Inakuwaje tunagombea urembo bandia unaokaribisha saratani?

27Feb 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Inakuwaje tunagombea urembo bandia unaokaribisha saratani?

KATIKA muundo wa afya ya mwanadamu, ngozi ni kiungo kimojawawapo muhimu.

Kama ilivyo pande nyingine za mwili wa binadamu, hata wanyama ngozi inaundwa na seli zinazozaliwa, kukua na kufa kila kukicha, katika mfumo wa asili unaojiendesha.

Nini vinaathiri chembehai? Hivyo vinatajwa kuwa msongo wa mawazo, jua kali, ukosefu wa mlo mzuri, kutokunywa maji ya kutosha, kujichubua, umri mkubwa, uchafu, vipodozi visivyo salama, magonjwa, maambukizi ya maradhi na kujeruhiwa.

Inaelezwa vitu hivyo vikitokea kwa kiasi kidogo hudhoofisha seli za binadamu na vikiondolewa, hujijenga upya kurudia hali ya kawaida.

Inapotokea kwa kiasi kikubwa au kuendelea kuwapo kwa muda mrefu hali hiyo, inadhoofisha zaidi seli na kuziua kabisa, hata kuharibu ngozi ya eneo hilo. Nadharia rasmi na tafiti zinazoendelea zinasema hivyo.

Kumekuwapo mtindo na tabia ya kuingiza nchini vipodozi vyenye kemikali hatari, licha ya serikali kupiga marufuku kutokana na madhara yake kwa watumiaji.

Imekuwa kawaida kusikia serikali imeteketekeza vipodozi feki kwenye mkoa fulani, lakini bado vinaendelea kuingizwa nchini, licha ya madhara yake kujulikana na kutangazwa zaidi ya mara moja.

Wapo Watanzania wanaoingiza vipodozi hivyo kwa njia za panya na kuziuza katika maduka ya dawa za binadamu na wengine katika njia nyinyine za kinyemela mitaani, bila ya kujali madhara yaliyopo.

Ni kilio kisichokoma. Nadhani umefika wakati wale wanaopenda ‘kujichubua’ wajali afya zao kwanza, kuliko urembo huo wenye madhara. Waachane na uthubutu wa kutumia vipodozi feki vilivyopigwa marufuku, kuingizwa nchini.

Inadaiwa, wapo wanaopenda urembo wakiwa wamefika hatua ya kujitengenezea mchanganyiko wa tindikali za maji ya betri ya gari, dawa za meno na sabuni ya unga, ili kupata mkorogo maalum wa kujipaka.

Ni hatari wanayoiendekeza. Hivyo, jambo la msingi ni kuzingatia matumizi ya vipodozi vilivyothibitisha kwamba havina madhara, kuliko kung'ang'ania urembo unaoishia hatarini.

Katika harakati zinazofananishwa na hayo, kuna anayedaiwa kuwa mdau wa nyendo hizo, alikamatwa mkoani Pwani, akiangukia tuhuma za kusafirisha shehena za vipodozi feki.

Kwa tukio hilo na mengine ya aina hiyo tunayosikia kutoka maeneo mbalimbali nchini, ni ishara kwamba vipodozi feki bado vina wateja wengi, ambao huenda bado hawajatambua madhara yake au elimu sahihi haijatua vichwani mwao.

Kimsingi, vipodozi feki ni muuaji aliyejificha kwenye urembo, ambaye jamii itakapomwelewa vyema na kumwepuka, itakuwa njia mojawapo ya ushindi.

Tunapozungmzia njia ya ushindi, ujumbe unasimama katika dhana kwamba, umuhimu wa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa kuhusu hatari ya matumizi ya kemikali hizo.

Siyo vyema kuendelea kukumbatia dhana potofu ya kwamba ‘kuwa mweupe ni urembo.’ Hilo ndilo limewafanya baadhi ya wapenda urembo, kutumia vipodozi vyenye madhara kwa kipaumbele cha urembo, bila ya kujali afya zao?

Ikumbukwe, madhara ya awali ya vipodozi hivyo huonekana kwa mtumiaji kwa kubabuka ngozi, kuwa na mabaka meusi au ngozi kuwa nyekundu, lakini utakuta bado anaendelea kutumia pasipo kushtuka kengele ya umma inayojaribu kuiwamamsha.

Watumiaji urembo wanapaswa kutambua, serikali inapopiga marufuku matumizi ya vitu hivyo, inavitambua kitaalamu kuwa vina madhara kwa binadamu.

Ni bahati nzuri, elimu sahihi inatolewa kwa umma wananchi wake na tena bahati nzuri elimu inatolewa kwa umma, ambao baadhi yao ni wazito kunasa somo.

Ni wazi, elimu na ushauri unahitajika zaidi kuwatoa katika mazingira hayo ambayo ni hatari kwa afya zao, hata wakatambua ‘weupe wa bandia’ siyo urembo bali madhara kiafya.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Georgia, Atlanta nchini Marekani, Kelly Lewis, alisema wanawake wengi nchini wanajihatarisha kuugua saratani kupitia vipodozi, pia kukaribisha madhara kwa watoto kuwa na mtindio wa ubongo.