Jamii ikemee daladala unyanyasaji wanafunzi

20Dec 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Jamii ikemee daladala unyanyasaji wanafunzi

MOJA ya changamoto zinazowakabili wanafunzi, hasa wale wanaoishi mjini ikiwamo jiji la Dar es Salaam ni kuachwa kwenye vituo vya usafiri na madereva wa daladala na makondakta, hali inayosababisha wachelewe masomo ama wakati wa kurudi nyumbani.

Changamoto hii ni kama imekosa ufumbuzi kutokana na ukweli kwamba, ni ya muda mrefu na imekuwa ikipigiwa kelele na watu mbalimbali, lakini bado imeendelea kuwapo kana kwamba hakuna tatizo.

Nasema hivyo kwa sababu, imekuwa ni kawaida kuona makondakta na madereva wa daladala wakiwazuia wanafunzi wanapotaka kupanda daladala ili kuwahi shuleni ama kurudi nyumbani.

Mtindo huu umekuwa pia ukiwagawa watu wazima katika makundi mawili wakiwamo wanaokerwa na vitendo hivi, huku wengine wakiona kama ni jambo la kawaida wanafunzi kuachwa vituoni kana kwamba hawatakiwi kuwahi masomo.

Katika mazingira hayo, watu wa aina hii hawaikemei hali hiyo na kuwafanya madereva na makondakta kuwa na kiburi, kwa sababu wanaona hakuna anayethubutu kuwakemea ili waache mtindo huo.

Nina uhakika kwamba wanafunzi hawapandi bure, bali wanalipa nauli kama kawaida kulingana na viwango vilivyowekwa na Sumatra, lakini bado wanazuiwa eti kwa sababu nauli wanayoitoa ni ndogo!

Kwa mujibu wa viwango vya nauli vya Sumatra, mwanafunzi anatakiwa kulipa Sh. 200 kwa ruti moja, lakini makondakta wamekuwa wakiwazuia wasipande daladala ama walipe nauli ya mtu mzima ambayo ni kati ya Sh. 400 hadi 600.

Wakati mwingine mwanafunzi akiwa na noti ya shilingi 500 kwa ajili ya kulipa nauli ya ruti moja ambayo ni shilingi 200, hukatwa nauli ya mtu mzima, huku makondakta wakidai kwamba wanapata usumbufu kutafuta chenji!

Utaratibu huo wa kuwakata nauli ya mtu mzima wanapotoa noti umewafanya wanafunzi wapate usumbufu wa kukosa nauli ya kuwafikisha wanakokwenda na hata kuchelewa vipindi shuleni ama kurudi nyumbani muda mbaya.

Kwa mazingira kama haya ya kuwatoza nauli isiyolingana na kiwango kilichowekwa na Sumatra, huwasababishia usumbufu usio wa lazima.

Hali hiyo huwaongezea bajeti isiyotarajiwa wazazi kwa sababu tu ya tamaa ya pesa ya makondakta.

Nikumbushe tu kwamba, hakuna mzazi ama mlezi anayependa mtoto wake apate taabu.

Nadhani kama wapo ni wachache wenye tabia hiyo, kinachosababisha watoto wao wasome shule za mbali ni mfumo wenyewe wa elimu.

Kwa mfano mwanafunzi anaweza kuchaguliwa kwenda sekondari ya mbali na nyumbani kwao, ama mzazi ameamua kumpeleka mbali kwa lengo la kufuata ubora wa elimu, hivyo atalazimika kupanda daladala ili kuwahi shule kwani ndiyo usafiri wa umma.

Mwanafunzi anatumia usafiri wa umma kwa sababu wazazi wake hawana gari ama njia nyingine ya kumfanya awahi shule, kwani siyo kila familia ina magari binafsi, hivyo kumzuia kupanda daladala ni kumnyanyasa na kusababisha asiwahi vipindi shuleni.

Kwa mazingira hayo unakuta wanalazimika kuamka asubuhi na mapema kuwahi usafiri wa umma ambao ni daladala ili wafike shuleni mapema, lakini wanajikuta wakichelewa vituoni kwa sababu tu ya msimamo wa makondakta na madereva.

Wakati mwingine daladala inaweza kupitiliza kituo pale dereva na kondakta wake wanapoona kuna wanafunzi, ama wanaweza wakasimama, lakini wasichukue mwanafunzi kutokana na sababu wanazozijua wenyewe ambazo zimekuwa zikipingwa wananchi.

Ukipata nafasi ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya vituo vya daladala, utakuta makundi ya wanafunzi yakisubiri usafiri na hata wakati mwingine baadhi yao hulazimika kutumia usafiri wa malori ama magari mengine ambayo siyo salama kwao.

Ikumbukwe kuwa mazingira kama hayo yanachangia kuwaathiri kielimu kwani wanatumia muda mwingi kutafuta usafiri wa kwenda shule ama kurudi nyumbani na kukosa nafasi ya kutosha kwa ajili ya kujisomea.

Katika mazingira kama haya siyo rahisi mwanafunzi anayehangaika na usafiri, akafika nyumbani akiwa na afya kiakili ya kumfanya aketi mezani na kujikumbushia mawili matatu aliyofundishwa na walimu wake shuleni.

Nasema hivyo kwa sababu wengi wao wamekuwa wakihangaika kwenye vituo vya daladala bila kuwa na uhakika wa usafiri hali ambayo inasabisha wafike shuleni wakiwa wamechelewa na hata wakati mwingine kuadhibiwa na walimu.

Kama imeshindikana kuwadhibiti madereva na makondakta wa daladala, basi ni vyema wanafunzi wakatafutiwa usafiri wao wa kuwapeleka shule na kuwarudisha nyumbani, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kuliko kuwaacha wakiteseka kana kwamba hawana haki ya kupanda daladala.