. Ikaja kwa maarasii, madisii, madedi, madasi, wenyeviti wa mitaa, mabalozi wa nyumba 10, wakachekelea.

Polepole uheshimiwa huu unaanza kutugawa, wale kule, hawa huku. Wa juu wa juu, wa chini wa chini! Waheshimiwa wanacharaza ndugu bakora hadharani. Wanajua kabisa sheria zinasemaje kwa mkosaji. Wanajua kabisa mahakama zimejengwa kwa minajili gani, lakini wanacharaza tu. Sisi ni ndugu, tujiulize tunakokosea, turudi tuitane ndugu, nyadhifa au vyeo haviondoki kwa kuitana ndugu, ila tunashikamana zaidi. Alamsiki!