Inakuwaje wazee kuhoji mahakamani…

19Oct 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Inakuwaje wazee kuhoji mahakamani…

KWA wanaokuwa mahamakani iwe kwenye kesi zao, za jamaa zao au nyingine, wakati mwingine wanaweza kujiuliza hivi kuna uhalali wazee wa baraza wanaosikiliza kesi kumhoji shahidi maswali mahakamani?

Kwa mujibu wa kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai, kinaelekeza kuwa kesi zote za jinai mahakama kuu ziendeshwe kukiwa na usaidizi wa wazee wa baraza, kadhalika kifungu cha 7 cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu kinataka vivyo hivyo kwa upande wa mahakama za mwanzo.

Kifungu cha 177cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu wazee wa baraza kuuliza maswali mashahidi wakati wa kesi. Huku kifungu cha 290 cha Sheria ya Ushahidi kikiruhusu hayo kufanyika, aidha wakili na wahusika katika kesi kwa maana ya mshitaki na mshitakiwa kuhojiana maswali pia ni jambo linaloruhusiwa.

Kifungu cha 177 kinawaruhusu wazee wa baraza kuuliza maswali wakati tukiona hiki cha 290 kikiruhusu wakili pamoja na mshitaki na mshitakiwa kuhojiana maswali. Kisheria kuna tofauti ya kuhoji maswali(cross examine) na kuuliza maswali au kwa lugha inayotumika mahakamani ‘ask or put questions.

Na tofauti ni hiyo kuwa katika vifungu hivi wazee wa baraza wameruhusiwa kuuliza, wakati mawakili na wahusika wa kesi wakiruhusiwa kuhoji.

Katika mahakama kuhoji ni kuuliza maswali ya kumchanganya shahidi, maswali ya mitego, maswali yaliyo nje na muktadha wa kesi ili kumvuta shahidi na maswali mengine ambayo hayajanyooka. Hata maswali yaliyonyooka yanaruhusiwa pia katika kuhoji.

Anayehoji au kwa lugha ya kortini cross examine, ana uwanja mpana wa kuhoji chochote. Kwake mbingu ndio mpaka wa kuhoji na anaamini kuwa huku ndiko kuhoji.

Vilevile, kuuliza maswali kwa mujibu wa tafsiri ya kifungu cha 177 Sheria ya Ushahidi ni kuuliza maswali yaliyonyooka tu na kuepuka swali lolote lenye lengo la kumchanganya shahidi. Ni maswali yanayolenga kupata ufafanuzi tu katika kile alichosema shahidi huyo.

Hii ndiyo tafsiri iliyotolewa na majaji watatu wa mahakama ya Rufani Jaji January Msoffe,Rutakangwa na Jaji Bwana katika Rufaa namba 147/2008 kati ya Mathayo Mwalimu na Masai Rengwa dhidi ya Jamhuri.

Ni makosa wazee wa baraza kuvaa joho la uwakili au joho la mshitaki na mshitakiwa na hivyo kuanza kuhoji maswali. Hii imekua kawaida sana hasa mahakama za mwanzo ambapo wazee wa baraza wamekuwa wakihoji kufikia hatua ya kupandisha jazba kana kwamba naye ni mhusika katika kesi.

Lakini pia wamekuwa wakihoji watuhumiwa katika staili ya uwakili. Yote haya ni makosa.

Iwapo jambo kama hili limekukuta basi hii inaweza kuwa sababu ya rufani kwa kuwa unahisi hukutendewa haki kwa kuhojiwa na wazee wa baraza.

Wazee wa baraza wanatakiwa kubaki na kazi yao ambayo ni kuuliza, kushauri huku kazi ya uwakili ya kuhoji na ile ya kuamua ya uhakimu au ujaji kuwaachia wenyewe. Wakati mwingine watuhumiwa hufokewa na wazee wa baraza. Hii si sawa na yafaa ifahamike hivi ilivyoelezwa kuwa si jukumu lao kufoka.

Kitu ambacho unaweza kufanya kama wewe ni mtuhumiwa na mzee wa baraza akakuhoji, au kupaza sauti kwa ukali yafaa umueleze kuhusu wajibu wake na uiombe mahakama iyaandike na kuyaingiza kwenye kumbukumbu hayo uliyomueleza.

Na usisitize yaandikwe kweli kwakuwa iwapo utapatikana na hatia hayo yanaweza kuwa sababu yako ya rufaa.

Ni vyema pia kufahamu kuwa mahakama ya rufani katika kesi iliyotaja hapo juu imeshauri muda wa wazee wa baraza kuuliza maswali.

Sio wakati wote watauliza maswali bali katika muda maalum. Mahakama ya Rufani imependekeza wazee kuuliza maswali mwishoni kabisa baada mawakili kufunga kumhoji shahidi(re-examination) au kama hakuna mawakili baada ya mshitaki na mshitakiwa kumaliza kuulizana maswali.

Wasiulize muda wowote au kumuingilia na kumkatiza shahidi wakati akieleza au akijibu swali. Wasubiri wanaohojiana wamalize ndipo waje kuuliza. Majaji hawa wabobezi wanashauri wazee kuyazingatia haya.