Jionee tofauti kati ya Buswita na Niyonzima

04Sep 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Jionee tofauti kati ya Buswita na Niyonzima

PIUS Buswita, kiungo wa zamani Mbao FC hivi sasa amekuwa maarufu sana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na si kwa sababu ya kuanza vizuri au kung'ara kwenye mechi za Ligi Kuu au timu ya Taifa, Taifa Stars la hasha.

Kilichomfanya mchezaji huyo awe maarufu kuliko Emmanuel Okwi aliyefunga mabao manne kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu si soka lake uwanjani, bali ni kufungiwa mwaka mmoja na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), baada ya kubainika amesaini klabu mbili za Simba na Yanga.

Mchezaji huyo pamoja na meneja wake wamekiri hilo la kusaini klabu mbili. Meneja wake anadai kuwa mchezaji wake alipitiwa na 'shetani.'

Yeye mwenyewe anadai kuwa Simba walimsainisha kwa nguvu, baada ya kwenda kumtishia mama yake mzazi nyumbani.

"Walikwenda kumtishia mama yangu nyumbani, unajua yule ni mwanamke, akaogopa, akaniambia nenda kawaridhishe, ndiyo nikafanya hivyo," alisema.

Ina maana Buswita anatuambia kuwa hakusaini Simba kwa matakwa yake, ila alilazimishwa au kulikuwa na shinikizo.

Hapa kidogo mimi nina wasiwasi naye. Ukisikiliza sakata hili tangu mwanzo utagundua kuwa kiungo huyo alianza kusaini mkataba Simba, baadaye ndiyo akaenda kusaini Yanga.

Angetuambia labda Yanga ilimlazimisha kusaini, hapo kidogo tungemuelewa. Buswita alisaini Simba wakati bado hajasaini Yanga, hapo sidhani kama kulikuwa na shinikizo lolote wala pingamizi. Lakini kwenda kusaini Yanga huku akijua ameshaingia mkataba na klabu nyingine hapa ndipo angalau angetuambia alishinikizwa.

Au labda angeanza kusaini Yanga, tungeweza kumuamini kwa kutuaminisha kuwa Simba ilimlazimisha na kumtisha hali iliyosababisha kufanya kosa la kusaini mikataba miwili.

Buswita anataka kutuambia kuwa alisaini Yanga kwa hiari yake, hakulazimishwa na mtu yoyote, lakini wakati huo huo akiwa ameshaingia mkataba na klabu nyingine.

Hilo ni kosa na TFF ya safari hii imekuja kivingine. Labda mchezaji huyo aliambiwa saini tu hayo mengine tutayarekebisha huko huko TFF.

Kwa kuwa ilikuwa ni kawaida TFF iliyopita kufungia wachezaji waliosaini mara mbili kwenye klabu ndogo, lakini klabu kubwa linakuja suala la kulinda kipaji cha mchezaji.

Huko nyuma tuliona mchezaji William Lucian 'Gallas', akifungiwa mwaka mmoja kwa kujisainisha klabu za Ndanda na Mwadui, Mohamed Mkopi naye akisajili klabu za Mbeya City na Tanzania Prisons.

Lakini kuna wachezaji kama Mrisho Ngassa, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani wakiachiwa kuchagua klabu za kuchezea, ili kulinda vipaji vyao, klabu moja ikirudishiwa pesa zao.

Uamuzi huo ulikuwa ukishangaza wengi. Lakini TFF mpya inaonekana kutaka kurudisha nidhamu ya soka kwa wachezaji na klabu zote bila kujali kubwa na ndogo.

Nadhani Buswita inabidi ajililie mwenyewe kama si kupambana na hali yake, kwani angeweza kuepuka hilo. Inabidi sasa ajifunze alichofanya Haruna Niyonzima.

Alishinda na kula na viongozi wa Yanga. Alikuwa mchezaji wa Yanga, lakini alikwenda kusaini Simba baada ya kufikia pesa aliyoitaka yeye.

Sidhani kama hakubembelezwa au kushawishiwa na viongozi wa Yanga. Lakini alikuwa na msimamo kuwa klabu yoyote ikifika kiwango anachokitaka anasaini.

Na ndicho alichofanya. Niyonzima angeweza hata kusaini klabu zote mbili, akakusanya pesa luluki zilizofikiwa na klabu hizo akaenda zake kupumzika Rwanda mwaka mzima, au kusubiri huruma ya TFF iliyopita ya kulinda vipaji vya wachezaji wa klabu kubwa.

Kwa mazingira yaliyokuwapo, ilikuwa rahisi zaidi Niyonzima kusaini mara mbili kwenye klabu hizo kuliko Buswita.

Lakini kwa sababu anajitambua hakuingia mkataba na klabu yake ya Yanga licha ya kuwa alikuwa na marafiki wengi waliokuwa wanamtaka abaki. Akasaini klabu moja tu. Anajua kuwa kusaini klabu mbili ni kosa.

Kusaini mkataba klabu mbili ni kosa kisheria. Buswita alitakiwa achague klabu moja tu kati ya Simba au Yanga. Kwa sasa hana wa kulilia zaidi ya huruma ya Simba kama watarudishiwa pesa na gharama zao.