Huu unaweza kuwa ukomavu wa kisiasa

11Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Huu unaweza kuwa ukomavu wa kisiasa

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemfukuza uanachama kada wake aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Bernard Membe, kwa kukiuka maadili ya chama.

Mbali na kumfutia Membe uanachama, kamati hiyo pia ikatoa karipio kwa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa kukiuka maadili ya chama, lakini kumsamehe Yusuph Makamba kwa makosa kama hayo.

Wakati adhabu ya Membe ikiendelea, CCM inasema milango ya kuondoka kwa hiari yao, kuwapokea wanachama wapya na waliofukuzwa wakienda kuomba radhi, wote kwa pamoja iko wazi.

Kwa hatua hiyo, CCM inasema kuwa kada wake huyo aliyefutiwa uanachama wa chama hicho, anaweza kuomba radhi akarudishwa kundini kuungana na wanachama wenzake.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kwamba chama kinasubiri kuona barua ya kuomba radhi kutoka kwa Membe, hivyo katibu huyo hawezi kuanza kubwabwaja kana kwamba hana picha pana.

Pengine kauli ya Dk. Bashiru inaonyesha kuwa anatambua kwamba kila binadamu ana upungufu yake na kila mtu ana maeneo, ambayo amebarikiwa kuwa na uwezo wa kuyaelewa na mengine hana.

Vilevile penye wengi ni lazima tofauti zitakuwapo tu ila jambo la msingi ni wahusika kusaidiana ili waendelee kuwa kitu kimoja, lakini suala la nidhamu ni muhimu zaidi ili kuwekana sawa.

Hali ikishafikia hapo kama hiyo ya kumfuta mtu uanachama, kama ana mapenzi na chama, kinachofuata ni kuomba radhi ili arudishwe kundini kama ambavyo katibu anasema.

Kwenye suala la kuomba radhi, wapo baadhi ya watu ambao wamejaliwa busara na hufikia kuomba hata kama hawajafanya kosa, lengo likiwa ni kuepusha malumbano yasiyo na msingi.

Hivyo ni nafasi ya kada huyo kutafakari kwa kina akitambua kuwa hata vikombe havina miguu, lakini siyo ajabu vikagongana kabatini, hivyo suala la kutofautiana lipo, lakini lisipewe nafasi ya kugawa wanachama.

Ikumbukwe kuwa wapo baadhi ya makada wa CCM ambao waliowahi kutimuliwa katika chama hicho, kisha wakaomba radhi na kurejeshwa kuendelea kukitumikia chama kama kawaida.

Kuomba radhi na kusamehewa ni jambo muhimu, kwa sababu hakuna binadamu aliyekamilika, na kwa kutambua hilo, ndiyo maana katibu huyo anasisitiza kuwa milango iko wazi kwa makundi hayo yote.

Chama ni wanachama na bila wanachama hakuna chama, hivyo akiondoka mwanachama mmoja au kufukuzwa, idadi ya wanachama inapungua, hivyo si jambo la kufurahia pale mwanachama anapoondoka au kufukuzwa.

Kutokana na ukweli huo, Dk. Bashiru anakemea wanachama kutosherehekea hatua zilizochukuliwa za kumfutia uanachama kada wao Membe kwa vile kumpoteza mwanachama ni msiba.

Inawezekana kinachosemwa na katibu huyo ni ukomavu wa kisiasa na hasa kwa kutambua kuwa siasa siyo uadui na pia kutofautiana kimtazamo, kimawazo ni jambo la kawaida.

Kwamba kada wao amekwenda kinyume na taratibu za chama na kufutiwa uanachama, lakini pia chama kimeweka milango wazi ili akitafakari kisha akarudi kuomba radhi, basi anapokelewa.

Hatua hiyo inaonyesha hakuna chuki yoyote, ila mara nyingi wapambe ndiyo huwa wanadaiwa kushabikia na kuongeza chokochoko pale tofauti kama hizo zinapojitokeza ndani ya chama.

Lakini inaonekana Dk. Bashiru amewashtukia, ndiyo maana anaweka wazi kwamba wanachama wasisherehekeee Membe kufutwa uanachama bali watambue kuwa kuondokewa na mwanachama ni msiba.

Matarajio yake ni kwamba ipo siku Membe atarudi CCM na kuungana na wanachama wenzake, kwa vile milango ya kuwapokea wanachama wapya, walioondoka kwa hiari na waliofukuzwa na kuomba radhi iko wazi.

Kauli ya katibu huyo inaonyesha kukomaa kisiasa juu ya uendeshaji wa chama, katika dhana na misingi ya demokrasia, uwazi kwenye ushiriki wa wanachama kukitumikia na kufanya maamuzi muhimu.

Utaratibu wa mwanachama kufutiwa uanachama, lakini bado akapewa nafasi nyingine ya kuomba radhi ili arejeshwe kundini kuendelea kuwatumikia wananchi ni wa mfano wa kuigwa.

Wapo baadhi ya makada wa CCM ambao waliowahi kutimuliwa katika chama hicho, kisha wakaomba radhi na kurejeshewa, utaratibu kama huu inaimarisha umoja ndani ya chama.