Jamani watoto wa kambooo!

14Sep 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Jamani watoto wa kambooo!

TUKIWA wadogo, bado tunaishi mashambani, tulikuwa ndugu, tukishirikiana kwa mambo mbalimbali bila hata kujua haraka huyu ni mtoto wa nani na hasa katika familia za mitala. Familia ambazo kulikuwa na mume mmoja wake wengi, lakini tukiishi mji mmoja.

Sote tuliitana ndugu na kuheshimiana kwa kuzingatia umri na jinsi. Ndiyo kama ulivyokuwa mfumo dume, watoto wa kiume tuliheshimiwa na kunyenyekewa na wale wa kike. Amini usiamini, dada mkubwa alimpigia magoti mdogo wake wa kiume. Mfumo uliruhusu.

Enzi hizo hatukupata kusikia kuwapo kwa baba, mama au mtoto wa kambo! Na hata kama neno hilo lilitamkwa, hakuna aliyejua maana yake haraka. Pengine lilikuwa la kigeni na ndiyo sababu hatukusumbuka kulifuatilia, ingawa tulikujaambiwa kuwa baba, mama au mtoto wa kambo si wa kuzaliwa katika muunganiko wa familia husika.

Yaani kumbe alikuwa mtu wa kufikia tu katika familia, hakuwa ndugu wa damu. Na kama walikuwapo hao haikuwa rahisi kutambua kuwa huyu ni wa damu au huyu ni wa kambo, kwa sababu tulishirikiana na kupendana na kuheshimiana katika kila kitu.

Maisha yalipozidi kusonga mbele, ndipo sasa tukaja kuona pengo hilo. Uchumi ulipoanza kuwaingia watu katika jamii, tukaanza kubaguana kuwa huyu wa damu na huyu la hasha. Tukaanza kusikia aah yule si baba yake ni baba wa kambo, yule si mama yake ni mama wa kambo, huyu si mwanawe ni mtoto wake wa kambo. Nakadhalika.

Pengo hilo au ufa huo, ukaibua chuki, si tu baina ya wazazi na watoto, lakini mpaka watoto wenyewe wakaanza kubaguana na kutambiana, wewe ni wa kambo huna haki hapa. Hakika watoto wa kambo wakaanza kubaguliwa, wakaanza kunyanyaswa, wakasingiziwa kila baya lililotokea.

Kila kilichopotea nyumbani kwenye familia, mtoto wa kambo akawa mtuhumiwa namba moja, kila kilichoharibika mtoto wa kambo aliulizwa kwanza. Hivyo wale wa damu nao wakaona wawatumie wale wa kambo kama kichaka. Kila wakiharibu walikimbilia kwa wazazi kuwashitaki wenzao wa kambo.

Nao wa kambo wakajiona kunyanyapaliwa, wakajitahidi kuwa waangalifu na kujiepusha hata kukaa karibu na vyombo vinavyovunjika, kwamba isijetokea bilauri ya udongo ikadondoka na kupasuka akasingiziwa hata kama ilisukumwa na mbwa.

Wakajiona hawana nafasi tena katika familia husika, wengine wenye roho ngumu wakajiondoa akili na kuamua kuwa na tabia mbaya ya wazi tu, baada ya kuona kusingiziwa kumekithiri. Wakajiapisha liwalo na liwe, kwa sababu hata wakifanya lililo jema walionekana waovu, kwa kuwa tu ni watoto wa kambo.

Ikawa sasa kila zuri likifanyika katika familia, watoto wa damu walipewa sifa, na hata kama lilifanywa na mtoto wa kambo, aliambiwa bila mtoto wa damu kusaidia lisingefanyika. Ili mradi watoto wa kambo wakaonekana hawafai katika jamii, hawana jema katika jamii, hawana mchango chanya katika jamii.

Walipopelekwa shule, aliyenunuliwa sare kwanza ni mtoto wa damu, wale wa kambo walisubiri msimu ujao wa pamba. Vinginevyo wavae masulupwete yaliyoachwa na wale wa damu. Na wakati mwingine madaftari yenye mwandiko mzuri hata kama ni ya mtoto wa kambo, yalilazimika kusingiziwa kuwa ni ya watoto wa damu.

Mtoto wa damu aliyeonekana nunda au kilaza, hakuzomewa kama wale wa kambo, bali alitiwa moyo na kuambiwa ni utoto tu, akikua atapata tu akili, lakini wa kambo aliambiwa amerithi akili za wazazi wake huko alikozaliwa. Wa damu ndiye ajuaye kila kitu, ndiye ajuaye kusoma na kuandika, ndiye ajuaye kuchora na kuchonga.

Hivi nani alisema mtoto wa kambo ndiye asiyejua kila kitu na ndiye asiyefaa katika jamii? Nani alisema? Aaah jamani, hivi kweli tunataka kuaminishwa hivyo? Mnayaona msijifanye hamwoni kinachofanyika leo katika nchi hii!

Hamkuona mapingamizi? Hawajui kuandika majina yao, hawajui kuandika majina ya vyama vyao, kweli? Wa kambo tu ndio hawajui hayo, lakini wale wa damu? Acheni kamchezo hako bhana. Tu sawa mbele ya Maulana ambaye anatuona!