Kambi za kitaaluma ni ufunguo kufaulu

26Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kambi za kitaaluma ni ufunguo kufaulu

KAMBI za kitaaluma zimekuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi katika kufikia maendeleo ya juu ya elimu kwa kuwawezesha kufanya vizuri kwenye mitihani yao na hivyo kuwa na uhakika wa kusonga mbele kitaaluma.

Wanafunzi ambao huwekwa katika kambi hizo maalum kwenye baadhi ya mikoa ni wale wa shule za msingi na sekondari, lengo likiwa ni kuwafundisha zaidi ili wafaulu.

Kwa kuzingatia hilo, kambi hizo za kitaaluma zinaandaliwa kwa ushirikiano kati ya shule na wadau mbalimbali wa elimu wakiwamo wazazi na walezi, ambao huchangia chakula na fedha.

Michango hiyo inawafanya wawe wadau muhimu kwenye maendeleo ya elimu kwa vile vyakula wanavyochangia na fedha wanazotoa vinatumiwa na watoto wao kambini wanapokuwa wanafundishwa.

Wanafunzi wanaowekwa kambini hupata muda mwingi wa kujifunza na kujisomea, kuchimba na kujiweka kwenye mazingira halisi ya kufanya mitihani.

Hali ambayo kwa namna moja au nyingine inasaidia kuongeza ari ya kupenda elimu na kufaulu.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa iliyobuni kambi hizi kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kufanikiwa kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari mkoani humo na kushika nafasi ya 10 kitaifa.

Nafasi hiyo ni katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka 2018, kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017 hadi kufikia ya 10 kwa mwaka jana.

Aidha, mkoa huo unaendelea kuziimarisha kambi hizo. Yapo maeneo mengine ambayo yameiga mfumo huo wa kambi za kitaaluma, lakini ninadhani ipo haja kwa nchi nzima kuutumia mpango huo ili kuwasaidia wanafunzi kupata muda wa kutosha kujiandaa kwa ajili ya mitihani.

Ikumbukwe kuwa katika mazingira ya Tanzania ni wanafunzi wachache ambao hupata nafasi ya kujisomea wanaporudi nyumbani au siku za mwisho wa wiki na wengi hawaipati.

Kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa wanafunzi wengine wengi kuwawezesha kuwa na muda wa kutosha kujiandaa na mitihani badala ya kushughulika na majukumu mengine ya nyumbani na kukosa muda wa kujisomea.

Njia ambayo imeonyesha matokeo mazuri ni kuwa na kambi za kitaaluma kwani wanafunzi hukusanywa pamoja na kuwa huko kwa miezi kadhaa hadi siku za mitihani na wanatoka wakiwa wamenolewa kikamilifu.

Siyo vibaya mikoa mingine kuiga kile kinachofanywa na Simiyu chini ya Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka, ambaye kwa kushirikiana na wadau wa elimu wa mkoa huo, walibuni kambi hizo za kitaaluma.

Najua kuna baadhi ya maeneo hapa nchini ambayo yameanza kuiga mfano huo, lakini ingependeza iwapo nchi nzima ingeiga mfano huo, kwani lengo ni kusaidia kuongeza uelewa na hata ufaulu kwa wanafunzi.

Kama nilivyosema, hali ya maisha inasababisha baadhi ya watoto wasipate nafasi ya kujisomea wawapo nyumbani, na inawezekana hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuanzisha kwa kambi hizo mkoani Simiyu.

Inaweza kutokea siku za mwisho wa wiki, mwanafunzi anakwenda kuchunga ng'ombe, kulima na shughuli nyingine za nyumbani, hizo zote ni muhimu lakini pia anatakiwa awe na muda wa kujisomea.

Njia bora ambayo imebuniwa na Mkoa wa Simiyu ni hiyo ya kuweka kambi za kitaaluma, ambayo kimsingi ni nzuri, kutokana na ukweli kwamba imekuja na matokeo mazuri, ndiyo maana nikasema mfano huo uigwe.

Hivyo, itapendeza iwapo kambi za kitaaluma zitaenea nchi nzima, jambo la muhimu ni kuwashirikisha wadau hasa wazazi ili wawe tayari kuchanga chochote kwa ajili ya kufanikisha kambi hizo.

Ninaamini kwamba mzazi au mlezi anayejua umuhimu wa elimu atakuwa tayari kuchangia kwa ajili ya kusaidia kuinua kiwango cha elimu cha mtoto wake ili aweze kusonga mbele katika masomo ya juu.

Elimu ni ufunguo wa maisha, ni mali, akiba na ina haina mwisho, kwa kuona jinsi ilivyo ya muhimu kwa mwanadamu ndiyo maana wale wanaowakwamisha wanafunzi masomo huchulikuwa hatua za kisheria.

Hivyo, mikoa ambayo bado haijaamua kuandaa kambi za kitaaluma, itafakari na kuanza kuwawezesha wanafunzi kwa kuandaa kambi hizo, ili waweze kunolewa kakamilifu na hatimaye ufaulu wao uongezeke.