Hizi sio dalili njema kabisa kwa vyama vya upinzani

06Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hizi sio dalili njema kabisa kwa vyama vya upinzani

CHAMA cha siasa cha ACT- Wazalendo kimeondokewa na wanachama wake wakiwamo viongozi wa juu hali inayoashiria kwamba huenda kikajikuta katika mazingira magumu iwapo viongozi wake hawatachukua hatua za kukinusuru.

Kwa mara ya kwanza aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

 

Kisha akafuata aliyekuwa Mshauri Mkuu wa chama hicho Prof. Kitila Mkumbo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

 

Katika mwendelezo huo, vigogo wengine akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, Wakili Alberto Msando, Peter Mwambuja ambaye ni mweka hazina Taifa wa zamani na Dennis Chembo aliyekuwa Katibu wa Uadilifu Taifa walihamia CCM.

 

Wapo wengine ambao ni Emmanuel Kitundu ambaye alikuwa ofisa tawala wa zamani makao makuu,Wilfred Kitundu aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa Singida na Lipu Loti Robert aliyekuwa katibu Mkoa wa Singida.

 

Wengine ni Mwantum Mgonja aliyekuwa ofisa wa sheria taifa, Nakamia John aliyekuwa mwenyekiti wa Jimbo la Singida mjini na Dani Olotu aliyekuwa katibu wa zamani Mkoa wa Arusha.

 

Tayari Mwigamba alishasema kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM unaofanywa na serikali ya awamu ya tano unashabihiana na ule wa Ilani ya ACT Wazalendo hivyo hakuna sababu ya kupinga hatua zinazotekelezwa na CCM.

 

Hili ni pigo kubwa kwa chama hicho, hivyo ipo haja kwa Kiongozi Mkuu, Zitto Kabwe pamoja na timu aliobaki nayo kujipanga ili kujiimarisha upya.

 

Waliohama wametumia haki yao ya kidemokrasia ya kujiunga na chama chochote wanachokitaka bila kushurutishwa, hivyo waliobakia ndani ya ACT- Wazalendo wajipange upya.

 

Hali hii pia iko Chadema hasa baada ya kuondokewa na baadhi ya madiwani wake pamoja na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, Lawrence Masha, David Kafulila ambao wote wamejiunga na CCM.

 

Mbali na hao, mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Abdallah Mtulia naye ametangaza kujiuzulu ubunge, nafasi nyingine zote na uanachama katika chama hicho kutokana na kazi kubwa inayofanywa na CCM.

 

Mchambuzi mmoja Abdulkarim Atiki aliwahi kuniambia kuwa taasisi yeyote mpya inapoanzishwa, kwa uhalisia inatakiwa kupitia katika hatua kuu tatu ambazo ni kuzaliwa, kukua na kufa.

 

Akatolea mfano Chama cha ACT kwamba kilipata usajili, baada ya hapo kilitakiwa kukua ikiwa ni kutangaza dhana, itikadi na falsafa kwa wananchi ili kipate uungwaji mkono kwa kufanya mikutano ya hadhara, kufungua matawi, kutambulisha viongozi wake wakuu ili wafahamike zaidi kwa umma na kujenga ushawishi.

 

Mchambuzi huyo akasema kuwa waanzilishi wa ACT- Wazalendo hawakuwa na nia ya dhati ya kuanzisha chama hicho bali kufukuzwa ndiyo ilikuwa sababu kuu, hivyo chama ni zao la mawazo ya kufukuzwa kutoka chama kingine.

 

Akafafanua kuwa kufukuzwa kwa viongozi hao ambao hawajulikani vyema walianzisha mapambano na kule walikotoka wakidhani kuwa wanakitangaza chama chao na kusababisha kupoteza muda.

 

Atiki akasema kuwa hata baadhi ya waanzilishi wake hawakuwa na mapenzi ya dhati na ACT. Walijiweka pembeni huku wakiendelea na ajira zao kwa kivuli cha washauri wa chama na wengine wakisubiri hadi wavuliwe ubunge kwingine ndipo wajiunge na ACT.

 

Kama alichosema mchambuzi huyu ni sahihi kwa asilimia 100, basi Zitto na wenzake waliobaki ndani ya ACT- Wazalendo wanahitaji kujipanga upya ili kuhakikisha chama kinasimama imara.

 

Tahadhari hii isiwe kwa chama hiki tu bali hata vyama vingine vya upinzani ambavyo vinaondokewa na wanachama huku vikidhani kwamba bado viko imara na kumbe vimeanza kutikiswa.

 

Suala la mwanachama kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine ni la kidemokrasia, lakini pia wenye vyama wanatakiwa kuangalia kasoro zilizomo ndani na kuzirekebisha ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea kuongeza wanachama wapya badala kukimbiwa.