Jamani, hakuna uchuro aina yoyote tunapoandikia warithi wosia wetu

20May 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamani, hakuna uchuro aina yoyote tunapoandikia warithi wosia wetu

SULUHU ya kumaliza migogoro ya mirathi katika familia, ni kuandika wosia kama watu wakijenga utamaduni wa kuandika wosia pasi na shaka migogoro ya mirathi haikuwapo, wala kuchomana visu kwa kugombania mali za urithi.

Tatizo ni kwamba, watu wengi wanaogopa kuandika wosia kwa imani potofu kwamba mtu anajichulia kifo kwa lugha nyepesi wanaita ‘uchuro,’ kitu ambacho sio sawa na kufa kupo tu, kikubwa ni kuwatengenezea mazingira mazuri watoto wako kabla ya kufa, ili mali zilizopo zisiwagawe na kuwatengenezea matabaka.

Pia, wapo wanaoamini maskini hatakiwi kuandika wosia, kwa kuwa hana mali kama ilivyo kwa tajiri. Lakini, kitu pekee cha kusema hapa, ni bora ukaandika wosia hata kwa kidogo ulicho nacho, kuliko kuingiza hizo imani kwa kuwa baada ya hapo utaiachia familia migogoro isiyokwisha.

Utafiti kuhusu wosia, umebaini theluthi mbili ya watu hawana uelewa wowote kuhusiana na dhana hiyo na umuhimu wa uwekaji wosia huku baadhi yao wakiamini ni uchuro na kwamba suala hilo ni la matajiri.

Ripoti ya Haki za Binadamu 2021, iliyozinduliwa hivi karibuni mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga, iliyojikita katika maeneo matatu, ikiwamo haki za binadamu, kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni na haki jumuishi inafafanua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuhusu wosia na kugawanywa katika makundi sita, ilibaini asilimia 72 walisema hawako tayari sababu bado vijana, asilimia 63 walisema hapana wakidai ni uchuro na asilimia 76 wakidai hawawezi kuandaa sababu hawana mali za kutosha.

Aidha, asilimia 15 walisema wapo tayari kuandaa wosia kwa mdomo na si maandishi, huku asilimia 44 wakisema hawana uelewa kuhusu suala hilo.

Ni mada na dhana inayoniinua kwenye kiti na kuzuru mtaani kusaka ukweli ulikosimamia. Hapo ndipo naonana na Jacob Kilamba, kutoka Iringa anayetoa mtazamo wake kuhusu kuandika wosia. Hapo nabaini kuwa si kwamba watu wengine hawataki kuandika wosia, bali wengine pia hawana uelewa wa kutosha hata juu ya kuandika wosia, pengine hawatambui hata kidogo nini maana ya wosia.

“Watu hawataki kuandika wosia wakiamni ni kujichuria kifo. Wengine wanaamini wosia ni kwa ajili ya walio na mali nyingi,” anavyonijibu Jacob.

“Suala la kuandika wosia ni la watu wa mjini, kwa sababu wao ndio wasomi. Katika jamii yetu hapa kuandika wosia kunamaanisha kuanzisha migogoro ya kifamilia,” naye akajibu mkazi wa mkoani Iringa, baada ya kuhojiwa na Nipashe.

Hata mwanahabari ninapopiga hodi hadi kijiji cha Mgowelo hukohuko Iringa kudodosa juu ya wosia na kumpata Limo Kilamba, anayetoa mtazamo wake kuhusu kuandika wosia.

Ananijibu: "Kuna wazee ambao wanaishi kwa hofu ya watoto wao wenyewe, wakijua kwamba wana uwezekano mkubwa wa kupigwa na watoto wanagundua kuwa kuna wosia.

“Baadhi ya watu huandika wosia wakiwa wagonjwa sana na kufariki muda mfupi baadaye. Kama matokeo, wosia hupotea au katika hali mbaya zaidi ya asili itafichwa na baadhi ya wanafamilia," anasema.

Rai yangu kwa serikali kufungua darasa la kuelimisha jamii juu ya masuala ya kuandika wosia, ili kupunguza mrundikano wa kesi nyingi mahakamani, ambazo kila uchwao utasikia tunagombania mali za urithi.

Vivyo hivyo, ukidodosa tatizo unagundua aliyekufa hakuandika wosia juu ya mali zake, ili iwe rahisi katika kugawanya mali na watu wakielimika katika hilo itasaidia kupunguza vifo vya ndugu, ambavyo vimekuwa vikitokea kwa ajili ya kugombania mirathi.

  • Mwandishi anapatikana kaa simu: 0787879707