Hoja hii ya usafi, kujali watoto tuungane nao viongozi wa dini

07Mar 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hoja hii ya usafi, kujali watoto tuungane nao viongozi wa dini

JUZI viongozi wa dini nchini, walitoa tamko la kukubali kushirikiana na serikali kukabiliana na ulinzi na usafi wa mazingira kwa watoto, kutokana na madhara yanayoendelea kuwapo.

Makubaliano yao ni kwenda kuwahamasisha waumini kupitia mahubiri, ili wafahamu umuhimu wa kulinda watoto na kuishi katika hali ya usafi wakati wote, kuwaepusha watoto na matatizo ya afya, kama kudumaa katika makuzi yao.

Muungano huu ni mzuri, kwa kuwa unagusa afya za wananchi moja kwa moja na kwenye nyumba za ibada, ndiko ambako wanapaamini, wanasikia na kutii sauti za viongozi wao. Maana yake, sasa tutarajie mabadiliko makubwa.

Hakuna ubishi, lipo tatizo kubwa la usafi wa mazingira kwenye mitaa mbalimbali ya miji mkubwa na mdogp. ambalo kwa kiasi kikubwa, limesababishwa na watu kushindwa kutekeleza wajibu wao na ukosefu wa miundombinu bora ya kuhifadhia taka, kupitisha na kuteketeza taka hizo.

Kauli ya viongozi wa dini katika kupaza sauti, itakuwa na nguvu zaidi, iwapo tu watashirikiana na mamlaka za kiserikali. Vinginevyo, hali itaendelea kuwa ile ile, kwa kuwa wakati mwingine, utatuzi huo unahitaji nguvu ya serikali.

Mathalani, masoko ya jiji la Dar es Salaam, ni chanzo cha uchafu na uondoshaji wa taka haufanyiki inavyotakiwa, huku kukiwa na sababu mbalimbali ambazo kimsingi siyo za msingi sana.

Mfano katika kila soko wachuuzi hulipa ushuru wa Sh. 500 kila siku na wapo wakusanyaji wa fedha hizo ambazo huenda Manispaa ambazo wakati mwingine mapato ya soko hufikia Sh. bilioni moja kwa mwezi, lakini fedha inayotengwa katika kuondosha takataka ni ndogo sana na wakati mwingine hakuna.

Kwa ujumla masoko ni machafu sana, magari ya takataka ambayo yalitakiwa kuwapo kila siku hukosekana hata kwa wiki moja na matokeo yake taka kuwa nyingi, mbaya zaidi kazi hiyo inafanywa na manispaa zenyewe.

Ukitembelea baadhi ya masoko, utajiuliza kwanini hali inaendelea kuwa hivi kwa kuwa kuna uchafu mwingi ambao siyo salama kwa afya za wauzaji na wanunuzi? Hakuna miundombinu muhimu na hakuna jitihada za haraka katika kuhakikisha masoko, yanakuwa ni sehemu salama.

Kwenye masoko hayo kuna watoto ambao wameambatana na mama zao kusaka riziki ya siku, moja kwa moja wanajikuta kwenye mazingira hatarishi na usalama wa afya zao upo hatarini.

Kwa ujumla, matamko ya viongozi wa dini liende sambamba na Manispaa kuchukua hatua ya kuleta mabadiliko kwenye masoko, yanayobeba mamilioni ya watu wakiwa wanunuzi na wakati huohuo wauzaji.

Eneo jingine ni uondoshaji wa takataka kwenye mitaa mbalimbali ambalo limeonekana kushindwa licha ya mbinu mbalimbali kutumika ikiwamo kutumia vijana maalum kukamata wanaochafua mazingira.

Mitaani, hakuna magari ya kuondosha takataka, matokeo yake takataka zinazozalishwa hutupwa sehemu mbalimbali nyakati za usiku, na hakuna jitihada za serikali za mitaa kuhamasisha wananchi kuchanga kwa ajili ya gari au wabeba taka.

Kama uondoshaji wa takataka kwenye nyumba za watu unashindikana na muumini huyu ndiye aliyekutana na mahubiri ya kiongozi wa dini akimataka kushiriki usafi wa mazingira katika kulinda afya za watoto, lakini hakuna pa kuhifadhi takataka bali zinazagaa.

Kwenye maeneo yenye taka, ndiko ambako watoto hupita au kucheza, hivyo kuokota ambavyo kwa uwezo wa akili zao wanaona vinafaa, lakini kiuhalisia ni hatari kwa afya zao.

Manispaa ya Moshi inahesabu mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika usafi wa mzingira kwa kuwa wameshirikiana kwa pamoja na Manispaa, mamlaka za serikali,viongozi wa dini, siasa na wananchi kusema hapana kwenye uchafu.

Wasifu kama huo wa usafi nao unaonekana kwa miaka mingi, katika Manispaa ya Iringa.

Mara nyingi, nimezuisikia manispaa na mamlaka nyingine za miji, zikienda huku kujifunza ili kuboresha na hata Manispaa za Dar es Salaam zilishakwenda kujifunza, lakini bado mabadiliko hayajaonekana, bali tunaona nyakati za mvua watu wanatoa mafurushi ya taka kwenda kurusha kwenye mitaro.

Eneo jingine ni chemba za majitaka ambazo mara nyingi hutiririsha majitaka kwa muda mrefu, jambo linaloleta madhara ya afya, kama mlipuko wa kipindupindu na magonjwa mengine.

Uamuzi wa viongozi wa dini unapaswa uungwe mkono, ili kuhakikisha serikali na wananchi wanakuwa kitu kimoja, kuhakikisha usafi wa mazingira ni utamaduni ya kila mmoja, kama ilivyowezekana Manispaa ya Moshi na kwingine itawezekana.