Huu ndio mwiba wa maadui watatu

03Nov 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Huu ndio mwiba wa maadui watatu

BAADA ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, ilitangazwa vita dhidi ya maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi ya umaskini, lakini hadi sasa maadui hao bado wapo.

Historia inaonyesha kuwa wakati nchi inapata uhuru, idadi kubwa ya watu waliokuwa hawajui kusoma na kuandika walikuwa ni wale ambao hawakubahatika kwenda shule pekee, lakini kwa sasa hata wanaokwenda sekondari bado wapo wasiojua kusoma na kuandika!

Serikali ya awamu ya tano ilishatangaza kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtoto wa Mtanzania anapata elimu na hakuna mzazi au mlezi atakayeleta kisingizio cha kukosa ada.

Ukweli ni kwamba adui mmoja ambaye ni ujinga akimalizika, hawa wengine ambao ni maradhi na umasikini watakwisha, kwa sababu elimu ndio inayomuwezesha mtu kupambana na maadui hao.

Ikumbukwe kuwa utawala wa awamu ya kwanza, hasa mwanzoni mwa miaka ya 70 uliazimia kuondoa ujinga ukiamini kwamba watu wakielimika itakuwa ni rahisi kupambana na maradhi na umaskini.

Hatua hiyo ya kupambana na ujinga ilienda sambamba na watoto wenye umri wa kwenda shule kuanza darasa la kwanza na pia kuanzishwa madarasa ya elimu ya watu wazima.

Madarasa hayo, ambayo yalikuwa yakifanyika saa za jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, yalikuwa kichocheo kwa ajili kuwaondolea wananchi umbumbumbu ili waweze kuepuka maadui hao.

Nimeanza kuelezea kidogo kile ambacho kilifanywa na utawala wa awamu ya kwanza kwa lengo ya kupambana na maadui hao, ambao kimsingi bila kuondoa huyo wa kwanza hawa wengine wataendelea kuwapo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa baada ya kuanzishwa kwa madarasa ya watu wazima, kati ya mwaka 1974 hadi mwaka 1975 serikali ilifanikisha kuandikisha wasiojua kusoma na kuandika kama milioni 4.5 kwenye madarasa ya elimu ya watu wazima.

Serikali ilitambua na kuamini kuwa nchi yoyote yenye watu wasiojua kusoma na kuandika ni kama mfu, kwani watu wake hawatakuwa na uwezo wa kumudu mazingira yanayowazunguka wala kuzalisha mali na badala yake watageuka kuwa watumwa au tegemezi.

Miaka ya hivi karibuni serikali ilishawahi kukiri kwamba imebaini kuwapo kwa wanafunzi 5,000 waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2012 wakiwa hawajui kusoma na kuandika jambo ambalo ni la kushangaza kwa karne hii ya sayansi na teknolojia.

Aidha, takwimu za sensa ya mwaka 2002 zilibainisha kuwapo watu wazima 22,500,000 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea sawa na asilimia 56 ya idadi ya watu wote, kiasi cha ujinga kilifikia asilimia 70.

Ongezeko hili la kiwango cha ujinga lilikuja kipindi ambacho ni miongo mitatu sasa, tangu kuanzishwa kwa sera ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa wote (UPE), kwa upande mmoja, pia Elimu ya Watu Wazima kwa upande mwingine.

Maana yake ni kwamba, elimu ya watu wazima au ‘kisomo chenye manufaa’ kilikuwa ni nguzo muhimu katika kufikia maendeleo ya haraka kwa mtu mmoja mmoja na hata taifa kwa ujumla.

Ninadhani sasa ipo haja ya kujipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kurejesha elimu ya watu wazima kwa kuwalipa walimu posho zinazofaa, kwani kwa namna moja au nyingine ukosefu wa posho unaweza kuchangia walimu kukata tamaa ya kufanya kazi hiyo.

Nimejaribu kuelezea kwa kirefu zaidi lakini lengo ni kutaka kuzungumzia juhudi zinazofanywa na Rais Dk. John Mafufuli ya kupambana kwa dhati ili kuwatokomeza maadui hawa ambao walitangazwa mara tu baada ya nchi kupata uhuru.

Kama nilivyoeleza mwanzoni, serikali ya awamu ya tano inaendelea kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtoto wa Mtanzania anapata elimu.

Kwa mfumo huu ni rahisi kila Mtanzania kupata elimu, cha msingi ni kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata elimu kwani ikiwa hivyo hakutakuwa na haja ya kuwapo kwa elimu ya watu wazima, kwa sababu kila mmoja atakuwa amesoma.

Lakini kutokana na changamoto mbalimbali za maisha, inawezekana wakawapo wale ambao hawakubahatika kwenda shule, hivyo elimu ya watu wazima inatakiwa kuwapo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Binafsi ninaamini kuwa kwa mwendo huu wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa elimu bure ni wazi kwamba adui ujinga anaweza kumalizika na kuwafanya maadui wale wawili kutoweka haraka miongoni mwa Watanzania.

Kinachotakiwa ni kila mmoja wetu kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali hii za kuhakikisha kila mtoto wa Mtanzania anapata elimu ili imsaidie kumudu mazingira yanayomzunguka.