Jamani shule zetu zikaguliwe basi!

27Sep 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Jamani shule zetu zikaguliwe basi!

ZAMANI tukiwa shuleni, shule za msingi, mara kwa mara tukiwa madarasani tulishitukia wakati mwalimu akiendelea kufundisha, akiingia ‘mwalimu’ mwingine na sisi kulazimika kusimama na kumwamkia “shikamooo Mwalimu” kwa pamoja.

Naye akiitikia “marahabaa hamjambo wanafunzi?” Nasi kumjibu “hatujambooo!” Na kuturuhusu tukae na kuendelea na masomo, huku mwalimu wetu naye akimkaribisha kwa unyenyekevu naye mgeni wetu akienda kukaa dawati la nyuma kabisa.

Ikumbukwe madawati ya nyuma katika madarasa ya wanafunzi wa shule za msingi yalikaliwa kwa kiasi kikubwa na wanafunzi manunda, wale wasiosikia si kwa masikio bali kwa akili, yaani watukutu waanzisha fujo.

Sasa siku ikitokea mgeni huyo kafika na kukaa nyuma, yalikuwa mateso kwelikweli kwao, lakini pia hata mwalimu alionekana kubadilika kitabia, kama alikuwa mkali, siku hiyo aligeuka mpole kupitiliza na kufundisha bila kiboko mkononi.

Bahati mbaya, ziku zote hizo hatukutambulishwa hao ‘walimu wavamizi’ walikuwa ni kina nani mpaka walimu wetu wanoko kupoa kiasi kile, wakifundisha bila kufoka na kutuita majina ya ajabu ajabu ya ng’ombe wewe, mbuzi wewe, nguruwe wewe, na mengine mengi tu.

Kumbe baadaye tukaja kujua kuwa walikuwa ni wakaguzi ambao walifika, kuona hali ilivyo ya kiufundishaji, mahudhurio na mambo mengine yaliyohusu ufundishaji na ujifunzaji. Walikuwa watu muhimu sana kumbe kwetu.

Ndio waliohakikisha kuwa mihutasari iliyopangwa inafuatwa bila vikwazo na walimu wanafundisha kikamilifu na kwa wakati. Walihakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri na kupeleka taarifa ngazi za juu na kama kulikuwa na matatizo basi ufumbuzi wa haraka ulipatikana.

Ndio hao waliopendekeza, mwalimu au mwalimu mkuu aliyefanya vizuri basi apandishwe cheo na kuwa Mratibu Kata kama si Ofisa Elimu. Shule ziliendeshwa kwa mipango mizuri, na kumbuka nyingi zilikuwa za Serikali na ndizo zilizolengwa hasa zikishindana na za Misheni.

Kwa hiyo unyenyekevu feki ule wa walimu wetu ulizingatia kuwa majaaliwa yao yalikuwa mikononi mwa wakaguzi hao, na ndiyo sababu mara walipoondoka, walimu walijivua ngozi za kondoo na kubaki fisi na chui walewale na kutuonesha cha mtema kuni.

Nimeikumbuka hii baada ya siku za karibuni kusikia taarifa na habari za kusikitisha, kuhusu wanafunzi 10 wa shule ya msingi ya kiislamu ya Byamungu wilayani Kyerwa, mkoani Kagera kupoteza maisha kutokana na ajali ya moto bwenini.

Habari za wanafunzi wawili wa shule ya msingi Chilala, wilayani Lindi, kuchapwa na walimu wao na kisha kulazimishwa kutafuna korosho mbichi. Lakini pia kusikia habari kuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Maweni, wilayani Chato, Geita, kupoteza maisha baada ya kufunikwa na kifusi akichimba shimo.

Wale wa Kyerwa, yawezekana ni ajali lakini pia yawezekana ni kazi ya mkono wa binadamu. Sijui mpaka tuambiwe na wahusika. Wale wa Lindi haki ya Mungu ni ukatili wa walimu, utawatafunishaje watoto korosho mbichi! Utomvu wa korosho mbichi ni tindikali, unaunguza. Watu wanachorea tattoo miilini kutokana na moto wake.

Wewe mwalimu unaamua kuwatafunisha ili waungue midomo, ili wababuke fizi! Kisha ujiite wewe ni mzazi na kusahau kabisa usemi wa uchungu wa mwana aujuaye mzazi! Unamwunguzia mwenzako mwanawe, halafu unajiita mwalimu mrekebisha tabia ya wanafunzi, tabia yako ikoje?

Huyu wa Chato, pamoja na kwamba ni ajali, lakini kuna mkono wa binadamu. Hivi wewe mwalimu uliyetoa adhabu hiyo, nani alikwambia hakuna adhabu mbadala? Au kwa kuwa udongo huo mlikuwa mnafyatua matofali mnayachoma na kuyauza kwa maslahi ya matumbo yenu?

Na ni bahati mbaya, kwamba wachimbaji wanafunzi, wafyatuaji wanafunzi, wachomaji wanafunzi, wauzaji wanafunzi, lakini walaji walimu! Ukatili na unyonyaji gani huu kwa jina la adhabu? Yote haya yanafanyika kutokana na kukosekana kwa wakaguzi waliokuwa wakituvamia enzi hizo.

Wangekuwapo pengine bweni la Byamungu lingekaguliwa na kasoro kurekebishwa kabla, kifusi kisingechimbwa Maweni na wala korosho mbichi zisingetafunwa Chilala. Wizara ya Elimu ipo, sasa kwa nini haya hayaonekani na kudhibitiwa mpaka watu waathirike? Mungu anawazoom. Alamsiki!