Hongera CHAMUDATA, mna kazi kubwa

14May 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera CHAMUDATA, mna kazi kubwa

HATIMAYE Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania kimepata viongozi wake watakaokiongoza kwa kipindi cha muhula mwingine, baada ya kupita miaka mingi bila ya kuwa na viongozi.

CHAMUDATA, chama kikongwe cha muziki nchini Tanzania, kilionekana ni kama kimekufa, kama ni kubebwa zaidi na Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Hassan Msumari ambaye ilionekana kama yeye ndiye kila kitu, Mwenyekiti, Katibu na vyeo vyote. Kwa kiasi kikubwa anastahili sifa, kwani bila yeye sidhani kama hata baadhi ya watu wangejua kama kulikuwa na chama hicho.

Mwanamuziki, mwimbaji wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Luiza Mbutu, ndiye Mwenyekiti mpya wa chama hicho kwenye uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mwanamuziki, mwimbaji na mtunzi wa bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra, Abdallah Hemba, yeye alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti, huku nafasi ya Katibu Mkuu, ikienda kwa Katibu wa bendi ya Msondo Ngoma Music Band, Said Kibiriti.

Kuna wajumbe sita waliochaguliwa, na kwa kweli nitoe pongezi kwa waliotengeneza katiba ya chama hicho, kwani haikuwataka au kuwapendelea wanamuziki tu, bali hata wadau na wapenzi wa muziki wameruhusiwa kugombea.

Ndiyo maana hata baadhi ya Waandishi wa Habari za muziki na burudani kama Said Mdoe na wengineo wamechaguliwa kwenye nafasi ya ujumbe.

Hii inaonyesha kuwa chama hicho kinatambua kuwa ili muziki wa dansi uendelee si lazima kiongozwe na wanamuziki tu, bali hata wadau mbalimbali, wanaofanikisha kuutangaza na kuuenzi muziki huo.

Nilisikia kuwa moja kati ya mikakati ni kulinda maslahi ya wanamuziki wa dansi, ikiwemo kufuatilia mirabaha yao.

Hii ni kweli, chama sasa kinatakiwa kuendeshwa kisasa. Nyimbo hazipigwi redioni tu au kwenye mabaa, bali hata kwenye mitandao ya kijamii.

Muziki kwa sasa umehamia kwenye mitandao ya kijamii na huko ndiko hasa inatakiwa akili za viongozi zielekezwe na si kuzuia bendi ndogo kupiga laivu nyimbo za bendi zingine kubwa.

Nilisikia eti chama kinaambiwa kipige marufuku bendi ndogo kupiga nyimbo za bendi kubwa. Hii haipo duniani kote.

Wanamuziki wote unaowaona wakubwa, walianza kwanza kuiga kuimba na kupiga nyimbo za bendi na wanamuziki waliotangulia ndiyo wakawa hapo walipo.

Hata nchini Congo DR, JB Mpiana alianza muziki kwa kuiga nyimbo za Papa Wemba. Wenge Musica kwa miaka 10 wakati ikiwa bendi ndogo ilikuwa ikipiga nyimbo za kina Tabu Ley, Franco, Papa Wemba, Debaba na wengineo.

Hakuna bendi yoyote duniani inayoweza kupiga muziki mwanzo hadi mwisho bila kupiga muziki wa bendi nyingine. Nadhani Luiza, na wenzake kwa sababu ni wanamuziki, wanalifahamu hilo. Acheni bendi ndogo na wanamuziki kupiga na kuimba nyimbo za watu wengine majukwaani, ili mradi tu wasirekodi.

Chama kina kazi kubwa ya kufanya kuliko hilo. Ni kuwarudishia kujiamini wanamuziki, pia kuiangukia serikali angalau kutengeneza studio, au ile ya TBC Dar na Dodoma, kuwapa unafuu wanamuziki wa dansi kurekodi kwa makubaliano maalum, kwani inavyoonekana tatizo kubwa la bendi za muziki wa dansi ni gharama ya kurekodi. Na ukiangalia hata studio wanazorekodi kwa sasa nadhani si nzuri, inawezekana ni za kurekodia muziki wa kisasa zaidi, kwani nyimbo za dansi hazitoki kwenye ubora kama ule wa nyimbo za zamani ambapo vifaa vilikuwa duni.

Nina uhakika kama bendi zitarejea kurekodi TBC, ambao wana studio zilizokamilika, kwa makubaliano maalum, muziki unaweza kurejea tena kwenye chati. Ni chama tu kukaa na serikali kushauriana, zirekodi bure kwa makubaliano ya kulipana watakapokuwa wanauza albamu zao.

Hiyo ndiyo kazi ya kufanya kwa Chamudata, ikiwemo sasa kuwa na mfuko wa kuwasaidia wanamuziki kama vile matibabu makubwa, siyo homa, maralia na tumbo, kifo, au matatizo ya kibinadamu mfano msaada kama wa kisheria kama akipatwa na tatizo lolote.

Mfuko huu unatakiwa kuchangiwa na wanamuziki wote wanachama wa Chamudata, lakini pia watengeneze mazingira pia ya wanamuziki au wadau ambao si wanachama wanaotoa michango yao pia kusaidiwa.

Wanamuziki wengi walionekana kujitokeza kwenye uchaguzi, hii inaonyesha kuwa wanataka sasa mabadiliko na wanataka kuona chama chao kinafanya mambo ambayo hata wao watajivunia kuwa nacho, pia watajivunia kuwa wanamuziki au wadau wa muziki.