Itapendeza kila Mkuu wa Wilaya, Mkoa wadhibiti wasiovaa barakoa  

22Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Itapendeza kila Mkuu wa Wilaya, Mkoa wadhibiti wasiovaa barakoa  

KATIKA jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa corona, serikali imeshaagiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa sehemu zenye mikusanyiko, ili kujikinga na wimbi la tatu lililoibuka katika mataifa mbalimbali.

Wakuu wa mikoa na wilaya nao wameshapewa maelekezo ya kuhakikisha wanatimiza agizo hilo kwa kuzishirikisha kamati za afya ya msingi, namna wanavyotekeleza, nayo inaingia katika tafsiri na thamani fulani ya utumishi, kuwa kipimo cha utendaji wao kikazi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, anaagiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kurejesha utaratibu wa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na matumizi ya vitakasa mikono.

Kwa mujibu wa waziri huyo, hatua hizo zinachukuliwa kwa kuwa Tanzania inazungukwa na nchi nyingi za Afrika Mashariki, majirani wa pembe za Afrika na safari zaidi, wageni wanapokewa kila kukicha kutoka pembe mbalimbali duniani.

Dk. Gwajima anabainisha kuwa, utaratibu wa kuvaa barakoa unapuuzwa, hali ambayo ni hatari kwa kuwa Tanzania imezungukwa na nchi ambazo tayari zinapigwa na wimbi la tatu la corona.

Kwa kuwa serikali imeshatoa miongozo, kilichobaki ni utekelezaji, wananchi wachukue tahadhari, pia suala la kutoa elimu lingechukuliwa kwa uzito kuanzia ngazi ya chini ili kudhibiti ugonjwa huo.

Elimu inapaswa kuanzia ngazi ya familia na kupanda juu hadi kwenye wilaya, mikoa na hata taifa kwa ujumla, ili kuondoa uzembe uliopo wa baadhi ya watu kutovaa barakoa kwenye mikusanyiko.

Si vibaya suala la kuvaa barakoa likihimizwa nchi nzima na kusimamiwa kikamilifu badala ya kusimamiwa na baadhi ya viongozi wa mikoa na wilaya huku maeneo mengine kukiwa kimya.

Wapo baadhi ya wakuu wa mkoa na wilaya, ambao kwenye maeneo yao wamepiga marufuku abiria kusafiri katika mabasi bila ya kuvaa barakoa, wakiwataka wananchi wao wawe salama.

Mfano hai ni kwamba, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, ameshapiga marufuku abiria katika mkoa huo kusafiri bila kuvaa barakoa, lengo ni kuhakikisha maambukizi ya corona yanadhibitiwa.  

Wakati Mtaka akipiga marufuku, Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Said Mtanda, anazitaka mamlaka za usafirishaji kuzuia mabasi kutoka stendi kama kutakuwa na abiria asiyevaa barakoa ili za kujikinga na corona.

Iwapo marufuku hiyo itapigwa nchi nzima, dhahiri kila Mtanzania atakuwa katika hatua ya kuona umuhimu wa nyenzo barakoa kujinga na kuwakinga wengine, badala ya kusikia kwenye wilaya moja na mkoa viongozi wake wakivalia njuga barakoa.

Wananchi wa wilaya hizo na mikoa hiyo wanaweza kuchukua hatua, lakini zikaharibiwa na wale ambao kwenye maeneo yao hajazuiwa kusafiri bila kuchukua tahadhari, ikiwamo kuvaa barakoa.

Itapendeza zaidi kuona, iwapo hatua kama hizo zitachukuliwa na viongozi wa wilaya na mikoa yote, ili kuwasaidia wananchi wao kujikinga dhidi ya wimbi la tatu la corona ambalo serikali imekiri athari zake tayari ziko nchini.

Watu wamekuwa wakisongamana bila kuvaa barakoa, hivyo ni vyema wakaagiza wizara husika kukachukua hatua kwa uzito, ikiwa ni pamoja na viongozi kwenye maeneo yao kuelekeza wananchi kuchukua tahadhari.

Viongozi wote wanapaswaa kuchukua hatua kama zilivyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Wilaya ya Moshi. Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake na anapaswa kuchukua hatua zinazoelekezwa na mamlaka zilizopo.

Si rahisi wizara yenye dhamana ya afya za Watanzania kufika kila sehemu, bali maagizo ambayo inatoa kwa viongozi wa wilaya na mkoa, yanatosha kupewa uzito, ili kuhakikisha ugonjwa huo haupati nafasi.

Ikumbukwe kuwa, tangu ugonjwa huo kuingia nchini, kumekuwapo na elimu mbalimbali zikiwamo zinazotolewa ‘vijiweni’ ambazo ni kinyume na maelekezo ya wizara husika kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO.

Wapo wanaowapotosha wenzao, kwamba kuvaa barakoa hakuna maana yoyote, hali ambayo kwa namna moja au nyingine inachangia kukwamisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo.

Hao wanaotoa hija hizo potofu ndio wasiochukua tahadhari za kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. Nini sasa kifuatwe? Itapendeza zaidi, iwapo kila wilaya na mkoa, ikatangaza umuhimu wa kuvaa barakoa na kuchukua tahadhari nyinginezo.