Jamii iwakabili kisheria wanaomwaga matusi

05Dec 2018
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamii iwakabili kisheria wanaomwaga matusi

MIONGONI mwa vipaumbele ambavyo vimesimamiwa vyema na Rais John Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitatu sasa ni eneo la maadili ya watumishi wa umma.

Maadili ya watumishi wa umma ni suala ambalo lilikuwa linalalamikiwa sana na wananchi kutokana na ukweli kwamba wengi wao walikuwa wamegeuka kuwa watawala.

Badala ya kuhudumia wateja, walizigeuza ofisi za umma walizokuwa wamekabidhiwa kuwa ngazi za kutengenezea ukwasi.

Ile kujali wateja (Customer Care) likawa ni neno lisilo na mashiko tena, kwani ilikuwa ni kawaida kwa mwananchi kutohudumiwa kwa wakati kutokana na mazonge mbalimbali.

Watumishi wengi walikuwa wakichelewa kufika ofisini, hawajali wateja, wanakaa saa chache ofisini na lugha ya njoo kesho ilikuwa jadi.

Kimsingi hili la maadili ya watumishi wa umma si tatizo tena kwa sasa baada ya wengi kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Wakati Rais Magufuli amepambana na hiyo saratani ya maadili ya watumishi wa umma, Muungwana anaona kuna tatizo jingine la kimaadili ambalo linapaswa kupigwa vita na jamii nzima kwa kuwa linazidi kuota mizizi.

Ninarejea tabia isiyokubalika ya watu hasa wanaume kumwaga matusi hovyo hadharani bila kujali jamii iliyo katika mazingira husika.

Tena matusi yenyewe kwa kiwango kikubwa yakilenga kinamama ambao ndio mama zetu, wake zetu na dada zetu.

Lugha hizi za matusi na zingine za aina hii ni miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha kukengeuka kwa maadili ya jamii.

Maadili yanayowaweka watu kwenye nafasi ya kuchanganua jema na baya kama sifa ya msingi ya binadamu inayomtofautisha na wanyama.

Ndiyo maana katika hali ya kawaida inatarajiwa basi binadamu awe na tabia njema, ikiwamo ya kuwa na lugha yenye staha katika mazingira ya aina yoyote na kwa watu wa rika zote.

Kibaya zaidi tabia hii ya kumwaga matusi inaonekana kushamiri zaidi maeneo ya miji na majiji, kama ilivyo kwa Dar es Salaam.
Unakuta mtu anatoa matusi mazito mazito bila ya kujali mazingira na hata kuogopa kuwa anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wiki iliyopita, Muungwana alikuwa katika daladala moja ifanyayo safari zake kati ya Tegeta Kibaoni na Makumbusho, jijini Dar es Salaam ambapo alishuhudia vijana wakipondana katika majadiliano yao kwa kumwagiana matusi ya nguoni ndani ya basi hilo.

Na kwa sehemu kubwa matusi yao yalijielekeza kwa kina mama kiasi cha kulazimu abiria wengine akiwamo Muungwana kuingilia kati kuwazuia wasiendelee kutukana.

Bahati nzuri kinamama walionekana kukerwa zaidi na matusi hayo yaliyokuwa ya kuwadhalilisha ambapo walifikia hatua hata ya kuwauliza vijana hao kwa nini matusi yao wanayaelekeza kwa kina mama tu!

Waliwauliza iwapo kuna mmoja wao ambaye hakuwa na mama yake, ama mke au dada yake miongoni mwao.

Baadhi ya abiria wakamtaka dereva wa daladala hilo alipeleke Polisi Kawe au Lugalo Jeshini, hali ambayo iliwafanya vijana hao watatu kuomba msamaha.

Ikumbukwe kwamba kutoa matusi hadharani ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria za Nchi kama inavyosema Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Nchi ambayo imeweka aina ya makosa yanahusu utoaji wa matusi ambapo mbali na faini, mtu anaweza kufungwa hadi miaka mitano jela akitiwa hatiani.

Ni rai basi ya Muungwana kwa jamii kupambana na tatizo hili la kimaadili linalonekana kuota mizizi ili kulimaliza.

Na hili linawezekana kama wananchi wote watadhamiria kuchukua hatua stahiki za kuwapeleka kwenye vyombo vya dola watu wote wenye tabia hii.

Kama Rais Magufuli ameweza kurudisha maadili kwa watumishi wa umma, vivyo hivyo wananchi tunaweza kumaliza tatizo hili la lugha za matusi iwapo tutaungana na kuchukua hatua.