Ibada hizi za mizimu ‘kiwazimu’ zidhibitiwe

04May 2021
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ibada hizi za mizimu ‘kiwazimu’ zidhibitiwe

HIVI karibuni kuna video iliyozunguka kwenye mitandao kadhaa ya jamii, iliyowaonyesha  familia ya watu wanane waliotembea kilometa kadhaa bila mavazi, wakidai wanafanya hivyo kuitii mizimu.

Kutokana na tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa, alilazimika kuitembelea familia hiyo iliyotajwa kuwa ni ya  Seleman Mpange, mkazi wa Kijiji cha Lukulunge katika Manispaa ya Morogoro, kujua kulikoni.   

Watu wanane wa familia hiyo wakiwamo baba, mama na  watoto na mkwe kwa pamoja walivua nguo na kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tatu asubuhi ya Aprili 7, mwaka huu, wakidaiwa kuwa wanatekeleza masharti ya mizimu ya ukoo huo.

 Baba wa familia, Mpange baada ya kuhojiwa  na Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa ameamua kufanya hivyo ili kutii masuala ya mizimu, mila na desturi za ukoo wao.

Mkuu wa Wilaya alishauri suala hilo kuzungumzwa kifamilia ili kubaini ukweli wa jambo hilo wakiwashirikisha wazee wa kimila.

Kwa upande mwingine uamuzi huu ni mzuri  ingawa kulingana na taharuki waliyoisababisha kwenye jamii haitoshi kuchukua maamuzi hayo, hatua zaidi zilihitajika ili kuifunza jamii kuishi maisha yenye maadili.

 Masuala ya  dini yanayohusishwa na imani za  kiroho ni jambo ambalo halipingwi kwani kila mtu ana haki ya kuabudu imani yake, lakini serikali haina dini licha ya kwamba imekuwa ikihusika katika kusimamia masuala ya dini zote.

Lengo la serikali ni kujiridhisha kuwa dini zinaendeshwa katika misingi ambayo havunji amani ya nchi wali haivurugi ustawi wa taifa.

 Ni wazi kuwa kila mtu ana uhuru wa kuchagua dini anayoipenda zikiwamo za jadi kutegemea na jinsi imani ya familia yake au maamuzi yake ama alivyovutika na taratibu za kuabudu zinazotumika.

Kitendo walichofaya familia hiyo ni wazi kuwa kilitumia vibaya uhuru uliopo wa kuabudu kulingana na maadili ya nchi hii, pia ilisababisha kuvunja heshima yao na kuweka kumbukumbu mbaya ya watoto wao kwenye jamii kutokana na kutembea utupu.

Tumeshawahi kusikia visa kadhaa kwenye dini mbalimbali duniani, vikiwamo vinavyohusu viongozi wa madhehebu ya dini hizo kushawishi waumini wao kutenda mambo ambayo yanasababisha fedheha, mateso hadi vifo.

Nchini Uganda miaka kadhaa iliyopita  kiongozi mmoja wa dini aliyetambulika kwa jina la Kibwetere alisababisha vifo vya waumini wake kwa kuwasha moto akiwaaminisha kuwa ndiyo mwisho wa dunia lakini alitoweka na hakuwa pamoja nao na kusababisha vifo vya maelfu.

Hivyo kuna umuhimu wa  kudhibiti dini ama madhehebu mbalimbali hasa wa kuwa mafundisho yanatofautia kulingana na njia za ufundishaji.

Jambo lingine ni kuwa kutokana na sayansi na teknolojia tukio hilo tayari limehifadhiwa  hivyo limeweka kumbukumbu mbaya ya kudumu kuhusu familia hiyo, ambayo inaweza kuwagharimu watoto  wao  ikiwamo hata kuwakosesha amani na fursa mbalimbali.

Kwa mujibu wa andiko liliopo kwenye kitabu cha Falsafa ya Sanaa Tanzania (Baraza la Sanaa la Taifa 1982) inabainishwa kuwa  tambiko ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na jamii za Tanzania.

 Ni ni ibada inayohusisha kuipa mizimu heshima na sadaka ili jamii inayohusika ipate amani, kwa kuzingatia kanuni za ibada hizi hazikuruhusu watu kumwendea Mwenyezi Mungu moja kwa moja hivyo hupitishia maombi yao kwa mizimu, sadaka kwa njia ya tambiko, ni ili ifurahi, itulie, ipate kuyafikisha maombi ya watambikaji kwa Mwenyezi Mungu na kumsihi ayakubali.

Hata hivyo, uhuru wa kuabudu usitumiwe vibaya na kusababisha jamii kupatwa na aibu kwa kujiingiza kwenye mambo ambayo hayana tofauti na yale yanayofanywa na watu wasio na elimu wa maarifa ya kutambua kuwa kutembea bila mavazi ni hatia si mbele ya sheria bali hata kwa jamii inayowazunguka.