Itikadi ya chama cha siasa ni zaidi ya ‘ulipo tupo’

13Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Itikadi ya chama cha siasa ni zaidi ya ‘ulipo tupo’

MBUNGE wa Mtama CCM, Nape Nnauye, amewahi kuzungumzia mtindo wa baadhi ya wanasiasa wa kuhama vyama kila kukicha na kusisitiza kitu ambacho kinaweza kuwa somo kwa wanasiasa.

Kwake uanachama ni kuamini na kuwa msimamo usiobadilika wa kiitikadi na si vinginevyo.

Ilikuwa ni wiki chache tu tangu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kujivua ubunge na kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema.

Baada ya Nyalandu kuhamia upinzani, Nape alifuatwa na vyombo vya habari ili kupata maoni yake kuhusu uamuzi wa mwanasiasa huyo, ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Katika maoni yake, Nape anasema: "Chama cha siasa ni itikadi ambayo ni imani, siamini sana katika kubadili imani kienyeji. Nitashughulikia mapungufu nikiwa ndani sio nje".

Kauli hiyo ya Nape inaonyesha ni yapi mwanasiasa anapaswa kuzingatia anapokuwa katika chama, hasa ajue ni kwanini yupo katika chama fulani, kwa misingi ya itikadi na imani.

Kwa mujibu wa Nape, mwanasiasa akiwa na itikadi ya chama hawezi kuhama ovyo kutoka kimoja kwenda kingine, hivyo inawezekana wenye mtindo wa kuhamahama hawajui hilo au hawalizingatii.

Sasa nikirejee kile ninachotaka kujadili, inawezekana baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiamini katika watu badala ya itikadi za vyama, matokeo yake wanatoka kwenda huku na kule kufuata watu.

Kwa mfano, miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa anahamia Chadema, akifuatwa na wanachama wengi, ndipo ilipoibuka kaulimbui ya 'ulipo tupo'.

Wanasiasa wenyewe walikuwa wakielezea maana ya kaulimbiu hiyo kuwa ni pale alipo Lowassa, mashabiki wake nao wanakuwepo kwa maana walimfuata alipoamua kujiondoa CCM na kwenda upinzani walimfuata.

Hata tukio la hivi karibu la kurudi tena CCM, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja naye ametangaza kujiondoa Chadema na kurudi CCM, kutimiza azma ya 'ulipo tupo'.

Amefanya uamuzi huo baada ya Lowassa kurejea CCM ikumbukwe kuwa Mgeja alikuwa ni miongoni mwa wana CCM waliohama na Lowassa kwenda upinzani mwaka 2015 ilipoibuka kauli mbiu ya ulipo tupo.

Amerudi CCM na kusema kuwa kwa muda aliokuwa Chadema yeye na wenzake walishauriana kuhusu masuala ya kujenga nchi ikiwamo kuwa na sera mbadala, kuchangia bungeni, kuachana na mkakati wa kuichafua Tanzania nchi za nje na kuepuka siasa za kejeli na matusi, lakini hawakusikilizwa.

Anasema walikishauri chama hicho kuwa cha kisiasa na si cha kiharakati, japo hawakusikilizwa na kueleza kuwa chama hicho kimegubikwa na ubinafsi na hakuna uwazi.

Mgeja anaomba radhi kwa mwenyekiti wa CCM taifa, wanachama, Watanzania na familia yake na kueleza sababu za kuamua kurudi nyumbani ikiwa ni pamoja na kazi nzuri za Rais John Magufuli.

Anataja kazi nzuri ni pamoja na kutekeleza mpango wa kuhamia Dodoma, ulioanza tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuboresha sekta muhimu za elimu, afya, usafirishaji, miradi mikubwa ya umeme na kukemea rushwa.

Siyo kwamba amefanya vibaya kurudi CCM, bali kinachoshangaza ni pale aliposubiri Lowassa kwanza ndipo yeye afuatie. Viongozi wa CCM wamekuwa wakisisitiza kwamba ‘chama kwanza, mtu baadaye'.

Chama kwanza, mtu baadaye ni kauli, ambayo haitofautiani na kile anachosema Nape kwamba chama cha siasa ni itikadi ambayo ni kama imani, hivyo wanachama wanatakiwa kuamini katika chama si watu.

Wanasiasa wanapaswa kujiuliza ni kwanini wapo katika chama fulani ili waamini itikadi za chama husika, lakini vinginevyo wataendelea kukimbia huku na kule wakiwafuata watu badala ya chama kwani lengo ni pale fulani alipo nao wawepo.