Kanuni mbovu Ligi Kuu ziondolewe

30May 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kanuni mbovu Ligi Kuu ziondolewe

TAYARI Bodi ya Ligi iko kwenye mchakato wa kutengeneza kanuni mpya za msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2016/17.

Bodi hiyo imetangaza kukaribisha maoni, mapendekezo na marekebisho kutoka klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya kuboresha ligi hiyo inayotoa wawakilishi wa Bara katika mashindano ya kimataifa.

Nianze kuipongeza Bodi ya Ligi kwa uharaka wa kukusanya maoni, mapendekezo na marekebisho kwa ajili ya kuondoa kasoro zilizojitokeza msimu uliomalizika hivi karibuni.

Nadhani kabla Ligi Kuu msimu mpya 2016/17 haijaanza, tayari kanuni zitakuwa zimeshakamilika na viongozi wa klabu kuzipitia na kuzisoma ili kusiwe na malalamiko.

Lakini pamoja na yote haya, ni lazima tuongee ukweli kuwa kuna matatizo kwa wadau wenyewe mpaka kwenye hizo kanuni.

Kwanza kabisa viongozi wengi wa klabu wanaonekana wako kwa kuangalia manufaa yao na si kwa ajili ya maendeleo ya soka au klabu wanazoziongoza, ndiyo maana tunaweza kusikia si wengi watakaopeleka maoni yao kwenye bodi kama ilivyotarajiwa.

Kwa muda huu ambao ligi imemalizika, mbali na wengine kuanza usajili, lakini viongozi wa klabu nyingine hawajishughulishi na soka wanaendelea na kazi zao binafsi.

Lakini hawafahamu kuwa usajili na kanuni za ligi ni vitu vinavyokwenda kwa pamoja.

Na hata pale zinapokamilika, viongozi hawa wa klabu wamekuwa hawajishughulishi kuzisoma na badala yake wanakurupuka na kusubiri 'mambo' yatakapowaharibikia na kusikika wakilalamika kuwa kanuni za ligi ni mbovu.

Huu sasa ndiyo wakati wa kukusanya maoni kupeleka mapendekezo ya kanuni bora na kuziondoa zile kandamizi na si kusubiri kulalamika kama ilivyowahi kutokea.

Kwangu mimi binafsi, moja ya kanuni mbovu kama ningekuwa kiongozi wa klabu zingependekeza ibadilike ni ile iliyoinyang'anya Azam pointi dhidi ya Mbeya City kwa kadi tatu za njano alizokuwa nazo mchezaji wake Erasto Nyoni.

Kadi ya njano au nyekundu ya mchezaji kwenye Ngao ya Jamii kuhesabiwa kwenye Ligi Kuu, hii ni moja ya kanuni mbovu kabisa na badala yake zianze kuhesabiwa kwenye mechi za kwanza za ligi.

Pili kuhamishwa mechi kiholela kama ilivyofanya Yanga dhidi ya Ndanda FC. Kanuni iwe wazi tu kuwa mechi ihamishwe kwa sababu za kiusalama, ubovu wa uwanja au matengenezo na si makubaliano baina ya klabu.

Kingine ni kubadilishwa kwa timu kuongoza kwa idadi ya magoli, badala yake iangaliwe zinapofungana wao kwa wao.

Hii inatumika kwenye kanuni ya Ligi Kuu Hispania, nadhani hapa kwetu inaweza kuwa nzuri zaidi ili timu kubwa zisipende kuzionea ndogo kwa kuzifunga idadi kubwa ya magoli, lakini zinapocheza zenyewe kwa zenyewe zinaonekana kuogopana.

Kanuni hii ndiyo itakuwa mwarobaini hata wa kununua mechi kwa magoli mengi kama ilivyokuwa kwa kina JKT Kanembwa na wenzake.

Mfano, Yanga msimu ulioisha kama kanuni hiyo ingetumika na ingefungana pointi na Simba ingetwaa ubingwa kwa sababu iliifunga Simba mara mbili.

Pamoja na hayo yote, Bodi ya Ligi, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na kamati zake waache tabia ya kuzibadili kanuni katikati ya ligi, pia kupindisha zinapozigusa baadhi ya timu hasa zile kubwa.