Inakuwaje Watanzania kuonea haya Kiswahili

26Jan 2021
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Inakuwaje Watanzania kuonea haya Kiswahili

KISWAHILI ni kati ya lugha zilizo maarufu duniani ikizungumzwa na watu wengi kama ilivyo kwa Kingereza, Kifaransa, Kichina na Kiarabu.

Ni lugha inayoeendelea kukua, kuzungumzwa na kutambulika duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), linasema Kiswahili, kinazungumzwa na watu milioni 180 duniani kote.

Mwaka 1986, UNESCO ilipitisha azimio la Kiswahili kutumika kwenye vikao vyake, kadhalika azimio la kukitumia katika Umoja wa Afrika (AU), kama lugha ya mawasiliano lilishapitishwa miaka ya karibuni.

Kiswahili kinazungumzwa zaidi Afrika Mashariki nchini Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na pia kinatumiwa Afrika ya Kati Visiwa vya Ngazija (Comoro), Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe na Zambia.

Pamoja na urithi huu wa kujivunia kizazi cha sasa hawakifahamu na Watanzania wengi waliozaliwa na kukulia nchini, hukikwepa.

Leo kuna mchanganyiko wa lugha mtu akizungumza anachanganya Kiingereza na Kiswahili ‘Kiswakinge au Kiswanglish’, kwa tafsiri mbili au zaidi aonekana msomi au ametembelea zaidi nchi zinazozungumza Kiingereza.

Ipo dhana kuwa, mzungumzaji wa lugha ngeni ni kati ya waliokwenda shule hadi chuo kikuu au ana uelewa zaidi na kwamba licha ya Kiswahili kuhitaji kukuzwa, kuenziwa, baadhi hawajivunii na kuionea aibu lugha hiyo pale wanapotaka kufikisha ujumbe kwa jamii.

Baadhi ya wasomi na wanazuoni ndiyo zaidi wanao kionea haya, wanataka kuaminisha umma kwamba wamekwishaisahau lugha mama ambayo waliizungumza tangu wakiwa ngazi ya awali shuleni, nyumbani na hata sasa mitaani.

Kundi hili na Watanzania lina nafasi kubwa ya kuitangaza lugha hiyo na kutoa maelezo yaliyonyooka katika Kiswahili bila kujali hatua za kielimu walizofikia.

Hivi sasa kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ni fursa nyingine ya kukuza lugha hiyo kupitia majukwaa yote mtandaoni hasa ya kijamii.

Kuzungumza ‘Kiswanglish’ katika kadamnasi au mtandaoni kwenye kurasa za twitter au whatsapp kunaishusha hadhi lugha hiyo ilijipatia umaarufu duniani.

Kwanza kuchanganya lugha, ujumbe haufiki ipasavyo na huwachosha wasikilizaji ni vyema kuchagua kutumia lugha moja mwanzo hadi mwisho katika uwasilishaji.

Tanzania inategemewa kuwa nchi ya kwanza kukipigia debe Kiswahili, ili kizungumzwe ndani na nje ya nchi badala ya kukikoroga na kusababisha kionekane duni.

Kiswahili ambacho kiliwaunganisha Watanzania kupitia juhudi zilizofanywa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ni vyema kukienzi ikiwa ni pamoja na kuandikwa na kukidumisha kama ilivyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, kwenye maadhimisho ya lugha hiyo yaliyoanza Januari 19 hadi 20.

Ikumbukwe kuwa kuna sababu zilizosaidia kukuza na kueneza lugha kama kupitia taasisi na sekta ya elimu, uchumi kwa njia ya wafanyabiashara pamoja na watalii.

Kumekuwa na mwingiliano wa lugha ya Kiswahili kupitia wafanyabiashara ambao wanaingia nchini, kufuata bidhaa hasa kutoka mataifa yasiyo na bandari.

Pia watalii ambao wanakuja kuzuru vivutio kama mbugani, magofu yakiwamo ya Bagamoyo na Zanzibar, michoro ya mapangoni kama ya Singida na sehemu za mambo ya kale kama Bonde la Olduvai.

Tanzania ambacho ni kitovu cha Kiswahili, inaweza kukienzi kwa kutumia vyuo vikuu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chenye Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili (TATAKI).

NI eneo linalosomesha wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja nchini kujifunza lugha hiyo na kuitangaza sehemu mbalimbali duniani kwa ufasaha zaidi lakini pia inaweza kuwa jukwaa la Kiswahili, chanzo cha machapisho na utafiti wa Kiswahili duniani.