Hofu yaweza kukwamisha vita dhidi ya virusi vya corona

04Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hofu yaweza kukwamisha vita dhidi ya virusi vya corona

KABLA na hata baada ya kuingia kwa ugonjwa wa corona nchini, jitihada zimekuwa zikifanywa na serikali na wadau wa afya. Hapo kuna kuelimishana, kujua mbinu mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huo.

Umma unaendelea kuelekezwa namna ya kujikinga uvaaji barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kupaka vitakasa mikono, kutosalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana na pia kutokaribiana.

Magari ya abiria sasa yanabeba kulingana na idadi ya viti, hakuna msongamano, lengo kuhakikisha usalama wa Watanzania, dhidi ya ugonjwa huo unaoendelea kutikisa dunia.

Hata hivyo, kuna sintofahamu itokanayo na baadhi ya watu kujawa hofu, wengine wanashindwa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku.

Wanafanya hivyo, huku wakiwa tayari wameshaelekezwa jinsi ya kujikinga na kuendelea na shughuli zao za kila siku, ratiba zao ziongozwe na umakini wa kulinda afya zao kwa kuzingatia maelekezo waliopewa.

Hofu hiyo, ilishamuibua hata Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni, alipowakumbusha Watanzania watulie na kuwajibikia yaliyo mbele zao.

Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu, kuna ufafanuzi wa neno hofu, kwamba “ni hali ya kutokuwa na ushujaa, woga, jambo linaloleta woga au kitisho, shindwa kukabili jambo lihitajilo vikumbo, kuwa na woga, ogopa, chelea na hatihati.”

Hayo yote ndiyo yanatokana na hofu hadi watu kusahau maelekezo ya kitaifa na kitaalamu kuhusu kujikinga, hata shughuli za uzalishaji mali zinakwama.

Kwa maana hofu haina nafasi tena. Kwani tikizingatia, haya hofu isipewe nafasi, kwa kuwa nao ni ugonjwa mwingine ambao ukiendelea kupewa nafasi unaweza kusababisha mengine, binadamu anaposhindwa kwa sababu ya hofu, hukata tamaa.

Iwapo kutakuwapo kukata tamaa, maana yake ni kuacha maelekezo ya wataalamu wa afya na hivyo kuruhusu ugonjwa huo kuendelea kuchukua nafasi badala ya kuukabili na kuutokomeza.

Ni kweli kila mtu ameumbwa na hofu ndani ya moyo wake, ambayo humsaidia pengine kuepuka vitu hatarishi katika maisha, na hilo haliepukiki katika maisha ya binadamu.

Ukweli ni kwamba kila siku mtu anapatwa na hofu juu ya mambo mbalimbali, kwani ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu, lakini pia imekuwa kikwazo cha mafanikio kwa baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa, hofu hujenga uoga ndani ya mtu na kumfanya ashindwe kuchukua hatua juu ya jambo husika, na ni kikwazo katika mafanikio, hivyo ikiendelea kupewa nafasi, inaweza kukwamisha vita ya virusi vya corona.

Hivyo, wakati huu wa vita dhidi ya virusi vya corona, siyo wa kuweka hofu mbele, badala yake iwekwe pembeni na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kama ambavyo rais amekuwa akisisitiza.

Watanzania pia wanashauriwa kutumia njia za asili za kupambana na ugonjwa huo ikiwamo ya kujifukiza, huku Wizara ya Afya ikiagizwa kufafanua ni namna gani suala la kujifukiza linasaidia kudhibiti corona.

Maana yake ni kwamba kila mmoja ajitahidi kadri inavyowezekana kujikinga na ugonjwa huo huku akizingatia kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kupaka vitakasa mikono na kutosalimiana na kukumbatiana.

Hayo yakifuatwa bila kuwapo kwa hofu, huku mbinu mbalimbali za kujiweka salama zikizingatiwa, ukiwamo suala la kumuomba Mungu, taifa linaweza kuendelea kuwa salama.

Karibu watu wote wanatambua kuwa virusi vya corona vipo, lakini visiwajaze hofu hadi kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku, bali wazingatie tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya.