Kampeni hizi ziwe chachu kukomesha mimba

18Jul 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kampeni hizi ziwe chachu kukomesha mimba

MKOA wa Lindi kwa sasa uko kwenye kampeni maalum iliyopewa jina la ‘msaidie akue, asome, mimba baadaye’, ikiwa na lengo la kukomesha  mimba za utotoni na kuwalinda mabinti.

Kampeni hizo zinafanyika kutokana na tatizo la mimba kwa watoto wa kike kuwa kubwa mkoani humo, ambapo uzinduzi wa kampeni huyo ulifanyika  Februari mwaka huu kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mpilipili,  Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.

Katibu Tawala wa Mkoa huo,  Rehema Madenge, akitoa taarifa kuhusu kampeni hiyo, anasema inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi kwa watoto kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa kwa kuwajengea uwezo wataalamu wanaoshughulikia masuala ya ulinzi na usalama wa watoto.

Anafafanua zaidi kuwa huduma kwa waathirika wa mimba za utotoni  ni muhimu na endelevu ili kwamba mwenye mimba awe na afya bora na hata mtoto  atakayezaliwa ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa mashauri ya watoto na kuwapatia msaada wa kisaikolojia wale waliopata mimba.

Lengo lingine la kampeni ni kusimamia na kuchukua hatua za makusudi kuzuia mimba za utotoni kwa kutoa elimu na kuwajengea uwezo watoto, wazazi, walezi na wadau juu ya madhara ya mimba za utotoni kwa kuhusisha vyombo vya habari na kutumia elimu ya sanaa," anasema Madenge.

Anaongeza kuwa katika mkoa wa Lindi ongezeko la mimba za utotoni lina uhusiano mkubwa na malezi duni ya wazazi au walezi, ambapo wazazi wengi wa maeneo hayo hawako makini kufuatilia malezi na makuzi ya watoto wao.

Mtindo huo wa wazazi inaelezwa kwamba uwafanya watoto hao kuwa huru, kufanya wanachokitaka, kucheza katika mazingira hatarishi, ambako wanakuwa wanajifunza mambo mengi yasiyostahili kwa umri wao.

Nikirejea kwa kile ambacho ninataka kukijadili, ni kwamba kwa muda mrefu baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakilaumiwa kwa kutofuatilia nyendo za watoto wa kike au kumalizana na wale wanaowapa mimba.

Mtindo huu unachangia kukwamisha juhudi za serikali za kupambana na mimba za utotoni, ambazo ni kikwazo kwa watoto wa kike kutimiza ndoto zao na ni hatari kwa afya zao pia.

Wataalamu wa afya wanasema, mimba za utotoni huathiri afya kwa vile wanaopewa mimba ni wale ambao maungo yao bado hayajawa na uwezo wa kuwafanya wajifungue.

Pamoja na maelezo hayo ya wataalamu wa afya, mimba zinasababisha wakose elimu, ambayo ni moja ya haki ya msingi, na pia mabinti wasio na elimu watakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea maisha bora na familia zao.

Licha ya kuwapo kwa kampeni mbalimbali zenye lengo la kumaliza tatizo hilo, bado mimba zimeendelea kuibuka kana kwamba ni jambo la kawaida kwenye baadhi ya jamii.

Nikumbushe kwamba Januari mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa wanafunzi 140 wa shule za msingi na sekondari walikatisha masomo mwaka jana.

Kwamba 54 walikuwa wa shule za msingi na 86 wa sekondari, huku wale wa kidato cha kwanza na cha pili wakiongoza kupata mimba, wakati msingi wakiwa ni wa darasa la sita.

Siyo hapo tu, hivi karibuni mkuu huyo wa mkoa alikaririwa tena na vyombo vya habari akisema kuwa Januari hadi Juni mwaka huu, wanafunzi 60 wa shule za msingi na sekondari wamepata mimba.

Anaweka wazi kuwa mazingira ya mimba yanaashiria kuwa kuna muungano kati ya watendaji na wazazi, kwa madai kwamba wanaowapa mimba wanafunzi hawakamatwi.

Kampeni hizo ziwe chachu kukomesha mimba na ikiwezekana hatua kali zichukuliwe kwa wahusika kuanzia kwa wazazi, watoto na wale wanaowapa mimba ili liwe fundisho kwa pande zote.

Tatizo la wahusika kutochukuliwa hatua kali za kisheria lisiachwe liendelee na pia mtindo wa kumaliza mambo kimyakimya usipewe nafasi ili kusaidia binti kuepuka mimba hizo.