Kagame ingependeza kwa sasa na si Chalenji

04Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kagame ingependeza kwa sasa na si Chalenji

KUNA wakati huwa najiuliza kwa nini Ukanda wa Afrika Mashariki uko nyuma sana kisoka, kuliko kwingine?

Ukanda huu ambao unaongozwa na Baraza la Vyama vya Soka  Afrika Mashariki (Cecafa), kisoka huwezi kufananisha na ule wa  Kusini, Kaskazini na Magharibi ambako soka limepiga hatua  kubwa.

Inawezekana kuna sababu mbalimbali zikiwamo za mifumo ya  uendeshaji, lakini pia inaonekana kama vile uongozi unachangia  kudidimiza soka kwenye ukanda huu ambao zamani ulitamba na  kutisha.

Ikumbukwe kuwa ukanda huu zamani ulikuwa unazishirikisha nchi kama Zambia, Zimbabwe, Malawi, ambazo zilileta chachu kubwa na kusababisha kiwango cha soka kuwa juu.

Lakini tangu nchi hizo zijitoe kwa sababu mbalimbali zikiwamo za  kiuongozi na kijiografia na kujikita Ukanda wa Kusini mwa Afrika(Cosafa), soka  la Afrika Mashariki na Kati lilianza kuyumba na kufikia lilipofika.

Naona nchi kama vile Sudan nayo wanaonekana kutaka kuipa kisogo kwani ushiriki wao kwa sasa umekuwa ni wa kusuasua.  Iwapo viongozi wa Cecafa wasipokaa na kufanya tathmini, basi huko  mbele ya safari tusishangae kuona hata nchi ya Ethiopia nayo  ikianza kujiondoa taratibu.

Ni kama vile viongozi wa Cecafa wamelala usingizi wa pono na  kuendesha michuano hiyo kwa kubahatisha, bila malengo au kwa  mazoea tu.

Hivi sasa michuano ya Kombe la Chalenji inaendelea nchini Kenya.

Hii ni michuano ambayo inazishirikisha timu za taifa wanachama wa   baraza hilo.

Lakini ukiangalia kwa makini utagundua kuwa kwa sasa michuano  hiyo haina faida yoyote na badala yake inaonekana ni kama  bonanza tu.

Ni michuano inayofanyika wakati timu zote za taifa wanachama zikiwa zimeondolewa kwenye michuano ya kimataifa iliyokuwa ikishiriki, isipokuwa Uganda tu ambayo itashiriki CHAN 2018  nchini Morocco.

Labda watuambie michuano hiyo ni maalum kwa ajili ya kuipa mazoezi Uganda, ukiondoa hapo hayakuwa na umuhimu wowote kwa sasa.

Wakati viongozi wa Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), wakikaa  na kuamua kubadilisha miezi ya kufanyika michuano ya AFCON  isiwe kipindi ambacho Ligi Kuu ya Ulaya zinachezwa badala yake kusogeza hadi Mei na Juni kipindi ambacho ligi zimeisha baada ya  malalamiko ya makocha wengi Ulaya, lakini pia kuyapa mvuto kwa  kuwapata hata wachezaji wanaoyakacha kwa kuhofia namba kwenye timu zao Ulaya, Cecafa wao wamekariri michuano ya  Chalenji kuchezwa Desemba tu.

Mimi nilidhani kuwa hiki kingekuwa kipindi cha timu za Ukanda wa  Afrika Mashariki na Kati kucheza Kombe la Kagame.

Michuano hiyo huchezwa kwa ngazi ya klabu na mabingwa wa nchi wanachama, na mabingwa na makombe ya vyama vya soka.

Na  lengo ingekuwa ni kuziandaa kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho inayotarajiwa kuanza Februari mwakani. Wawakilishi kwenye ukanda huu wangekutana ili kuzipa mazoezi timu hizo na kuwapa nafasi makocha kuangalia makosa, wapi kwa  kurekebisha, wapi kwa kuongeza wachezaji ili zifanye vizuri kwenye  michuano hiyo ambayo timu za ukada wa Cecafa zimekuwa kama  wasindikizaji wa kudumu. Hebu fikiria,

Chalenji inachezwa sasa, lakini haina manufaa yoyote yale na hatoisaidia timu ya taifa lolote kwa wakati huu.Michuano hii ilibidi ichezwe kabla ya kuanza michuano ya awali wa AFCON na Kombe la Dunia.

Timu za Uganda wa Cecafa, zinakwenda kucheza michuano ya  kimataifa kuanzia Februari, hivyo binafsi nilidhani kuwa Kombe la Kagame kwa muda huu ingekuwa ndiyo maandalizi sahihi kwao badala ya Chalenji.