Huduma ya afya bure ni muhimu kwa makundi haya

08Nov 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Huduma ya afya bure ni muhimu kwa makundi haya

MOJA ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wazee ni ile ya kukosa huduma ya afya bure, kama inavyoelekeza Sera ya Afya na kusababisha kundi hili kukumbana na usumbufu usio wa lazima.

Wazee wamekuwa wakikumbana na usumbufu kwa sababu wanapofika hospitali wakiamini kwamba wanaweza kupata huduma ya matibabu bure, lakini hujikuta wakikwama na hivyo kuwekwa katika wakati mgumu.

Kwa mujibu wa sera hiyo, wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa kupata huduma ya afya bure wanapokwenda hospitalini.

Sera hiyo ya mwaka 1990 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2009, inayatambua makundi hayo kwenye jamii kwamba yanatakiwa kupata matibabu bure kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali.

Licha ya kuwapo kwa sera hiyo, utekelezaji wake umekuwa ni mgumu na kusababisha makundi hayo kukosa huduma hiyo, kitendo ambacho kimekuwa chanzo cha malalamiko ya mara kwa mara karibu kila kona ya nchi.

Kumekuwa na malalamiko kupitia vyombo vya habari kuwa walengwa wa sera hiyo hasa wazee, ambao hudai kukosa huduma za matibabu wanapokwenda kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali, huku wakitakiwa kulipia gharama za huduma hiyo.

Wamekuwa wakidai kwamba wanapokwenda kupata huduma hiyo huambiwa kuwa hakuna dawa na badala yake wanaandikiwa vyeti na kutakiwa kununua dawa kwa fedha zao!

Kama dawa hakuna, wakati makundi hayo yakitakiwa kutibiwa bure, kwa nini wasipewe fedha za kununulia dawa hizo ili kutimiza matakwa ya sera hiyo inayolenga kuwapa huduma za matibabu bure?

Mbali na kukosa huduma hiyo, wamekuwa wakidai kukalishwa kwenye mabenchi ya vituo vya afya kwa muda mrefu bila kuhudumiwa na mwisho wake wanaambiwa hakuna dawa.

Makundi hayo yanadai kwamba, pale wanapokuwa na barua kutoka kwa watendaji wa vijiji na kata, zinazoyatambulisha, barua hizo zimekuwa hazitambuliwi na baadhi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Ikumbukwe kuwa malalamiko haya ni ya muda mrefu na hata baadhi ya wabunge walishawahi kushauri kwamba ni bora kwenye vituo vya afya, zanahati na hospitali kuwe na dirisha maalum la kutolea fedha za kununulia dawa.

Maana yake ni kwamba mzee anapokosa dawa, basi aende dirishani apewe fedha za kununulia dawa hizo badala ya kuambiwa akajinunulie wakati hana uwezo kifedha.

Binafsi ninaunga mkono ushauri huu kwa sababu na sera inasema wazi kwamba, makundi haya yanatakiwa kupata huduma bure, hivyo kuyatoza fedha za matibabu ni kwenda kinyume na sera yenyewe.

Wakati serikali ikiendelea kujipanga vizuri ili kuweka dawa za wazee, wajawazito na watoto wanaoguswa na sera hiyo, basi iweke fedha kwenye zanahati, vituo vya afya na hospitali ili wanapoandikiwa dawa, wapewe fedha wakanunue.

Sera hii iliwekwa kwa kutambua kuwa makundi haya haya yanahitaji kupata huduma ya afya bure, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha walengwa wanapata haki hiyo bila usumbufu kama ilivyo sasa.

Ninaamini kwamba kwa kasi ya serikali ya awamu ya tano, hakutakuwa na kigugumizi tena na badala yake ni utekelezaji kwa vitendo utafanywa kwa kasi ya hapa kazi tu.

Kama ambavyo serikali imekuwa ikipunguza na kubana matumizi, basi itafanya hivyo hata huku kwenye afya na kuelekeza nguvu katika kuhakikisha hakuna tena malalamiko kuhusu huduma bure kwa makundi haya yaliyoanishwa na sera.

Nakumbuka wizara husika ilishawahi kukiri kwamba changamoto, ambazo makundi hayo yamekuwa yakikumbana nazo zinatokana na baadhi ya wahudumu katika hospitali za umma kutofahamu kwa undani sera hiyo.