Juhudi zaidi zahitajika kuepusha ajali za barabarani

09Jun 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Juhudi zaidi zahitajika kuepusha ajali za barabarani

Maisha ya zama hizi ni kwamba, matumizi ya vyombo vya usafiri ikiwemo barabarani ni ya lazima kabisa. Hayaepukiki kwa sababu ya umuhimu wake wa kurahisisha usafiri na usafirishaji kutoka eneo moja kwenda jingine.

Mazingira hayo ndiyo yanayosababisha watu wengi wajikute hawana namna nyingine zaidi ya kuutegemea usafiri huo.

Kukithiri kwa ajali za barabarani nchini hata kusababisha watu wengi kupoteza maisha, kunaleta hofu kubwa hususan kwa watumiaji wa usafiri wa barabara kwamba hawana uhakika wa usalama wa maisha yao wakiwa barabarani.

Katika hali hiyo, usalama wa abiria tangu wanapoanza safari hadi mwisho, hutegemea zaidi uimara wa gari, miundo mbinu ya barabara, umakini wa dereva katika kuzingatia sheria za usalama barabarani na vinginevyo.

Hata hivyo, usafiri huo umeleta hofu kwa kipindi cha miezi minne mfululizo sasa hapa nchini, kwa sababu ajali zimekuwa zikigonga vichwa vya habari vya vyombo vya habari tofauti katika namna ambayo inatia hofu na simanzi kubwa.

Pamoja na juhudi zinazofanywa na Kikosi cha usalama barabarani katika kuhakikisha kuwa, kanuni na sheria za usalama barabarani zinazingatiwa ili kuleta utatuzi wa hilo, lakini hali bado ni mbaya.

Kwa namna yoyote ile, juhudi zaidi zinahitajika ili kubaini kiini au chanzo cha ajali hizo, ambazo zinaacha simanzi kwa familia nyingi kufiwa na wapendwa wao, kusababisha majeruhi , ulemavu wa kudumu na upotevu wa mali.

Kuna kila sababu ya kuchukua hatua za haraka ili kupunguza na kudhibiti kabisa ajali hizi kwa lengo la kuokoa maisha ya watu na mali zao.

Pengine ongezeko la watu na shughuli zao, kunalazimisha kuwe na ushindani katika soko la usafiri na biashara kwaujumla hata kuvutia ongezeko la kampuni lukuki za usafiri, na mabasi ya kila aina yanayotoa huduma za usafirishaji abiria na mizigo.

Napendekeza kuwa, ni muhimu sana kufuatilia kwa karibu mabasi yote yanayoingizwa na kuundwa nchini kama yana ubora unaotakiwa katika barabara zetu ? Madereva wapimwe akili, macho, kilevi ikiwemo kufuatiliwa kwa karibu historia zao katika ngazi za familia ili kubaini kama wana akili timamu.

Kama hiyo haitoshi, utaratibu wa utoaji wa leseni unafaa kutazamwa kwa makini kwambakila anayepewa leseni anastahili hasa au tu kwa sababu anamudu kulipia? Je suala la rushwa katika utoaji wa leseni limekwisha au halipo? Kama lipo tufanye nini kuhakikisha kuwa haliathiri maisha ya watumiaji wa barabara?

Muundo mzima wa gari unakaguliwa mara ngapi baada ya kuwa barabarani na kufanyiwa marekebisho haya na yale
Vipuri, matairi ya magari ambavyo vingi huingizwa nchini kutoka nchi za nje, vifanyiwe ukaguzi zaidi, na Shirika la Viwango nchini (TBS), ambalo lina dhamana hiyo.

Vifaa hivyo vimekuwa vikitiliwa shaka na baadhi ya watu ambao, wamekuwa wakiuliza maswali lukuki kuhusu kuongezeka kwa ajali.

Pamoja na kuhitajika umakini wa dereva awapo barabarani, ikiwamo weledi na uzoefu kutamsaidia dereva, iwapo kutatokea kitu ghafla barabarani, na kuchukua maamuzi sahihi.

Safari za kuelekea mikoa mbalimbali, kama Tabora, Shinyanga, Mwanza, Songea ama Mbeya kuna changamoto nyingi barabarani ambazo zinakuwapo, ikiwamo milima na kona kali.

Uzoefu wa madereva unahitajika katika barabara hizo ili kuepusha ajali kutokea.

Takwimu zilizotolewa katika kipindi cha hivi karibuni na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga , anasema katika ajali za barabarani 2,224 zilitokea Januari hadi mwanzoni mwa Aprili.

Watu 866 walikufa na wengine 2,363 walijeruhiwa kati ya Januari na Machi, wakati wengine 103 walipoteza maisha.
Katika ajali hizo chanzo kikubwa kinaelezwa kuwa ni mwendokasi wa madereva kutozingatia alama na michoro ya barabarani.

Ajali zinaweza kuepukika iwapo, zitazingatiwa sheria za usalama barabarani, lakini Watanzania tunaendelea kumuomba Mungu atuepushie na ajali hizi.