Itapendeza 'level seat' kwenye daladala ikiwa ya kudumu

22May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Itapendeza 'level seat' kwenye daladala ikiwa ya kudumu

TANGU Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji Ardhini (Latra) kuviagiza vyombo vya usafiri kubeba abiria kulingana na idadi ya viti (level seat), karibu daladala za jijini Dar es Salaam, zimetelekeza maagizo hayo.

Ubebaji huo wa abiria kwa 'level seat' umesukumwa na kuwapo tishio la maambukizo ya virusi vya corona, ambalo liliifanya Latra kusimamia utaratibu huo ambao upo lakini umekuwa hautekelezwi.

Ingawa mwanzoni kulikuwapo na changamoto za hapa na pale, hasa baadhi ya makondakta kutozingatia ubebaji huo wa abiria ambao kimsingi ni wa kisheria, lakini kwa sasa angalau wameanza kuelewa na kuutumia.

Changamoto hizo zilitokana na ukweli kwamba walizoea kujaza abiria kupita kiasi kwa lengo la kujipatia fedha nyingi, lakini sasa hilo halipo wakati huu ambao dunia inakabiliwa na tishio la ugonjwa huo.

Sasa, kwa vile karibu wote wametekeleza maelekezo ya Latra, basi kuna haja mamlaka hiyo kuendelea kusimamia maelekezo hayo hata pale corona itakapokwisha, ili 'level seat' iwe ni ya kudumu.

Ninasema hivyo, kwa sababu kwa tabia ya baadhi ya Watanzania kutoheshimu sheria, inawezekana corona ikiasha na wakarudia kujaza abiria katika magari kupita kiasi kama zamani.

Kwa kuwa sasa wahusika wanazingatia umuhimu wa kubeba abiria kwa idadi inayotakiwa, ni vyema Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na Latra, wakaendelea kusimamia utaratibu huo hata kama corona itaisha.

Siyo siri kwamba, tangu kurejeshwa 'level seat', siku hizi daladala hazikawii vituoni kusubiri abiria kama ilivyokuwa siku za nyuma na watu wanawahi safari zao.

Imewezekana kuwaweka sawa makondakta hadi wakakubali kubeba abiria kulingana na idadi ya viti, kwa nini utaratibu huo usiendelee hata kama maambukizo ya corona yataisha?

Nadhani 'level seat' isiwe mkakati wa kupambana na kuenea kwa virusi vya corona, pia ni wa kuheshimu sheria usalama barabarani, ambazo zimekuwa zikivunjwa na daladala.

Ilikuwa kawaida daladala kujaza abiria kupita kiasi, kutofunga mlango wakati gari likiwa kwenda mwendo, makondakta kutowapa abiria tiketi na matendo mengine mengi ambayo ni kinyume.

Hilo la kubeba abiria kulingana na idadi ya viti, laweza kuwa limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ingawa pia inawezekana wapo baadhi ya makondakta ambao bado kwa kificho hawajali 'level seat'.

Suala la msingi ni kwamba, ubebaji abiria wa sasa katika daladala uwe mfumo wa kudumu, kwa sababu ndivyo sheria za usalama barabarani zinavyotaka, kwamba abiria wasijae katika gari kupita kiasi.

Pamoja na hayo, kuna haja makondakta na madereva kuelimishwa ili watambue na kuzingatia sheria hizo, wasione kama wanaonewa, kwani wapo baadhi yao wanalalamikia 'level seat' kuwa inawaumiza.

Kwamba hawapati fedha nyingi kama zamani walivyokuwa wakijaza abiria kupita kiasi kana kwamba ni halali kufanya hivyo, na kumbe wanakwenda kinyume na sheria kwani haziruhusu ubebaji wa aina hiyo.

Hivyo, waelimishwe, pia Latra na polisi trafiki wasilegeze kamba kwenye hili suala la 'level seat' ili wahusika waache kufanya kazi kwa mazoea bali wafuate sheria zinazowataka kubeba abiria kwa 'level seat'.

Kusiwapo kisingizio chochote cha kusababisha kurudi nyuma na badala yake sheria ichukue nafasi yake katika kusimamia usafiri ili makondakta na madereva wasijifanyie wanavyotaka.

Ikumbukwe, pamoja na kuwapo foleni za magari jijini Dar es Salaam, nyingine zilikuwa zikisababishwa na uzembe wao, kwa kusimama hata pasipo kituo kusubiri abiria hata kama daladala imejaa.

Wao wanaamini kwamba daladala haijai bali ndoo ya maji ndiyo inayojaa, hivyo wana haki ya kuendelea kujaza abiria wanavyotaka, hali ambayo ilikuwa inasababisha watu kuchelewa katika shughuli zao.

Itapendeza, iwapo mamlaka husika hazitawarudisha tena abiria kwenye mtindo huu wa zamani ambao ni kero na tayari wameshanza kuusahau baada ya Latra kusimamia sheria.