Hongera TFF kuwahisha Ligi Kuu mapema

02Jul 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera TFF kuwahisha Ligi Kuu mapema

KATIKATI ya mwezi uliopita niliandika kwenye safu hii kulitaka Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kupitia Bodi ya Ligi kuanza ligi  ya msimu ujao mapema.

Niliandika hivyo kutokana na kuwa na wasiwasi kuwa msimu ujao huenda Ligi Kuu ikachelewa kuanza.

Kwa sababu ya msimu huu ilichelewa kuanza na imechelewa pia kumalizika. Ilianza Septemba 27 na kumalizika Juni 29.

Nilitoa sababu za kutaka TFF kupitia Bodi ya Ligi kwanza kabisa kuisaidia timu ya taifa, Taifa Stars ili iwe sawa kwa ajili ya mechi ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali AFCON zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini, Ivory Coast.

Ndiyo, kuisaidia kwa sababu baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Algeria na sare ya bao 1-1 dhidi ya Niger, Taifa Stars itacheza tena mechi yake ya tatu dhidi ya Uganda, Septemba 19 mwaka huu.

Sasa kama ligi ya msimu uliomalizika ilianza Septemba 27, basi mechi hiyo ingeweza kuikuta Stars ikiwa na wachezaji ambao hawajaanza ligi.

Ni kipindi ambacho wachezaji watakuwa bado hawako fiti, kwani wengi watakuwa wanajitafuta kwa sababu ya kutoka kwenye mapumziko marefu. Hata kocha jinsi ya kuchagua itakuwa shida.

Nikashauri tu angalau ligi ianze katikati ya mwezi Agosti, ili mpaka mechi ya Uganda inafika, tayari wachezaji wameshaanza kuchanganya, na hata unaweza kuwapata wachezaji wapya ambao wameonyesha viwango bora.

Kwa sababu hizi na zingine nitakazoziandika, nikaitaka TFF na Bodi yake kuangalia uwezekano wa ligi msimu ujao kuanza mapema kabla ya Septemba, vinginevyo tutakuwa tumeumia kwenye maandalizi ya kwenda AFCON.

Inawezekana kabisa kuwa mawazo niliyoandika kwenye safu ile yameonekana na majuzi Bodi ya Ligi imetangaza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2022/23 utaanza Agosti 17 na kumalizika Mei 27 mwakani.

Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo akabainisha kuwa ligi ilichelewa kumalizika kutokana na janga la virusi vya corona.

Lakini nimkumbushe Kasongo kuwa siyo kuchelewa kumalizika, hata kuanza ilichelewa kwani si mara nyingi Ligi Kuu inaanza Septemba 27, badala yake huanza Agosti.

Na hii yote kama alivyosema ilisababishwa na ugonjwa wa COVID-19, unaosababishwa na virusi vya corona.

Niwapongeze TFF na Bodi ya Ligi kwa kuwa wasikivu na kufanyia kazi mawazo au ushauri wote unaotolewa na wadau mbalimbali wa soka, wakiwemo waandishi wa habari, watangazaji na wachambuzi pia.

Kwa kuanza Agosti 17 mpaka kufika Septemba 19 ni mwezi mzima, hivyo angalau wachezaji watakuwa wameshajiunga na timu zao, wameshafanya mazoezi magumu ya kujenga miili yao kwa ajili ya purukushani za msimu mzima, lakini kizuri zaidi watakuwa wameshacheza angalau mechi mbili au tatu za Ligi Kuu. Hii inatosha sana kuwaweka vema na kwenye hali ya utimamu watakapokwenda kuitumikia timu ya taifa.

Pia kuanza kwa ligi mapema kutazisaidia timu nne za Tanzania zitakazokwenda kucheza mechi za  Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Najua timu ya Simba itaanza kucheza Oktoba raundi ya kwanza na yenyewe ndiyo itakayonufaika zaidi kwa sababu itacheza mechi nyingi za Ligi Kuu hadi mwezi huo itakapoanza kampeni zake, lakini angalau timu za Yanga, Azam na nyingine itakayopatikana zitakuwa zimecheza mechi kadhaa za ligi kabla ya kuanza hatua ya awali.

Hii itazisaidia kwani wachezaji wao watakuwa wameshaanza kuzoeana na kupata mikiki ya ligi kabla ya kwenda kwenye michuano hiyo migumu.

Tuliona misimu kadhaa nyuma, ligi ilipochelewa kuanza na timu kuanza michuano ya kimataifa kabla ya ligi zikatolewa.

Simba ilitolewa na UD Songo ya Msumbiji kwa sababu ilicheza mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa ligi ya Tanzania ikiwa bado haijaanza, hivyo kuwa na tatizo la muunganiko na wachezaji kutozoeana.

Simba ilianza kucheza michuano hiyo, ikiwa ugenini Agosti 10, 2019, zikatoka suluhu na  mechi ya marudiano ikapigwa Agosti 25, 2019 na kutoka sare ya bao 1-1, ikatolewa kwa goli la ugenini.

Ligi ya msimu huo ilianza siku ya pili baada ya Simba kucheza mechi ya marudiano Agosti 26, yenyewe ikianza kucheza Agosti 29 dhidi ya JKT Tanzania.

Ni mechi iliyowaumiza mno wanachama na mashabiki wa Simba, lakini ukiiangalia kiundani timu hiyo ilicheza bila kuwa na mechi sahihi ya ushindani kwa sababu ya kuchelewa kwa ligi.

Kwa hili ni lazima nitoe pongezi kwani Bodi ya Ligi na TFF si tu inaongoza soka, lakini inajali maendeleo yake, mawazo na maoni ya wadau pia.