Jamani ‘traffic light’ mpya Dar safi, ila kuna shida ratiba ya dakika

20Jan 2022
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamani ‘traffic light’ mpya Dar safi, ila kuna shida ratiba ya dakika

KUKUA kwa teknolojia kumerahisisha huduma mbalimbali kwenye jamii, ikiwamo miundombinu ya barabara, ambako sasa taa za kuongoza magari maarufu ‘traffic light’ hivi sasa ni za kidigitali, jijini Dar es Salaam, kukipendeza hasa.

Matumizi ya huduma kidigitali yameleta mapinduzi makubwa kiuchumi ikiwamo kuokoa muda, kwa sababu huduma zinapatikana papo hapo na si analogia ambao ulikula muda wa watu wengi.

Hiyo inamaanisha kwamba imeirahisishia hata polisi usalama barabarani, kulazimika kukaa kwenye kila makutano ya barabara penye askari wa kuongoza magari tena kwa kupokezana, mfano halisi ni awali eneo la Ubungo.

Makutano hayo ya Ubungo kabla ya kujengwa daraja la juu liitwalo Kijazi, foleni ilikuwa kubwa na kusababisha usumbufu kwa watumiaji. Iliwachukua muda mrefu eneo hilo hata zaidi ya saa nne hadi tano kuvuka. Leo hii ni hadithi ya zama za kale.

Sasa, kuwapo kwa taa za kisasa za kidigitali zinazotumia sekunde kutokana na ‘zilivyosetiwa’ kumefanya foleni iwe historia kwa kuwa muda unaonekana wazi na kumwandaa dereva kuondoka kwa muda sahihi, ingawa changamoto imeanza kujitokeza tena eneo hili.

Majira ya jioni taa zinazoongoza magari hasa yanayotokea eneo la Mwenge kuelekea maeneo tofauti, ikiwamo Kimara, Buguruni, kutokana na hali iliyopo kwamba muda wa taa nyekundu ‘kusetiwa’ sekunde nyingi kuliko muda wa taa za kijani inayoruhusu magari kuondoka, ambayo ni sekunde 30.

Hivi sasa muda wa kuruhusu magari ni sekunde 120 au dakika mbili, ambazo kutokana na wingi wa magari hayo kutoka upande mmoja kuelekea nje ya mji kuwa mengi majira ya jioni.

Kuwekwa sekunde za kuruhusu magari kuondoka kuwa mdogo (sekunde 30) kuliko ule wa kusubiri (sekunde 120), pengine wataalamu wa masuala ya barabarani wana majibu, ingawa ukweli ni kwamba foleni katika daraja hili inaanza kurudi kimya kimya.

Kutokana na hilo, ni vyema mamlaka husika zikafuatilia suala hili na kubaini muda sahihi ambao unahitajika eneo fulani hususani katika makutano ya barabara zote jijini, kwa kuwa ukweli kwamba majira ya asubuhi mtiririko wa magari kutoka nje ya mji kuja mjini kati ni mkubwa.

Vivyo hivyo majira ya jioni magari yana kuwa na mtiririko mkubwa kutoka mjini kati kuelekea nje ya mji, hivyo kuliko na taa za kuongozea magari barabarani muda ‘usetiwe’ ambao unaoendana na majira husika.

Hilo linawezekana, kwa sababu hivi sasa taa zilizofungwa jijini sehemu nyingi ni za kidigali ambazo ‘zinasetiwa’ na hii itasaidia kupunguza usumbufu na kuondoa foleni pasipo sababu.

Suala la taa hizo kuchukua muda mrefu upande mmoja bila ya kuzingatia majira, inaathiri maeneo mengine kama vile taa za kuongoza magari yanayoingia na kutoka njiapanda ya ITV.

Majira wa jioni mtu akifika kwenye njiapanda ya ITV, mtiririko mkubwa wa magari huwa ni kutoka njiapanda hiyo na kuingia barabara ya Bagamoyo, kipaumbele kwa magari yanayotokea ITV kuliko eneo la viwanda na shughuli nyingine, ni kidogo.

Hali hiyo, pia inaleta foleni kubwa eneo la njiapanda, kutokana na taa hizo kupewa kipaumbele kikubwa kwa magari pekee yanayotoka na kueleke mjini kati.

Hili, wataalamu waliangalie na kulifanyia kazi, mtu akisimama maeneo haya machache ya yaliyotajwa kwa mfano, atabaini kitu kwamba aidha foleni inasababishwa na taa nyekundu au ya kijani katika makutano ya barabara.

Wakati teknolojia inakuja kurahisisha huduma na shughuli mbalimbali, iwe ukombozi wa kubadili fikra na mitazamo kwamba ‘kupoteza muda hata wa nusu saa si kitu’ ni mazoea au utamaduni wetu.