Hongereni wazazi, walezi kwa uchangiaji huu wa vyakula shuleni

24Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongereni wazazi, walezi kwa uchangiaji huu wa vyakula shuleni

ELIMU bora ina faida kwa maisha ya kila mmoja na inachangia ukuaji wa uchumi, na ndiyo maana serikali katika nchi nyingi zinazoendelea na zilizoendelea elimu ni kipaumbele katika mipango ya maendeleo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, kwani serikali imeipa kipaumbele sekta ya elimu ikiwamo kutoa elimu bure kuanzia elimumsingi hadi kidato cha nne ili kuhakikisha kila mtoto anaelimika.

Pamoja na juhudi hizo, kumekuwapo na changamoto mbalimbali zinazochangia baadhi ya shule kuwa na ufaulu usioridhisha, utoro na mambo mengine yanayokwamisha maendeleo ya watoto shuleni.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau wa elimu wamekuwa wakifanya kila njia kuhakikisha wanatoa mchango wa maoni na mawazo yenye lengo la kuinua kiwango cha elimu kwenye maeneo hayo.

Mfano mmojawapo ni , wadau wa elimu wa mkoa wa Mara, ambao mwisoni mwa mwezi uliopita walikutana na kujadili changamoto zinazokwamisha kupanda kwa ufaulu katika shule za msingi na sekondari.

Katika mkutano huo, wadau hao waliibuka na maazimio nane, ambayo wanaamini kwamba ikitekelezwa, itasaidia kupandisha ufaulu na pia kumaliza changamoto nyingine zinazozikabili shule za umma.

Miongoni mwa maazimio hayo ni wazazi kuchangia shuleni kama njia kudhibiti utoro na kuongeza ufaulu, kwa vile mwanafunzi anapokuwa ameshiba anaweza kufuatilia kikamilifu masomo darasani.

Jingine ni kuwapo kwa uhusiano mzuri kati ya walimu na wazazi kama njia mojawapo ya kufuatilia kwa karibu mienendo ya wanafunzi wawapo shuleni na nyumbani ili kama kunakuwapo na tatizo hatua zichukuliwe haraka.

Baada ya maazimio hayo, baadhi ya wazazi wameanza kutekeleza la kuwapo kwa chakula shuleni ili kuhakikisha watoto wao wanakipata wawapo shuleni badala ya kusubiri hadi warudi nyumbani jinoni.

Wazazi hao ni wa Shule za Msingi Chirorwe na Sokoine zilizopo katika kijiji cha Chirororwe, Halmashauri ya Wilaya Musoma, ambao wiki iliyopita walichanga tani 5.6 za mahindi na maharage.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halamshauri ya Wilaya ya Musoma, John Kayombo,wanafunzi wa shule hizo mbili watatumia tani hizo za mahindi na maharage kwa muda wa mwaka mmoja.

Wazazi wamechanga mahindi na maharage kwa kuwa chakula shuleni kinakuza ufaulu wa wanafunzi, kinaboresha afya zao na kupandisha kiwango cha ufaulu.

Tatizo ambalo baadhi ya wazazi wanalo ni kuamini kwamba shule za umma siyo zao na wanadai kwamba serikali ilishatangaza kutoa elimu bure, hivyo hawahusiki kuchangia chakula shuleni!

Kuna haja ya kuwatoa katika mawazo hayo na kutambua kuwa shule za umma ni zao na wao ndiyo umma wenyewe na pia waache kukariri bali watambue wanatakiwa kuzihudumia shule hizo.

Huduma hizo ni pamoja na kuchangia chakula cha wanafunzi ili wapate angalau mlo mmoja wawapo shuleni, kuliko kushinda njaa, hali ambayo inasababisha wasiwe na usikivu wa masomo wawapo madarasani.

Kwa wale wao Mkoa wa Mara, wazazi wa kijiji cha Chirorwe wameonyesha mfano, ambao ni muhimu ukaigwa na wengine mkoani humo ili kuhakikisha kila shule inakuwa na chakula.

Hii inatokana na umuhimu wa chakula, ambao kimsingi ni vigumu wanafunzi kufuatilia masomo kwa umakini iwapo hawajapata chochote kuanzia asubuhi hadi mchana au jioni.

Ninajua wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya biashara ndogo kama mihogo ya kukaanga kwenye maeneo ya shule, lakini bado haiwezi kumuondolea njaa mwanafunzi.

Vilevile si wanafunzi wote ambao wanapewa pesa na wazazi au walezi kwa ajili ya kununua vitu hivyo shuleni, kwa hiyo jambo la msingi ni wazazi kuchangia chakula shuleni.

Yawezekana vipo baadhi ya vijiji ambavyo vimeanza kutimiza azimio hilo la kuchangia chakula shuleni mkoani Mara, lakini wakazi wa kijiji cha Chirorwe taarifa zao zimewekwa wazi ndiyo maana ninawatolea mfano.