Inakuwaje tunavipa ujumbe mchafu vyombo vya moto?

11Jan 2018
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Inakuwaje tunavipa ujumbe mchafu vyombo vya moto?

NIMEONA nilizungumzie hili la kuwepo baadhi ya vyombo vya usafiri vinavyoandikwa majina yasiyofaa na yenye upotoshaji mkubwa wa maadili. Binafsi nayaita ujumbe mchafu?

Nimeona niseme hivyo, kwa sababu ukikuta baadhi ya vyombo vya moto vina majina yasiyofaa hata kuyatamka, lakini wahusika wanaona ni mazuri na fahari.

Ukweli wake, majina hayo hayana hata manufaa kwa jamii. 

Utakuta Bajaji imeandikwa majina yasiyo na maana, kiasi hata ukipishana nalo, unajisikia kero au hata hasira kutokana na maneno yaliyoandikwa. 

Ni vizuri vyombo vyetu vya usafiri tuviandike majina yanayokubalika, kuliko kuandika majina yasiyo na maadili kwa taifa na vizazi vyetu. 

Hata hao wanaoletewa vyombo hivyo kuviandika, hawawaulizi lina maana gani au kazi yao ni kuchukua pesa tu? 

Tuna mambo mengi ya kujifunza kupitia lugha zetu, kwa manufaa ya taifa na jamii na sio kuviharibu vizazi vyetu, kwa hizo lugha zisizo na maadili. 

Tukumbuke kuwa baadhi ya shule za bweni, kila moja linakuwa na jina la mtu au nchi. Hiyo inamsaidia mwanafunzi kujua hili, jina la huyo mtu limewekwa katika bweni na inaelezwa maana yake. 

Kutokana na mabweni mengi kuwa na majina ya viongozi au watu mashujaa, walimu wanawaelimisha wanafunzi kuhusu hayo majina.

Hata bweni likiwa na jina la nchi fulani,  napo mwanafunzi anapata elimu kujua  hiyo nchi ipo wapi na ilifanya kitu gani kwa taifa. 

Lakini vyombo vya moto baadhi vina majina mabaya ambayo hatuoni kama vina msaada wowote kwa jamii kujifunza. 

Wazo langu ni kwamba, vyombo vyetu tuviandike majina yenye manufaa kwa vizazi vyetu na taifa na sio kuandika majina yasiyo na faida kwa jamii.

Pia, mamlaka zinazosimamia usalama barabarani katika ngazi tofauti, zinapaswa kutunga sheria ndogo za kuwadhibiti wamiliki wa vyombo vya moto wanaobandika majina yasiyofaa, ili wachukuliwe hatua. 

Ushauri wangu ni kwamba, kuna majina ya busara kama vile wilaya, mkoa na mambo mengine muhimu tunayoweza kuyatumia na yakasambaza ujumbe muhimu katika vyombo vyetu vya moto.

 

Suala la kuandika ujumbe, jina au mambo kadha wa kadha, kama vile methali na ujumbe wa kidini, si la jana au juzi. Ni mfumo uliodumu kwa muda mrefu.

 

Katika miaka ya karibuni, nadhani (ingawa sina uhakika sana) kutokana na kasi fulani ya mwamko uliojitokeza vyombo vingi vya moto, ikiwamo usafiri wa Bajaji, zimepewa ujumbe wa kidini.

 

Vivyo hivyo, wapo watu wanaoamua kutoa yao ya moyoni kama vile hisia zake za mafanikio alikofikia, anayawasilisha katika maandishi hayo.