Kampeni, ushawishi uwe sera si mlungula

12Aug 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kampeni, ushawishi uwe sera si mlungula

OKTOBA 28, mwaka huu, Watanzania watapiga kura kuwachagua rais, wabunge na madiwani ikiwa ni baada ya zaidi ya miezi miwili ya kampeni za uchaguzi huo utakaoshirikisha wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa.

Ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inaonyesha kuwa kampeni za uchaguzi huo zinatarajia kuanza rasmi Agosti 26 hadi Oktoba 27 na kufuatiwa uchaguzi wenyewe siku inayofuata.

Katika kipindi hicho cha zaidi ya miezi miwili, wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani waliopitishwa na vyama vyao, watanadi sera na ilani za vyama vyao kwa wapigakura ili wawachague.

Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na mabadiliko kidogo ya siku, kutoka Jumapili hadi katikati ya wiki, ambayo itakuwa siku ya Jumatano, na sasa kuna hatua mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kufanikisha uchaguzi huo.

Miongoni mwa hatua hizo ni wagombea kuchukua fomu za kuwania urais, ubunge na udiwani, huku vyama vingine vikiwa, katika mchujo wa kupata wanachama wa kuviwakilisha katika uchaguzi huo.

Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo, vyema pia kuwakumbusha Watanzania kuwa makini, kwamba, wajikite katika maandalizi ya kupiga kura, ili kupata viongozi bora na siyo bora viongozi.

Hatua hiyo itawasaidia kuepuka kuchagua wagombea ambao hawana manufaa kwa maendeleo ya maeneo yao, hivyo wasichukulie wakati huu kama wa kula na kujikuta wakichagua wagombea wasiofaa.

Ikumbukwe kwamba, katika kampeni za uchaguzi, wagombea hutumia mbinu nyingi, kwa lengo la kuwaweka sawa wapigakura, hali ambayo inaweza kusababisha 'wanakula badala ya kupiga kura'.

Siyo jambo la kushangaza kukuta wagombea wakiingia nyumba kwa nyumba mara baada ya kampeni, wakati wa usiku kwa lengo la kurubuni wapigakura kwa kuwapa chochote ili wawachague. Mtindo huo ni sawa na kula siyo kura.

Huu sasa ni wakati wa kura siyo kula, wananchi wakiendekeza kula watajikuta wanachagua watu wasiofaa, hivyo watumie haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaotaka, lakini si kwa kigezo cha kupewa chochote.

Watanzania wanahimizwa kujiandikisha, katika daftari la kudumu la wapigakura, lengo ni kutaka wawe na haki ya kushiriki kwenye uchaguzi huo, hivyo wasikubali kuipoteza kwa kuchagua wagombea wasiofaa.

Julai, mwaka jana wakati akizundua rasmi uboreshaji wa daftari hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliihimiza vijana waliotimiza miaka 18 kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa kuwa bila kujiandikisha hawawezi kushiriki uchaguzi.

Kwa mantiki hiyo walioajiandikisha katika daftari hilo, watumie haki hiyo kuchagua viongozi sahihi watakaowaletea maendeleo na kuachana na wale wenye mpango wa kutoa chochote ili wachaguliwe.

Wanasiasa nao wawaache wapigakura, waamue wenyewe kuchagua viongozi wanaowataka, bila kuwapo kwa mbinu zozote chafu zinazoweza kuwaingiza katika mtego wa kuchagua kula badala ya kura.

Kila upande ukitimiza wajibu, hakutakuwa na wagombea wa kuingia nyumba kwa nyumba wakati wa usiku, kwa lengo la kurubuni wananchi kwa chochote ili wawapigie kura, watakuwa huru kuchagua viongozi wanaowataka.

Ikumbukwe kuwa uzoefu unaonyesha kuwa kuna mchezo huo ambao wakati mwingine baadhi ya wagombea hudaiwa kuwapa wapigakura vitu ili wawachague.

Wanavyopewa ni pamoja na khanga, kofia, fulana na hata wakati mwingine fedha, ikiwa ni mojawapo na ushawishi kwa wananchi, ili watoe kura zao kirahisi kwa wagombea wasiofaa.

Yawezekana kukawa na mtifuano mkali kutoka kwa wagombea watakaopitishwa na vyama vyao, hivyo ni muhimu wananchi kuwa makini, ni la msingi kwa kuwa huenda baadhi wakatumia mbinu chafu kupata ushindi.

"Wapo wanasiasa kutoka vyama mbalimbali wenye ushawishi mkubwa kwa wananchi, kinachotakiwa ni ushawishi wa sera na ilani za vyama uwe msingi wa kuwapigia kura, si mbinu za kutoa chochote.

Mgombea mwenye lengo la kuleta maendeleo hapaswi kutumia ujanja ujanja kutafuta uongozi, badala yake anaweka wazi kile anachotaka kuwafanyia wananchi ili waamue.