Hongera ofisi kijiji kufanikisha maendeleo kwa wakazi staili hii

15Jan 2021
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera ofisi kijiji kufanikisha maendeleo kwa wakazi staili hii

OFISI za vijiji zina wajibu wa kutumia fursa walizo nazo katika vijiji ili kutatua changamoto katika maeneo yao.

Hapo kuna wawekezaji wanakuja kuwekeza na hao wakitumiwa vizuri wanaleta maendeleo makubwa katika maeneo yao.

Kama ofisi za vijiji vitajikita kusimamia vizuri vyanzo vya vyake vya mapato, ni haki inayokifanya hata kijiji kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Uzoefu unaionyesha kuna baadhi ya vijiji havina maendeleo, lakini ukiangalia upande wa pili wa shilingi, ni mahali panapofanyika uwekezaji mkubwa.

Hapo ndipo penye hatua inayozaa swali, inakuwaje kijiji kilichobeba sifa kamili kinakosa sura na mwonekano wa kukosekana maendeleo, wakati kuna wawekezaji wa kutosheleza mahitaji.

Kinachotakiwa hapa ni viongozi husika wa vijiji kukaa pamoja na kushirikiana na wawekezaji, ili kuhakikisha maeneo yenu sahihi yanasonga mbele katika tija ya maisha.

Tunafahamu kuwa daima wawekezaji kabla ya kuingiza mitaji yao katika sehemu zetu, wanakubaliana na kijiji kuhusu vitu vya kimaendeleo, ambavyo watakifanya kwa faida ya wanakijiji.

Pia hata ofisi ya kijiji inaweza kutumika rasilimali za kijiji kwa ajili ya kutatua kero za wananchi na sio kila kero ikatatuliwe na serikali. Hapana! Lazima kuwa na mikono yetu walau kwa asilimia fulani.

Tukumbuke kuwa, serikali mambo mengi ya kimaendeleo ya kufanya, lakini kuna vitu vidogo ambavyo hata kijiji kinaweza kufanya na kumaliza bila kuitegemea serikali.

Ni hivi karibuni Ofisi ya Kijiji Mwanambaya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ilitenga fedha Sh. milioni 20, kwa ajili ya kutatua kero ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya msingi Mwanambaya.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Leila Chaburuma, ana mtazamo kwamba wana mtazamo kuwa wameazimia kutenga Sh. milioni 20 kupitia mapato ya ndani ili kujenga madarasa mawili.

Anaongeza kwamba, mbali na kujenga vyumba vya madarasa, pia wamejipanga kutatua changamoto ya madawati na madarasa katika vyumba hivyo.

Ofisi hiyo katika namna yake, inampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Injinia Mshamu Munde, kwa kuwajengea darasa moja katika shule hiyo na kufanikiwa kukabidhiwa mwezi uliopita.

Nilivutiwa na hoja kwamba, Mhandisi Munde aendelee kuiangalia shule hiyo kwa jicho la huruma, kwa kuendelea kuisaidia kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi, ambao wanatoka katika vijiji mbalimbali.

Anasema, kijiji hicho kupitia ofisi yake kimeridhia kujenga jengo la mama na mtoto kwenye Zahanati yao Mwanambaya, huku wakijiandaa kujenga wodi ambayo itawawezesha kukabiliana na ongezeko la wagonjwa kutoka katika vijiji vya Mwanadilatu na Mipeku.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Jumanne Bofu, alilipongeza Shirika la Songas kufadhili ujenzi wa nyumba pacha ya Mganga Mfawidhi  wa zahanati hiyo, ilipokabidhiwa mwezi huu.