Jitihada nzuri kuwavuta darasani waliofaulu darasa saba Mkuranga

11Jan 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jitihada nzuri kuwavuta darasani waliofaulu darasa saba Mkuranga

NINAGUSWA kusema kwamba, na rai ya kutaka jitihada zifanyike kuwasaida wanafunzi waliokosa nafasi za kujiunga na masomo kidato cha kwanza mwaka huu, hadi ifikapo mwezi Machi, wanapaswa kuwezeshwa wajiunge na masomo.

Hiki ni kipindi ambacho shule za msingi na sekondari nyingi zimefunguliwa katika mikoa yote nchini, tayari imetimu wiki moja masomo yameanza.

Katika kundi hilo la wanafunzi, mbali na walioanza masomo tangu Januari 9 mwaka huu, wengine wanatarajia kuanza Jumatatu ijayo.

Pia, wapo walioingia madarasa mapya na wengine wameandikishwa kujiunga na elimu ya awali.

Hizo zote zinajumuishwa kuwa furaha kwa wazazi kuona watoto wameanza elimu ya msingi na wengine wana furaha kwamba watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari.

Ni kitu ambacho hakipingiki, kwamba wazazi wanafurahi kuona watoto wao wamepata fursa shuleni, kwa ajili ya kusonga mbele na masomo.

Kuna ambao, upande wa pili wa hisia zao unajitokeza, kwamba furaha yao inatoweka japo watoto wamefaulu. Hoja iliyopo ni kwamba, watoto hao wamekosa dhule kutokana na vyumba vya madarasa kuwa vichache, katika shule zilizopo.

Nasema, kukosekana nafasi za kujiunga na masomo ya sekondari kwa kila mwaka ambao ufaulu unaongezeka, kunasababisha baadhi ya wanafunzi kukosa nafasi za kuingia kidato cha kwanza.

Hicho ni kitendo kinachowaumiza vichwa wazazi, ambao wanakuwa katika mategemeo kwamba, kuna shule ambazo hazikufanya maandalizi ya kutosha katika kuwapeleka watoto masomoni, kama kuhudumia haki yao ya kisheria ya kufaulu masomo.

Niseme, pamoja na wanafunzi hao kukosa nafasi katika shule zao, serikali daima huwa haiwaachi. Wanafunzi hao wanakuwa katika ahadi ya kuendelea na masomo, baada kukamilika vyumba vya madarasa.

Nizungumzie hapa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambako kuna wanafunzi zaidi ya 1,000 wameshindwa kuendelea na masomo mwaka huu, japo wamefaulu mitihani ya kuingia kidato cha kwanza.

Sababu inayotajwa hapo, ni uhaba wa vyumba vya madarasa ndio hali hiyo imechangia wanafunzi kukosa nafasi hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Injinia Mshamu Munde, anasema kuwa jumla ya wanafunzi 1,017 wameshakosa nafasi za kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu, japo wamefaulu katika mitihani yao.

Anakiri ufaulu wa vijana hao umekuwa ukiongezeka kila mwaka na wameshajenga shule tatu za sekondari, lakini hazikupata usajili, kwa sababu ya kukosa maktaba.

Injini Munde anaahidi kuwa, maktaba hizo wataziweka katika shule hizo na hadi kufikia Machi mwaka huu, wanafunzi waliokosa shule wataanza masomo yao kama kawaida.

Nasema, ni hatua ya kujituma inayopaswa kuigwa na viongozi wengine, hasa wa halmashauri zilizopo, kuwawezesha wanafunzi waliokosa nafasi wapate fursa na waendelee na masomo yao.

Tahadhari ya wazi iliyoko ni kwamba, kama wanafunzi hao wataendelea kukaa nyumbani, wanaweza kujiingiza katika mambo yasiyofaa kitabia.

Kwa sasa, niseme jitihada zinatakiwa kufanyika ili mwaka huu katika miezi ya mwanzo, wanafunzi waliokosa nafasi wapate nafasi waendelee na masomo kuijenga Mkuranga bora.