Huenda ni zama za ACT- Wazalendo kutamba upinzani

27May 2020
Ani Jozen
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Huenda ni zama za ACT- Wazalendo kutamba upinzani

WAKATI bunge linapokaribia mwisho wa shughuli zake tunapoelekea mwezi ujao, macho na masikio yanaanza kuhamia kwenye uchaguzi mkuu ambao mwaka huu unaweza kufanyika katika mazingira tofauti.

Ni kuogopa kutokana na uwepo wa ugonjwa wa corona, hivyo kuweka vizuizi vya mikusanyiko ya watu, kulingana na hali itakavyokuwa hadi kipindi cha kampeni kikianza rasmi mwezi Agosti.

Hata hivyo kinachoangaliwa sasa ni jinsi watu wanavyojipanga kugombea, na hasa wabunge waliopo sasa.

Utafiti kuelekea uchaguzi mkuu unaonyesha kuwa kuchaguliwa tena katika nafasi ya ubunge si kazi ndogo, na tatizo siyo nguvu ya vyama vya upinzani ila uwezo wa mbunge husika kuwaridhisha wapigakura kuwa bado ndiye mtu sahihi kwa nafasi hiyo. Wapigakura hawana hulka ya kuchagua vyama, licha ya kampeni za miaka mingi za wanaharakati wa vyama vingi, kuwa mfumo wa viti kutokana na uwiano wa kura ndiyo utaleta demokrasia halisi.

Uchaguzi mkuu ujao hautakuwa rahisi kwa wagombea kutoka vyama vya upinzani kwa upande mmoja, na labda zaidi ya ilivyokuwa awali, hata wabunge kutoka CCM watakuwa na wasiwasi zaidi pia.

Katika kila uchaguzi mkuu kuanzia mwaka 1995, kunakuwa na chama cha upinzani ambacho kwa wakati huo kinakuwa kimejiandaa vyema zaidi kuliko wengine, hasa kwa kunasa viongozi wa kitaifa wenye mvuto kwa wapigakura.

Mwelekeo huu siyo rahisi kusema kama utafikiwa katika uchaguzi mkuu ujao au la, lakini zipo dalili kuwa ACT-Wazalendo wako tayari au wana uwezo wa kisaikolojia wa kujiandaa kupokea mtu maarufu atakayepeperusha bendera yao kwa mafanikio zaidi. Ni mtu anayemzidi ‘kimo’ kiongozi wa kitaifa Zitto Kabwe, avute wapigakura.

Kwa upande wa pili, unaweza kusema hakuna uwezekano wa Chadema kupata mgombea wa aina hiyo, baada ya kufarakana na kada wa CCM, Edward Lowassa, ambaye baada ya kukatwa na CCM aliendeleza ‘safari ya matumaini’ Chadema, hata hivyo hakuiva kiitikadi na chama hicho na akaondoka.

Kuibuka kwa Chadema kulifuatia kudorora kwa Chama cha Wananchi (CUF) baada ya uchaguzi mkuu 2005 ambako ilikuwa na matumaini makubwa kushinda urais Zanzibar na wabunge wengi. Ikatokea kuwa mgombea mwenza wa Chadema asiyefahamika Zanzibar na kwa kawaida ni mkazi wa Bagamoyo, Jumbe Rajab Jumbe, akafariki dunia siku nne kabla ya kupigwa kura, Zanzibar wakaendelea na upigaji kura lakini Bara ukaahirishwa hadi Desemba 4.

Maalim Seif alipotangazwa kushindwa Zanzibar, wafuasi wa CUF wakakosa ari Bara, na wengi hawakujitokeza kupiga kura, hivyo mgombea wa CCM akapata kura kwa asimilia 80.

Baadhi katika CCM wakatafsiri kuwa ndiyo kiwango halisi cha kupendwa chama hicho hasa kutokana na kura ya maoni ya mwaka 1991 kuhusu mfumo wa vyama vingi, ambako asilimia 80 walitaka chama kimoja, huku asilimia 20 wakipendekeza vyama vingi.

Ni kama waliotaka mfumo wa chama kimoja kimsingi wapo CCM, wakati mpangilio wa matokeo ya uchaguzi mkuu tangu mwaka 1995 yanaonyesha kuwa CCM ilikuwa inaungwa mkono kwa takriban asilimia 70 katika maeneo ya vijijini, au chini ya asilimia 50 kwa maeneo ya mijini. Hivyo wagombea upinzani wakawa wanashinda mijini tofauti, na maeneo machache zaidi vijijini.

Hali hii inaboreshwa pale upinzani unapopata kiongozi wa kitaifa anayejulikana apewe bendera ya chama kimojawapo aipeperushe, watu waone kuwa ni mbadala halisi na wenye uwezo wa utawala ukilinganisha na rais aliyeko madarakani.

Hivyo hadi sasa alikuwapo Augustine Mrema mwaka 1995 wa NCCR-Mageuzi na Lowassa 2015, na 2010 Chadema ilikuwa na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa kitaifa wa taasisi kubwa ya dini.

Kwaupande mwingine, licha ya kukimbiwa na makada waandamizi kuanzia pale uchaguzi mkuu 2015 ulipokamilika, kwani makada wake ndiyo waliovutiwa zaidi na uzalendo wa utendaji wa awamu ya tano (hasa katika kutumbia majipu, hata kabla ya suala la makinikia), Zitto Kabwe hajawahi kuwa na migogoro ndani ya chama.

Anao washindani wake ambao walirudi CCM ila walifanya hivyo kutokana na mazingira na siyo malumbano ndani ya chama. Kwa njia hiyo anaweza akavuna kiwango kikubwa zaidi cha kuaminiwa na wapiga kura wa upinzani na hata wanaotaka kugombea ubunge ikiwa ni pamoja na waliopo Chadema, hasa kama atavuta kiongozi wa kitaifa anayejulikana ‘kupimana ubavu’ na JPM. Ndiyo taswira inayojengeka sasa.