Itikadi, mrengo kisiasa isikwamishe kuungana

20May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Itikadi, mrengo kisiasa isikwamishe kuungana

WANAWAKE ni wadau muhimu kwenye demokrasia ya vyama vingi, kwa kuwa wanashiriki siasa za uchaguzi na ndiyo wapigakura wakubwa na wahamasishaji kwenye kampeni.

Pamoja na hayo, kilio chao cha muda mrefu ni kutopata nafasi za kutosha za uongozi kwenye uchaguzi na hivyo kuonekana kama wamewekwa pembeni kana kwamba hawana uwezo.

Lakini, katika kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kutafuta uongozi, zipo harakati za kuwaunganisha zinazofanywa ili wanapojitokeza, waungwe mkono bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa.

Hii inatokana na ukweli kwamba bila kuweka itikadi za kisiasa pembeni na kuungana, hawataweza kufikia kile wanachokusudia cha kutaka usawa katika uongozi huku wenyewe wakiwa si wamoja.

Vinginevyo jamii itaendelea kukumbatia dhana potofu iliyopo kwamba wanawake hawapendani, itaendelea kutawala na hivyo kukwamisha juhudi zao za kutaka kuungana ili kupata nafasi nyingi za uongozi.

Sasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu, ni vyema wanawake bila kujali tofauti za itikadi za vyama vyao na kuwa kitu moja ili kuwaunga mkono wenzao watakaojitokeza kuwania uongozi.

Siyo siri wanawake wamekuwa wakitoa kilio kwa kuwa wanatambua mikataba mbalimbali ikiwamo ya kimataifa, ambayo imekuwa ikipitishwa ukiwamo ule wa kuondolewa kwa aina zote za ubaguzi dhidi yao.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni ule unaotokana na maazimio ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wanawake uliofanyika Beijing nchini China mwaka 1995, na kuwa chachu kwa wanawake kudai haki zao.

Hivyo ili kuhakikisha wanashika nafasi nyingi za uongozi, ni vyema wakaungana na kuwa kitu kimoja kwenye uchaguzi ujao, kwani wameshajengewa uwezo wa kujiamini na kuvunja vikwazo vinavyowazuia kuwania nafasi za uongozi.

Iwapo watakuwa wamoja kwa kuweka pembeni tofauti zao za itikadi za kisiasa, ushiriki wao wa moja kwa moja kwenye maamuzi ya kisiasa waweza kuendelea kuwa kama ulivyo sasa ingawa wanataka kupiga hatua.

Kwa maana hiyo uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni vyema wakawa na umoja ambao utawawezesha kuweka wagombea wa kutosha na kuwapigia kura na hatimaye washinde nafasi za udiwani, ubunge na nyingine.

Binafsi ninaamini kwamba wanawake wana uwezo wa kusimama wenyewe kupata nafasi za uongozi katika siasa kama walivyo wanaume, njia pekee ni kuungana na kujitenga na dhana kwamba hawapendani.

Tanzania ni moja, lakini ya vyama vingi, hivyo wakiona mmojawao awe wa chama tawala au upinzani anakubalika, basi wote hawana budi kumuunga mkono ili aibuke na ushindi.

Ushirikiano huo wa bila kujali itikadi za vyama wanaweza kuzaa matunda ya ushindi, huku wakiendelea kudumisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kutambua kwamba Tanzania ni moja yenye vyama vingi.

Hiyo ndiyo njia mojawapo ya kupanua wigo wa wanawake wengi zaidi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika siasa, kuliko kutengana kwa sababu za itikadi za kisiasa.

Siyo wakati tena wa kubaguana kwa itikadi za kisiasa kumuona mwanachama wa CCM, Chadema, CUF kama wanawake wakizingatia hayo, hawatawaona wenzao.

wapinzani, anasema mwanzoni mwa mafunzo hayo alikuwa akiwaona wanawake wenzake wa CCM kama maadui, lakini sasa anatambua umuhimu wa kushirikiana bila kujali itikadi za kisiasa.

Sasa ni wakati wa wanawake kuweka ajenda zao mbele kwa ajili ya kufanikisha malengo ambayo wamejiwekea kuliko kuweka itikadi vyama vyao mbele au kukumbatia dhana kuwa wanawake hawapendani.

Vilevile huu si wakati wa kuogopa kujitokeza kuwania uongozi, kwa sababu tayari wameshajengewa uwezo na mbinu mbalimbali za kuwawezesha kufikia pale wanapopakusudia.

Uongozi si kwa ajili ya wanaume tu bali hata wanawake, kwani si kwamba ubebwa kichwani, bali ni mbinu na uwezo wa kuongoza, ambavyo mwanamke na mwanaume wote wamejaliwa kuwa nao.

Uwezo ambao wanawake wamekuwa wakijengewa mara kwa mara, ni muhimu uwe chachu ya kuwaunganisha wanawake kuwa na umoja imara wenye lengo la kufanikisha ajenda yao.

Malalamiko ya muda mrefu ya wanawake ya kukosa haki za msingi ndani ya jamii, ikiwamo kupata nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali yanaweza kumalizika kwa juhudi zao wenyewe kwa kuungana.