Kamati masaa 72 kwa Simba, Yanga tu?

06Mar 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Kamati masaa 72 kwa Simba, Yanga tu?

NI ukweli usiopingika kuwa Obrey Chirwa wa Yanga alipata kadi ya njano ya kwanza kimakosa kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Jumatano iliyopita.

Kwenye mechi hiyo iliyiochezwa Uwanja wa Taifa na Yanga kupata ushindi wa mabao 2-0, Chirwa alifunga goli lililoonekana halina dosari yoyote, lakini mwamuzi Ahmed Simba akalikataa.

Kwa mawazo yake, mwamuzi alidhani kuwa mchezaji huyo alifunga bao baada ya kuushika kwanza, au alifunga kwa mikono.

Marudio ya televisheni yanaonyesha kuwa lilipaswa kuwa goli lisilokuwa na doa, lakini mwamuzi alishamzawadia kadi ya njano ambayo ilimfanya baadaye apewe nyekundu baada ya awali kuwa na nyingine kwa kosa lingine.

Chirwa ambaye kwa sasa amekuwa tegemeo kwenye safu ya ushambuliaji Yanga baada ya Donald Ngoma kuonekana kama vile 'anadengua', alikuwa kwenye hatari ya kukosa mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar.

Wanachama na mashabiki wa Yanga walipiga kelele. Wakapaza sauti zao juu kuilalamikia kadi hiyo.
Sauti zao zikaifikia Kamati ya Masaa 72 ya Shirikisho la Soka (TFF).

Kwenye kikao cha Jumamosi, kamati ikatengua kadi hiyo na kumfanya Chirwa sasa awe na kibali cha kucheza jana. Ukiangalia yote hayo yaliyofanyika hadi kamati hiyo kuingia kati ni sahihi kabisa.

Lakini cha kujiuliza ni kwa nini kamati hiyo inaonekana kukaa vikao vyake haraka yanapokuja masuala yanayozihusu timu za Simba, Yanga au Azam tu?

Kamati hii inaonekana iko haraka sana kutatua mambo yakionekana kwenda kombo kwa timu hizo pekee dhidi ya timu nyingine, huku timu zinazoitwa au kujiita ndogo zikiwa hazinufaiki na kamati hiyo.

Tangu msimu uliopita sijaona kamati hiyo imekaa haraka kutatua tatizo la timu kama Mbeya City, Stand United, Toto African kwa mfano.

Ikumbukwe Kamati ya Masaa 72, ilikaa haraka kuifuta kadi nyekundi ya Jonas Mkude aliyopewa na mwamuzi Martin Saanya, kwenye mechi kati ya wakati wa jadi hao Oktoba Mosi mwaka jana.

Kabla Simba haijacheza mechi iliyofuata, tayari kamati hiyo ilikuwa imeshakaa na kuifuta kadi hiyo.

Na hii ilitokana na wanachama, mashabiki na viongozi wa Simba kuja juu, kutokana na uamuzi wa Saanya kwenye mechi hiyo.

Uharaka huo huo wa kamati hiyo ulikuja kwenye tukio la beki Juma Nyoso kuonekana kumfanyia kitendo kisicho cha kiungwana straika wa Azam FC, John Bocco.

Nguvu ya vyombo vya habari kutoa vipande vya picha ya tukio hilo, pamoja na video, kelele na sauti za mashabiki wa soka baada ya kuona marudio ya tukio lile, liliamsha kamati hiyo na kumfungia Nyoso mwaka 2015.

Sisemi kuwa kamati isifanye kazi yake, la hasha. Lakini ninachosema hapa isifanye kazi kwa shinikizo kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari, na klabu zenye viongozi, wanachama na mashabiki wengi nchini.

Badala yake ifanye kazi kwa usawa. Kuna baadhi ya mechi ambazo hazizihusu Simba, Yanga wala Azam yanatokea matukio kama hayo, lakini hatuoni hatua zikichukuliwa haraka.

Hivi karibuni, Stand United ililalamika kipa wao namba moja, Hamza Mhonge kupigwa kadi nyekundu kwenye moja kati ya mechi yao ya Ligi Kuu, siku chache tu kabla ya kucheza dhidi ya Yanga.

Msemaji wa Stand United, Deokaji Makomba alipiga sana kelele, lakini haikusaidia. Ni kama vile alikuwa akitoa kilio cha samaki, machozi yake yanabaki majini daima. Ni kwa sababu alikuwa peke yake.

Labda kama timu yake ingekuwa ina mashabiki wengi na ushawishi mkubwa, Kamati ya Masaa 72 ingeweza kukaa.

"Kweli tunaumia sana, si sahihi hata kidogo. Kipa namba moja, kapewa kadi ambayo utaona si sahihi, kocha wetu kaondolewa kwenye benchi wakati wanajua tunakwenda kupambana na Yanga," alisema Makomba.

"Tunaona ni kama kutudhoofisha. Tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwenye Bodi ya Ligi. Lakini msisitizo tunawaomba wawaruhusu hata kipa na kocha wetu, wawaondolee hizi adhabu.

"Tunajuwa mwamuzi Alex Mahagi amekosea, ametunyima haki yetu. Lakini hili la kocha na kipa nalo limevuka kipimo, waliangalie hili."

Hakuna kikao cha Kamati ya Masaa 72 kilichokaa hadi Stand inacheza dhidi ya Yanga Februari 3 na kubugizwa 4-0, ikiwatumia kipa namba mbili na namba tatu.

Napata shaka kama hili lingetokea kwa Simba, Yanga au Azam kama lingefumbiwa macho.
Ndiyo maana najiuliza, hivi kamati hiyo kwa timu kubwa tu?