Kampeni hizi zisambae zaidi kunusuru mabinti

02Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kampeni hizi zisambae zaidi kunusuru mabinti

KISWAHILI kina msemo 'ukimsomesha mtoto wa kike, utakuwa umeelimisha taifa zima' na ufafanuzi zaidi unafuata kuwa ukiwekeza elimu kwa mtoto wa kike kuna mafanikio makubwa na manufaa zaidi.

Hizo zote ni njia zinazohamasishwa na wadau wa elimu kwa lengo la kubadilika na kumsomesha watoto bila ubaguzi, kwa vile wote wana haki ya kupata elimu na kujileta maendeleo.

Wakati kukiwa na kampeni hizo, bado wapo baadhi wasiotambua umuhimu huo wa kumsomesha mtoto wa kike, badala yake wanawaingiza kwenye vitendo ambavyo vinawakwamisha kielimu.

Kwa mfano tangu shule zifungwe Machi mwaka huu, kupunguza maambukizo ya virusi vya corona, baadhi ya wanafunzi wa kike wamekumbana na changamoto zinazoweza kuwakwamisha kielimu.

Wanafunzi hao ni wa wilayani Serengeti mkoani Mara, ambao wamekutana na sintofahamu hiyo ambayo ya kuandaliwa kwa ajili ya kukeketwa, badala ya kuachwa wajisomee wakati wakisubiri shule zifunguliwe.

Katika wilaya hiyo vitendo vya ukeketaji vinadaiwa kufanyika huku zikiwa zimefungwa na kuwafanya wakose amani, hali iliyosababisha wadau wa elimu kuingilia kati na kuanzisha kampeni za kuwanusuru.

Lengo la kuanzisha kwa kampeni hizo si kuwaepusha dhidi ya ukatili huo, bali ni kutaka waachwe wawe na muda wa kujisomea ili shule zitakapofunguliwa wawe na kitu walichojifunza wakiwa nyumbani.

Hope for Girls and Woman Tanzania ni moja ya wadau wa elimu ambao kwa kushirikiana na vyombo vya dola, wanafanya kampeni za kuwanusuru wanafunzi dhidi ya ukeketaji ambazo zilianza tangu Aprili mosi mwaka huu.

Katika kampeni hizo, tayari wamepatikana wanafunzi 47, huku baadhi yao wakiwa tayari wamekeketwa, na pia zinaambatana na elimu kwa jamii ili iachane na mila hizo, ambazo zimepitwa na wakati.

Hivyo ndivyo, anavyosema Mkurugenzi Mtendaji wa Hope, Rhobi Samwelly na kufafanuwa kwamba, licha ya juhudi mbalimbali za kukomesha vitendo vya ukatili huo, bado vitendo bvya ukeketaji vipo ndani ya jamii.

Kwa maelezo hayo ya Rhobi ni wazi kwamba bado kuna safari ndefu ya kuibadili jamii ya huko, ili iachane na mila potofu zinazokandamiza mtoto wa kike na kusababisha akose elimu.

Hii inatokana na kile kinachoelezwa na baadhi ya wenyeji wa huko kwamba msichana akishakeketwa huwa anaandaliwa kwa ajili ya kuolewa, hivyo kama ni mwanafunzi, anaweza kukatishwa masomo na kuingiza kwenye ndoa.

Hivyo ni vyema kampeni hizo za kupambana na ukeketaji zikasambaa maeneo yote ya mkoa wa Mara ambayo yanadumisha mila hizo kuwanusuru wanafunzi ili waendelee kujisomea wakati wakisubiri shule zifunguliwe.

Serikali na shule zinajitahidi kutoa elimu kwa wanafunzi wakiwa nyumbani, lakini inasikitisha kusikia wapo baadhi ya wazazi ambao badala ya kuwaacha watoto wajisomee, wanawapeleka kwa ngariba wakeketwe.

Ingependeza kama mzazi au mlezi angemtafutia mtoto wake mwalimu wa kumfundisha masomo mbalimbali kuliko kumtafutia ngariba ambaye ni hatari kwa maisha na hata kwa maendeleo yake ya elimu.

Serikali ilishaweka wazi kwamba wanafunzi wamerudishwa nyumbani ili kuepushwa na maambukizo ya virusi vya corona, lakini ikiwasisitizia wazazi kutowaruhusu kuzurura ovyo.

Inasisitiza hivyo na kuwataka wahakikishe wanabaki nyumbani wakijisomea, na ndiyo maana imeanzisha vipindi vya masomo kupitia vyombo vya habari ikiwamo televisheni ili wanafunzi wasome.

Si hapo tu bali shule nazo zimekuwa zikisambaza masomo kwa wanafunzi, lengo ni kutaka wanafunzi wasiwe na muda wa kukaa bila kujisomea ili mwisho likizo ya corona wawe kama hawakuwa likizo.

Kwa hiyo wanaokwenda kinyume na maelekezo hayo na kuingiza watoto wao katika hatari ya kukeketwa, ni vyema wakafuatiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha mila hizo.

Ufuatiliaji wa vitendo vya ukeketaji lisiwe jukumu la serikali na baadhi ya asasi za kiraia tu, bali raia wote kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kufanikisha kampeni kukomesha ukeketaji Serengeti na kwingineko.