Ijue haki ya notisi kwa mpangaji

27Jul 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Ijue haki ya notisi kwa mpangaji

KUNA matatizo jamii kati ya wapangaji na wenye nyumba, kuhusu notisi ya kuondoka au kuondolewa katika nyumba. Wako wanaosema notisi ni ya mwezi mmoja, pia wako wanaosema ni ya miezi mitatu.  Kama ni kweli au vinginyevyo, tuone sheria husika inasemaje?

Masuala ya pango yanaongozwa na  sheria  kuu  mbili.  Moja Sheria ya Ardhi Namba 4 ya  mwaka  1999;  pili  Sheria  ya  Mikataba  Sura  ya  345.  Kwa pamoja sheria hizo zote kwa mapana, husimamia jambo husika.

Mkataba wa Pango

Mkataba wa pango, unahusisha makubaliano ya upangaji  kati  ya  mwenye  nyumba  na  mpangaji  au  mpangaji  na  mpangaji  mwingine  wa  pili.  Pango linaweza kuwa kwa ajili ya chumba/nyumba ya kuishi, biashara, nyumba ya ibada au hata shughuli nyinginezo za kibinadamu. Yote hayo, kwa ujumla ndiyo yanayokamilisha maana ya neno pango.

Aina za mikataba

Sheria ya Ardhi, 1999 (Kifungu cha 78 na 79) inatambua mikataba ya upangaji ya muda mrefu na kwa vipindi vifupi. Inatambua pango la wiki, mwezi, miezi, mwaka na miaka.  Imetoa uhuru kwa wahusika wenyewe  kuamua  ni  muda  gani  wangependa  kuingia  mkataba.

Katika  vitu  muhimu  sana  katika  suala  la  pango,  ni  notisi ya kuondoka   au  kuondolewa  katika  pango.  Jambo  la  kuzingatia awali  kabisa,  ni  kuwa   notisi  hii  ni  muhimu  pande  zote  mbili.

Upande wa  mwenye  nyumba  na  upande  wa  mpangaji.  Kila mmoja kwa  nafasi  yake  anawajibika  kutoa  notisi  kwa  mwenzake,  penye mahitaji  ya  kuondoka  au  kuondolewa.

Ikumbukwe  kuwa, notisi  si  kwa  ajili  tu  ya kuondoka  na kuondolewa,   bali  yanapotokea mabadiliko  yoyote  katika  masharti  ya  mkataba. Hiyo  ina  maana  kwamba, hata  kuongeza  kodi, kupanga  kukagua  nyumba, kufanya  marekebisho, notisi inaaa itolewe.

Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 haijatamka moja kwa moja kuhusiana na suala la notisi ya kuondoka au kuondolewa iwe ya muda  gani. Kinachohitajika na cha muhimu au lazima, ni kuhakikisha notisi inatolewa katika   muda   unaokadirika na kuingia akilini, wataalamu wa sheria.

Hivyo, notisi inaweza kuwa ya muda wowote isipokuwa uwe unaokadirika na kuingia akilini.

Ili kuenenda kiungwana, mhusika anafaa aangalie muda wa pango uliopo katika mkataba. Kwa mfano, mtu mwenye mkataba wa miaka  mitano,  hawezi  kupewa  notisi  ya kuondoka  ya   mwezi  mmoja  au  hata miwili.

Lakini,   kwa mwenye mkataba wa miezi minne au mitatu, unaweza  kupewa  notisi  hata ya  mwezi  mmoja.  Hali kadhalika, wa  mwaka,  notisi ya miezi  mitatu  inaweza  kuwa  sahihi.

Muhimu ni Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, haijataja wazi wazi muda hasa wa notisi ya kuondoka, hivyo ni  vyema  sana  kuhakikisha  mkataba wa  pango unaeleza  muda  wa notisi.

Inalaezwa kwamba, ni muhimu sana, endapo muda utafika mwenye nyumba anataka chumba au nyumba yake au ikiwa mpangaji anahitaji kuondoka.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo, muda wowote wahusika watakaokuwa wamekubaliana unatosha  na  unakubalika  kisheria,  kwa sababu  unatokana na  hiari  za  wahusika.

Isitoshe, mhusika asikubali kusaini mkataba ambao hauelezi muda wa notisi. Hatua hiyo itamwepusha na masahibu ya baadaye.

Tabia hiyo ni kosa kwa mujibu wa taratibu za kisheria, hususan ile ya mikataba: Kifungu cha 73 (1), inasema ikitokea hivyo, basi mwenye nyumba lazima atawajibika kumlipa fidia mhusika, yaani mpangaji wake.

Ni kosa ama kuvunja au kusitisha mkataba wa pango kama ilivyo kuvunja mikataba mingine yoyote kinyume na taratibu za sheria.

Mwisho, jambo hilo ni tofauti kidogo, na pale mpangaji anapoamua kuondoka yeye mwenyewe katika chumba/nyumba kabla ya mkataba kwisha. Mwenye nyumba hatowajibika kwa chochote au lolote lile, zaidi labda akifanya ni uungwana tu. Naomba kuwasilisha.