Hongera TAMWA, miaka 30 ya mapambano si mchezo

03Sep 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Hongera TAMWA, miaka 30 ya mapambano si mchezo

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Novemba 17, mwaka huu kinaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, mwaka 1987.

Jina la TAMWA limepata umaarufu mkubwa si ndani ya nchi bali hata nje ya nchi kutokana na juhudi zake za kutetea haki za wanawake na watoto.

Utafiti wa kihabari uliofanyika katika sehemu mbalimbali nchini kwa kushirikisha waandishi wa habari, ulisaidia kuibua mambo mengi ya ukatili wanaofanyiwa watoto na wanawake na hatimaye serikali kuchukua hatua.

Matokeo ya utafiti huo yalisaidia hata taasisi za serikali katika taarifa zake kunukuu takwimu za utafiti uliofanywa na TAMWA.

Mpaka kinapata umaarufu huo, chama hicho kimevuka mabonde na milima na kuhimili mikikimikiki mingi bila kukata tamaa hata pale wanachama walipovunjwa moyo.

Wakati chama hicho kikianzishwa, watu walikuwa na mitazamo tofauti hasa kwa kuzingatia waanzilishi walikuwa na waandishi wa habari wanawake, kutokana na mfumo dume uliojengeka tangu enzi za mababu na mabibi.

Hata hivyo, TAMWA kupitia vyombo vya habari na kampeni mbalimbali ilizofanya, kimeleta mabadiliko katika sheria, sera na mitazamo ambazo zilimnyima mwanamke haki stahiki.

Wananchi walipata taarifa mbalimbali na elimu kupitia habari nyingi zilizoripotiwa na chama hicho kupitia habari zake za uchunguzi zilizoibua mambo mengi yaliyojificha ya ukatili wanaofanyiwa wanawake na watoto.

Katika harakati zake za kutetea haki za wanawake na watoto, kupitia magazeti, radio na televisheni, mwaka 1998, TAMWA ilishiriki katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA), ambayo ilirekebishwa tena mwaka 2005.

SOSPA ilikuwa na ajenda ya kitaifa kupitia Muungano wa wadau kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali 50 (FEMACT), na TAMWA iliongoza harakati za kuleta mabadiliko hayo katika sheria hiyo na kwa mara ya kwanza sheria hiyo ikatamka kuwa ukeketaji ni kosa la jinai, ikampa mtoto wa kike ulinzi wa kutofanyiwa ukatili akiwa chini ya umri wa miaka 18.

Katika kushinikiza mabadiliko ya sheria hiyo, TAMWA kwa kushirikiana na wanaharakati wa kupinga unyanyasaji huo, ulipiga kambi bungeni mjini Dodoma, kupiga kampeni kwa wabunge ili wapitishe mabadiliko hayo.

Pamoja na changamoto ya kukosa fedha za kukaa hotelini, wanaharakati hao hawakujali, bali walijenga mahema na kulala humo ili lengo lao liweze kutimia.

Marekebisho mengine ya sheria yaliyowahi kufanyika kwa juhudi za chama hicho ni Sheria ya Ardhi ya mwaka 1923 na ya mwaka 1999, kwa vifungu vyote kumwezesha mwanamke kumiliki ardhi sawa na mwanaume.

TAMWA ambayo ina wanachama pia kwa upande wa Tanzania Visiwani (Zanzibar), ilisaidia kuleta mabadiliko kwenye Sheria ya Spinster ambayo ilimtaka mtoto wa kike aliyepata mimba chini ya umri wa miaka 18 afukuzwe shule na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, wakati mwanaume aliachwa huru kutokana nakutokua na kifaa cha kupimia vinasaba (DNA).

Marekebisho yalifanyika katika sheria hiyo kwa kufutwa kifungo kwa mtoto wa kike na mwanaume aliyempa mimba anawajibishwa kwa kutoa matunzo ya mtoto hadi atakapofika umri wa miaka 18.

Katika kuelekea maadhimisho hayo ya miaka 30, TAMWA imeandaa harambee kwa ajili ya kujenga Kituo cha Usuluhishi Nasaha na kituo cha matangazo ya online ya televisheni.

Lengo ni kuhakikisha chama hicho kinafanyakazi zake kwa ufanisi zaidi na wananchi wapate huduma iliyo bora.

Unyanyasaji wa kijinsia hauwahusu wanawake na watoto pekee, bali hata wanaume wanapata ukatili huo, lakini wanaogopa kujitokeza kwa kuona aibu.

TAMWA imekuwa ikiwahudumia watu wote bila kujali jinsi ya mtu na watu wengi wamepata haki baada ya mashauri yao kupatiwa ufumbuzi.

[email protected]; Simu: 0774 466 571