Kama hunywi maji ya kutosha una dalili hizi

16Jan 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kama hunywi maji ya kutosha una dalili hizi

KUNA mambo matano, yanay- otajwa na wataalamu wa afya kwamba ni miongoni mwa dalili zinazoonyesha kuwa mtu hanywi maji ya kutosha, ambayo ni kupungua kwa kiwango cha mkojo na ngozi kuwa kavu sana.

Mengine ni kuumwa kichwa na mdomo kuwa mkavu na mkojo kuwa wa njano, hivyo mtu akiwa na hali ya aina hiyo, ajue kuwa kinachochangia ni kutokunywa maji ya kutosha.

Hivyo ndivyo anavyosema, Dk. Tumaini Mgutu wa Kituo cha Afya cha Alexia kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha.

Dk. Mgutu, ambaye anasema ni mtaalamu wa magonjwa ya ndani ya mwili wa binadamu, anafafanua kuwa mtu akisum- buliwa na kichwa, atambue sababu kubwa inaweza kuwa ni upungufu wa maji.

Vilevile, akiwa na ukosefu wa mate, mdomo kuwa mkavu, mkojo kuwa na rangi ya njano ajue tatizo ni hilo, kwa vile ran- gi ya mkojo inatakiwa kuwa ya njano kwa mbali, lakini njano kupitiliza ni tatizo.

Anasema, mwili wa binadamu unaundwa na asilimia 70 ya maji, na kwamba ni muhimu kunywa maji ya kutosha, ili kuuwezesha kufanya kazi inavyotakiwa na iwapo haupati maji ya kutosha ni tatizo.

“Kwa wastani, mtu ana- takiwa kwenda haja ndogo mara sita hadi saba kwa siku, na kama anakwenda chini ya
mara mbili kwa siku, basi ajue kuwa hunywi maji ya kutosha,” anasema Dk. Mgutu.

Anafafanua kuwa kutokuny- wa maji ya kutosha kunaweza kusababisha madhara mbalim- bali ya muda mfupi na muda mrefu, ikiwamo magonjwa ya shinikizo la damu, saratani na magonjwa ya figo.

“Baadhi ya watu wanadha- rau maji ya kunywa, wanaona kula ni muhimu kuliko kunywa maji, wanaona vinywaji vingine ndivyo bora kuliko maji, hawa- jui ni hasara kubwa kiasi gani wanajisababishia katika miili yao,” anasema.

Anasema kujijenga kwa kinga za mwili hutegemea sana maji, katika mwili, hivyo ni vyema mtu kuhakikisha anaongeza kinga ya mwili wake kwa kunywa maji ya kutosha, hasa kabla ya kula kitu cho- chote.

Anasema iwapo mtu akiona ana ngozi kavu, atambue hana maji ya kutosha mwilini, kwa vile hata kiwango cha maji kwenye ngozi yake kinatokana na unywaji wake wa maji.

Aidha, mtu akiona anasum- buliwa na kichwa, atambue sababu kubwa inaweza kuwa ni upungufu wa maji na pia akiwa na ukosefu wa mate, na mdomo kuwa mkavu, vilevile chanzo chake ni upungufu wa maji.

“Kwa upande wa mkojo ni kwamba rangi yake inatakiwa iwe nyeupe au njano kwa mbali, kama ukiona rangi ya mkojo si ya kawaida kuwa njano kupitiliza, tambua una upungufu wa maji mwilini,” anasema.

Pamoja na kuhamasisha watu kunywa maji, joto kali li- natajwa kuchangia kupoteza maji kwa wingi mwilini, kama mtu hakunywa ya kutosha, wakati wa joto kali anaweza ku- kumbwa na upungufu wa maji.

Kuhara na kutapika pia hu- poteza maji mengi mwilini, hivyo inashauriwa kunywa maji mara kwa mara, ili kuzuia upungufu wa maji na pia ishau- riwa kutumia maji yaliyoonge- zwa chumvi na sukari wakati mtu anapohara na kutapika kwa wakati mmoja.

Aidha, unywaji wa pombe kupita kiasi nao unachangia kupunguza maji mwilini, kwa vile pombe inasababisha mtu kwenda haja ndogo mara kwa mara na kupoteza maji kwa wingi.

Hata hivyo, mtu anatakiwa kunywa maji kulingana na uzito wako na kwamba mwenye kilo 50 anatakiwa kunywa lita mbili, wakati mwenye kilo 65 anatakiwa kunywa maji lita tatu kwa siku moja.

Kwa mtu mwenye kilo 80 na kuendelea, anatakiwa kunywa maji lita nne kwa siku, na kwamba kukaa bila ya kunywa maji ni hatari kwa afya, lakini mtu anatakiwa aanze kunywa kiasi.

Wataalamu wa afya wanase- ma, sio lazima mtu aanze moja kwa moja kunywa lita moja ya maji, mbili au tatu kwa siku, bali aanze kiasi polepole na kuongeza idadi au chupa za maji na kufikia lengo lake kwa kuzingatia uzito wake.