Jamii iamuke, kuzembea elimu ni kukumbatia kipindupindu

12Jun 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamii iamuke, kuzembea elimu ni kukumbatia kipindupindu

UGONJWA wa kipindupindu jijini Dar es Salaam bado umetamalaki kwa wiki kadhaa sasa na watu waliokumbwa na ugonjwa huo wameongezeka kutoka 34 mwishoni mwa Mei hadi kufikia 55 sasa, huku watu watatu wakiwa wamefariki dunia.

Hiyo ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye amekaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akiwataka watu kuacha kutiririsha majitaka mitaani.

Inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa kipindupindu ni miongoni mwa magonjwa ambayo husababishwa na aina ya bakteria aitwaye Vibrio cholerae, na kwamba ugonjwa huo ni wa kuambukizwa.

Njia kubwa ya kuambukiza inatajwa na wataalamu kuwa ni kupitia kinyesi, kwamba viini kutoka kwa wagonjwa wenye kipindupindu huenezwa kwenda kwa watu wengine kwa njia hiyo.

Dalili za ugonjwa huo ni kuharisha kinyesi kilicho na majimaji, mwili kushindwa kutumia maji na chakula na kumfanya mgonjwa kudhoofika haraka, kwa sababu ya kukosa maji mwilini.

Dalili zingine ni mgonjwa kuhisi kiu kingi na uchovu mwingi, na kushindwa kutulia, ngozi yake ya nje na ndani kunyauka, macho kuingia ndani huku akihisi kichefuchefu na kiharusi kisicho cha kawaida.

Wataalamu wanasema njia ya kuepukana na kipindupindu ni kunawa mikono kwa sabuni, viganja, upande wa nyuma wa mkono, katikati ya vidole na kucha kwa sekunde kadhaa baada ya kutoka msalani na kabla ya kula.

Si hayo tu, wanaishauri mara kwa mara jamii kuacha kutiririsha majitaka mitaani, kutumia vyoo safi na kuchemsha maji ya kunywa, lengo likiwa ni kuepukana na ugonjwa huo. Pamoja na hayo bado baadhi ya watu hawazingatii hayo.

Kuzembea elimu hiyo ni kuendelea kuhatarisha maisha, hivyo ni muhimu jamii ikabadilika na kuzingatia kile ambacho wataalamu wa afya wanaelekeza.

Muungwana anashangazwa na hatua katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ya wakazi wake kutiririsha majitaka mitaani kipindi cha mvua na hata wakati wa kiangazi.

Mtindo wa kuvizia mvua na kuelekeza uchafu wa vyooni kwenye mkondo wa maji ya mvua ni jambo linalowaweka wakazi wa jiji katika hatari kubwa ya magonjwa ya mlipuko.

Ieleweke kuwa mazoea haya yanawapoteza, hivyo ni vyema kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya.

Usafi ni adui mkubwa wa kipindupindu, hivyo jamii ikizingatia usafi ni wazi kwamba ugonjwa huo utakoma, lakini kuendelea kukumbatia uchafu ni sawa na kuukaribisha.

Kwa sasa kipindupindu kipo jijini Dar es Salaam na tayari serikali imeshatoa onyo la kuwataka wakazi wa jiji kuzingatia kanuni za afya ili kuepuka ugonjwa huo ambao chanzo chake ni uchafu.

Muungwana anabainisha kwamba kipindupindu ni ugonjwa unaoweza kutoweka iwapo kila mmoja atazingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Oktoba mwaka 2017, ulifanyika mkutano wa kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ifikapo 2030, ambao ulijumuisha maofisa kutoka nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo ulifanyika nchini Ufaransa.

Katika mkutano huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilieleza matumaini yake ya kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya ugonjwa wa kipundupindu, pamoja na idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 90 ifikapo 2030.

Hiyo ni kwa sababu ni aibu kuwa na ugonjwa huo katika karne hii.

Sasa wakati WHO ikifanya juhudi hizo, jamii nayo iwe tayari kumkabili adui huyo maradhi kwa kukubali elimu inayotolewa na wataalamu wa afya, vinginevyo adui huyo atakuwa anaondoka na kurudi kama, ambavyo imekuwa ikitokea nchini.

Ugonjwa huo ambao katika karne ya 21 umeelezwa kama ‘aibu kubwa kwa dunia,’ unaua karibu watu 100,000 kila mwaka.