Jiko ni silaha kubwa ya mwanamke dhidi ya maadui!

17Apr 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Jiko ni silaha kubwa ya mwanamke dhidi ya maadui!

MPENZI msomaji, leo hebu niwape siri mbili zinazoonyesha umuhimu wa wa jiko kwa mwanamke. Kama kuna kitu ambacho wanawake wengi wamekuwa wakipuuzia ni jiko, hasa katika suala zima la kumwandalia mumewe chakula kizuri.

Kumbe wanajisahaulisha kwamba jiko linapoyumba, mume ndani naye anayumba. Wajua ni kwanini? Chakula kitamu ni sumaku kwa kinababa wengi. Njia ya kuupata moyo wa mwanaume ni kupitia chakula.

Hata wengine wametumia chakula kuwapata maadui zao kama tutakavyoona kwenye makala haya.

Kwenye maandiko ya Mungu, mfano Biblia Takatifu, zipo siri mbili ambazo tunapaswa kuzitafakari kwa undani ambazo zinadhihirisha umuhimu wa jiko kwa mwanamke.

Siri ya kwanza ni ifuatayo;- Kulikuwa na vita kali kati ya Israeli na taifa jingine. Kiongozi wa kambi ya adui, aitwaye Sisera alikamatwa na mke wa Heberi, Mkeni.

Mungu alitamka Baraka juu yake kwa sababu alifanikiwa kumuangamiza kiongozi wa maadui zake kupitia jiko (chakula).

Tusome kitabu cha Waamuzi 5:24-27, imeandikwa;- “Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Hebeli, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.

Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima. Akanyoosha mkono wake akashika kigingi, nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya ufundi;

Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo ya fundi, akamtoboa kichwa chake. Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala, Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.”

Msomaji wangu, ona nguvu ya jiko la mwanamke inavyoweza pia kuleta maangamizi. Jiko lina nguvu sana. Kumbuka Sisera alikuwa amepigana vita kali sana na pia alikuwa amechoshwa na nguvu ya Mungu iliyokuwa inapigana naye pasipo kuchoka. Waamuzi 5:20 Imeandikwa; “Walipigana kutoka mbinguni, nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera”.

Mungu alihitaji mtu mmoja tu wa kummaliza. Sisera aliomba tu maji ya kunywa. Pengine ni kutokana na kiu kali aliyokuwa nayo. Swali hapa ni je, kwanini hakutambua kwamba alikuwa anaulizia maji kutoka kwa adui yake? Ni Mungu pekee ndiye anayeweza kujibu.

Yapo mambo tumefichwa. Ni kama ambavyo huwezi kujua utakufa lini na nini kitakachokuua. Mungu anasema katika andiko lake moja kitabu cha Mhubiri 8:7 kwamba, “kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa?”.

Sisera hakujua kama litampata baya. Alipoomba maji, Yaeli hakubishana naye, hakumfokea Sisera, nguvu yake ilikuwa katika jiko. Akamletea maziwa na siagi katika sahani la heshima, na mara tu alipomuona yule mwanamke analeta maziwa akalainika kama mtoto.

Kabla Sisera hajafahamu nini kinaendelea, tayari alikwisha uawa. Siri ya ushindi wake unaelezewa tu kwa kile alichokileta kutoka jikoni.

Ewe mwanamama, jifunze kutamka maneno ya kinabii kwa imani kwenye chakula unachompikia mumeo. Tamka vile unavyotaka mumeo awe. Hii ni siri kubwa! Kama mwanamke, ni kitu gani kizuri unachoweza kukitoa jikoni kwako?

Siri ya pili: Ukisoma katika Biblia, utaona jinsi malkia Esta alivyoweza kumwangamiza adui wa Wayahudi aitwaye Hamani, ambaye alikuwa amekusudia kuwaangamiza Wayahudi wote. Yeye (Esta) alitumia pia JIKO, yaani chakula, kama silaha dhidi ya adui aliyekuwa anahatarisha maisha ya watu wa taifa lake. (Soma Esta 5:4-8).

Siku iliyofuata Mfalme na Hamani walijongea karamuni. Muda wote huo, malkia Esta alikuwa akiomba katika roho kuwa mfalme atokeapo kula na kushiba, moyo wake utakapofurahi, lazima angekubali kumwadhibu adui yake. Na ndivyo ilivyotokea. Hamani aliangamizwa kwa kutundikwa kwenye mti.

Mpenzi msomaji, hapa tunapata fundisho kwamba jiko ni silaha kubwa ya mwanamke dhidi ya maadui. Mwanamke atakapolitumia jiko kwa ujuzi na hekima, anaweza akawashinda maadui wanaofuatilia maisha/ndoa yake. Wapo wanaume waliotekwa na makahaba na kuziasi ndoa zao. Kisa wake zao wameshindwa kuwapikia chakula kitamu, na badala yake uhondo huo wanaupata nje ya ndoa.

Wapo wanawake wamezembea, wakawaachia wadada wa nyumbani( hausigeli) wawapikie waume zao kila uchao. Upishi ule ule huchosha ndio maana kinababa wengine hupiga kisogo na kutafuta ladha tofauti ya chakula. Michepuko inaanzia hapo. Anaponaswa mahala anapopikiwa chakula kizuri, kwako arudipo ameshiba, utamlaumu nani?

Jiko lina nguvu. Linaweza kukupeperushia ndege wako uliyemtunza kwa gharama kubwa, akanaswa kwenye tundu lingine linalomliwaza, ukaishia kulalamika, kumbe chanzo ni wewe mwenyewe. Mithali 14:1,“Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’. Maisha Ndivyo Yalivyo.

Niishie hapa kwa leo. Je, unalo la kuongezea? Ukiwa na maoni kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]