Imara ya chombo ni nanga

12Jan 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Imara ya chombo ni nanga

‘NANGA’ ni dude zito kama jiwe au chuma linalofungwa kwa kamba na kutoswa majini lizuie chombo kisichukuliwe na maji au kujongeajongea. Maana yake chombo cha majini kama vile jahazi hakiwezi kuwa imara bila ya nanga.

Methali hii huweza kutumiwa kumnasihi mtu anayetaka kufanya kazi inayohitaji kiasi fulani cha pesa kuwa anapaswa kuwa na kiasi kinachotakikana ili kazi yake itengemae (kuwa sawasawa kama inavyotakikana).

Leo wanachama wa Yanga watapiga kura kuchagua viongozi wao. Jambo muhimu wanalopaswa kujua wagombea ni kwamba uongozi ni madaraka anayopewa mtu ya kusimamia au kuongoza shughuli. Hapa ‘shughuli’ ni kuiamsha Yanga kutoka usingizini ili kuiletea maendeleo ya jumla. Maana yake klabu ijitegemee badala na kuwa tegemezi kama ilivyozoeleka.

Wapo wagombea walioahidi kuiletea klabu maendeleo kama wakichaguliwa. Wamesema mengi ya kufurahisha lakini hilo lisiwapumbaze wanachama kwani kampeni ni shughuli zinazofanywa na wagombea kuwashawishi wanachama wawape kura.

Katika hili, wanachama wanapaswa kuwa makini sana kwani wameahidiwa mambo mengi yanayowezekana na yasiyowezekana!
Lazima wamkatae mgombea yeyote aliyetoa rushwa ili achaguliwe.

Ni wazi mgombea kama huyo hatainufaisha klabu bali atainufaisha nafsi na familia yake kwa kuinyonya klabu! Mgombea anayetaka kuisaidia klabu kwa nini atoe rushwa? Yashangaza sana kama mtu anakuja kwako ‘kuomba’ akusaidie na kukubembeleza kwa hela ili ukubali! Mtu anapotaka kutoa msaada kwa mwingine hamwombi bali humsaidia tu.

Kwa ufupi mgombea anayegawa rushwa kwa wapiga kura ili wamchague hafai kuwa kiongozi wa ngazi yoyote. Wengine wametoa ahadi nyingi kuwa wakichaguliwa watafanya haya na yale kumbe mtu huchongewa na ulimi wake.

Watakaochaguliwa wanapaswa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni. Nawashauri wamtafute mtu mwenye hatimiliki ya nyumba ya Yanga iliyo kwenye makutano ya barabara za Mafia na Nyamwezi ili aikabidhi klabu. Kama akikataa, klabu imfungulie mashitaka mahakamani ili aeleze alivyoipata na kama aliyempa yu hai, naye afikishwe mahakamani kueleza sababu za kufanya hivyo.

Klabu ikifanikiwa kupata hatimiliki, viongozi wajitahidi kuomba mkopo wa benki ili kujenga jengo la biashara itakayofaa eneo lile. Pili wajitahidi kutafuta eneo la kujenga viwanja vya mazoezi na mashindano.

Kwa hali ya Dar es Salaam ilivyo, wasubiri wakati wa masika ndio watajua sehemu inayofaa kujenga viwanja hivyo, hosteli ya wachezaji, ukumbi wa michezo ya viungo, zahanati na ukumbi wa majadiliano na mafunzo ya ubaoni kati ya makocha na wachezaji.

Twataka viongozi wenye wivu na maono ya maendeleo badala ya viongozi wa kujinufaisha kwa mgongo wa klabu. Viongozi watakaoifanya Yanga kuwa klabu ya hisa itakayokuwa ya hisa na kuijenga klabu itakayojitegemea yenyewe kama zilivyo vilabu vingine duniani.

Jambo lingine ni ukarabati wa makao makuu ya klabu pale Jangwani. Panaweza kubadilishwa na kuwa sehemu nzuri ya ofisi za klabu, eneo la mikutano ya viongozi na wachezaji. Chini kuwe na duka la kujihudumia la vyakula na vifaa (supamaketi). Lile eneo wanalogombea kujenga uwanja, litengenezwe ili kuwa eneo la kuegesha magari baada ya kulijaza udongo/mchanga na kumwagwa zege.

Viongozi watakaochaguliwa leo wafanye kila linalowezekana ili kuigeuza klabu kuwa ya kisasa, inayojitegemea yenyewe badala ya kuwa tegemezi. Ikiwezekana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atumike kukagua matumizi ya fedha kila mwaka na itapendeza kama akikamatwa atakayetuhumiwa kutumia vibaya fedha za klabu na kupelekwa gerezani ili kuwa fundisho kwa wengine.

Itabidi iwe hivyo kwani kuna baadhi hugombea ili kujinufaisha kwa kuinyonya klabu. Ni aibu kwa klabu iliyoanzishwa miaka 83 iliyopita kuendelea kuwa tegemezi kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na wanaoshughulikia usafi na ulinzi!

Kwa upande mwingine, Shirikisho la kandanda Nchini (TFF) lapaswa kuvisaidia vilabu visivyoweza kujitegemea kwa kuvitafutia kampuni zitakazozifadhili kwani tangu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Vodacom zijitoe, hali imekuwa ngumu.

Kama Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 yashindwa kulipa mishahara ya wachezaji, fedha za usajili na benchi la ufundi ikoje kwa vilabu visivyokuwa na wanachama wengi kama Yanga na Simba?

Nashauri viongozi watakaochaguliwa kufanya ziara za mara kwa mara kwenye matawi yao wakianzia Dar es Salaam na kwingineko nchini. Lengo ni kuwaelimisha wanachama na kuwavuta mashabiki kuwa wanachama na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kuiendesha klabu yao kwa mafanikio.

Wakati hayo yakitendeka, viongozi pia wajitahidi kuwa na kituo maalum cha kuwaandaa wachezaji wadogo watakaokuwa hazina ya baadaye kwa klabu badala ya kutumia milioni kadhaa za hela kila msimu kusajili wachezaji kutoka nnje ya nchi. Hii yaweza kuisaidia nchi kuwa na timu bora kuliko ilivyo sasa.

Vijana hao wakiwa na bidii, huenda wakasajiliwa na timu za nnje. Huko watapata ufundi zaidi na baadaye kuisaidia Tanzania kwenye mashindanao ya kimataifa.

Kadhalika klabu yaweza kuwa na duka lake litakalouza vifaa vya michezo mbalimbali zikiwemo jezi zake, skafu, bendera, kanga zenye rangi na picha za majengo ya Yanga, picha za wachezaji, mwalimu na viongozi kwa ajili ya kumbukumbu.

Zote hizi zitaiingizia klabu fedha za kuiwezesha kujiendesha bila shida endapo watachaguliwa viongozi wenye maono (picha au taswira ya vitu au mambo yanayomtokea mtu akilini mwake) ya maendeleo.

“Mkokoto wa jembe si bure yao.” Mkokoto ni alama inayoachwa na kitu kilichoburutwa. Maana yake mtu anayeshinda akilima au akifanya kazi ya kulima japo polepole hakosi kuambulia kitu.

Methali hii hutumiwa kutunasihi tujibidishe kufanya kazi hata kama ni kwa hatua za polepole, hatimaye tutafanikiwa.

[email protected]
0784 334 096