Jammeh ni heri ulevi wa kilauri kuliko madaraka

10Dec 2016
Nkwazi Mhango
Nipashe
Jammeh ni heri ulevi wa kilauri kuliko madaraka

WIKI iliyopita ilitoa somo moja kubwa dunia kuwa kweli, cheo ni dhamana. Nikiwa natoka kupiga kanywaji si nikamkuta bi mkubwa wangu ameganda kwenye runinga yetu ya inchi 60! Naona yule anatikisa kichwa akidhani najipa ujiko.

Wee sitanii.Kwa taarifa yenu, nina kitu kikali.

Hiyo nyumba ya picha ni babkubwa.

Ili majambazi wakiinasa, watakuja kunivunjia hekalu na kuiiba wakauze chapchap hasa usawa huu ambao njuluku za dili zimekaushwa.

Turejee kwenye somo Mamsapu wangu si kawaida yake kuing'ang'ania televisheni saa za mchana kwani anakuwa jikoni akiniandalia kalaji, lakini nilimkuta siku hiyo amenasa.

Kuuliza kuna mchezo gani mpya umetokea hadi ukambabaisha alijibu. “Kweli cheo ni dhamana na kila chenye mwanzo shurti kifike mwisho na kigote.”

Kiasi fulani aliniudhi ikabidi nisonye na kutaka kurejea kwenye kanywaji. Nikiwa najiandaa si ndiyo akanitonya kuwa yule rais kigeugeu na king’ang’anizi wa Gambia mwenye kujipachika vyeo kuliko hata Idi Amin, Yahya Jammeh, alikuwa ametumbuliwa kwenye uchaguzi!

Mwenzenu, hamu na kiherehere vya kurejea kwenye kanywaji viliniisha; ikabidi mimi na bi mkubwa tung'ang'anie kioo kuzisikiliza habari kabla ya kwenda kupata kalaji.

Japo kudondoka kwa Jammeh si stori tena, kuna masomo kibao. Kwanza hebu fikiria jamaa aliyewahi kusema kuwa alikuwa akiwasiliana moja kwa moja na kuongoza kwa amri ya Allah asingeondoka kwa uchaguzi.

Somo jingine ni kwamba cheo ni dhamana. Ukifika wakati wa wenye dhamana kuirejesha, hata uwe mjanja na nguvu, au unapendwa au kujipendekeza kiasi gani, utaondoka tu. Cheo ni kama koti mabegani. Si la kulewa wala kukufanya ujifanye u bora kuliko wengine.

ikiria jamaa kama hili lililokuwa limepindua na kukaa kwenye ulaji kwa miaka zaidi ya 22 kudondoka kirahisi hivi.

Itakuwaje kwa wale wa kuteuliwa tena kwenye vijinafasi uchwara wanavyotumia kutukogea na kutudhalilishia walevi wakati wanapwaya?

Niligundua kuwa heri kulewa kanywaji kuliko madaraka.

Maana, Jammeh alikuwa na uwezo wa kuwapiga makofi raia waliokuwa wakimbana wakati wakitaka kumsalimia ukiachia mbali kuwafunga hata kuwaua wapinzani.

Jammeh hakujua kuwa kuna mwisho. Hata hivyo, ana bahati ya mtende. Kwani, hakuondolewa 'kigadafigadafi' ingawa ni mapema kusema nini utakuwa mwisho wake, hasa ikizingatiwa kuwa alichafua ofisi ya rais vilivyo.

Nadhani hii, imani ni kutokana na ulevi wa madaraka, au ujinga tu utokanao na kiwango kidogo cha uelewa alichokuwa nacho Jammeh na wapambe na washauri zake.

Nimejifunza kuwa sisi wavutaji wa bangi tuna nafuu. Kwani, huwa tunajivutia bangi na kubanguliwa nayo, lakini si ukubwa. Heri kuvuta bangi kuliko kuvuta ukubwa tena ukubwa wenyewe uchwara.

Baada ya kudurusu namna Jammeh alivyojisahau kwa ulevi wa madaraka na kubanguliwa na ukubwa, hebu turejee kwenye kaya ya walevi.

Kwanza, tunao akina Jammeh wangapi hata kama si marais? Hapa naongelea vijijamemeh vidogo vidogo vinavyonyevuanyevua ndiyo viishi.

Vipo vilivyolalamikiwa hata kuwatukana watendaji wenzao kama alivyolalamika dingi wa haki za walevi hivi karibuni akilaani ulevi huu wa madaraka.

Nani angeamini kuwa mlevi anayetumwa angemtukana mwenzie anayetumwa kama yeye? Juzi si nilisikia chizi mmoja wa madaraka akimtukana mwenzie eti ni chizi wakati ukiangalia wawili hawa chizi yuko dhahiri.

Wakati mwingine kiherehere, kujikomba na tongotongo ni matatizo. Majuto ni mjukuu.

Tumewaona wangapi tena wanaojaa kwenye kiganja wakaondoka kama wezi? Wapo waliosema tulikuwa wavivu wa kufikiri wakaishia kuwa mabingwa wa kutofikiri. Japo siasa ni usanii, mwingine unatia kinyaa.

Huwezi kufanya madaraka kuwa maonyesho ukafanikiwa. Na ukifanikiwa ni kwa muda tu. Madaraka, hata kama ni ya kutawala walevi, ni kufuata sheria na kanuni badala ya kujikombakomba na kufanya usanii. Kwanini hawakujifunza toka kwa mzee Nchonga jamani?

Tumalizie kwa kuwakumbusha kuwa tulichojifunza kwa Jammeh ni kwamba ulevi wa madaraka ni mbaya kuliko wa kanywaji.

Na ubanguaji wa madaraka, kadhalika una madhara kuliko wa bangi yenyewe. Nadhani akina Jammeh wetu wasioona mbele wala nyuma wamenipata. Tieni akilini.
Hakuna marefu yasiyo na ncha jamanini.