Kanuni za mgawanyo wa pato lako

19May 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Kanuni za mgawanyo wa pato lako

WAPENZI wa safu hii, tumeangalia mambo mbalimbali katika mtazamo wa kibiashara ambayo yanaweza kumfanya mfanyabiashara wa ngazi yoyote au yule anayekusudia kuanzisha biashara afaulu.

Kimsingi, juhudi na nidhamu ya hali ya juu inatakiwa kama ilivyo katika kazi yoyote ili mtu afikie ndoto za mafanikio.

Tumeona kanuni tofauti za fedha ambazo mfanyabiashara ama mtu mwingine anazotakiwa azifuate katika biashara yake ili iweze kuchanua na siku moja aje kuwa mmoja wa watu wenye mafanikio.

Leo tuangazie kanuni nyingine muhimu ya fedha ambayo inapaswa uitumie kwenye vyanzo vyako vyote vya fedha ili uwe na mafanikio yenye amani katika shughuli yako.

Kimsingi kanuni hii kwa njia moja au nyingine inahusisha kukigawa kipato chako katika makundi manne ama matano tofauti kwa wenye imani za kidini na iwapo nidhamu ya uhakika itafuatwa, basi mafanikio yatakuwa hayaepukiki.

Makundi hayo manne au matano ni pamoja na fedha kwa ajili ya matumizi, akiba, dharura, msaada na fungu maalum la shughuli za kidini iwapo mtu ana imani hiyo.

Kwa hiyo pato la mtu inabidi ligawanywe kiasilimia, kwamba matumizi yachukue asilimia 40, akiba, asilimia 30, dharura, asilimia 10, msaada, asilimia tano na asilimia zilizobaki yaani asilimia 15 iende kwenye shughuli za kidini kwa mtu mwenye imani hiyo.

Hivyo, kwa mfano mfanyabiashara ama mfanyakazi mwenye mshahara wa Shilingi 100,000 kwa mwezi baada ya makato, anapaswa atenge asilimia 40 sawa na 40,000 kwa matumizi yake.

Hapa ninarejea matumizi ya kila siku kwa maana ya chakula, maji, safari za mapumziko na kadhalika.

Fungu hili ndilo linalohusisha hata fedha kwa ajili ya starehe na ni muhimu nidhamu ya matumizi ikazingatiwe ili yasizidi kiwango hicho cha fedha.

Kwa upande wa akiba mtu anapaswa kuweka asilimia 30 sawa na Shilingi 30,000 kwenye pato la Sh. 100,000 kwa mwezi. Kimsingi akiba ni kwa ajili ya matumizi ya baadaye kama vile kujenga, kusomesha, kulima, kuwekeza kwenye biashara na kadhalika.

Fungu lingine ni la dharura linalopaswa kuchukua asilimia 10 ya pato sawa na Sh. 10,000.

Hili ndilo fungu ambalo ni kwa ajili ya mambo yasiyotarajiwa kama vile msiba, ugonjwa au mikwamo yoyote.

Asilimia tano sawa na shilingi elfu tano ni fedha ya msaada kwa maana ya kuwakumbuka ndugu, jamaa, wajane na wasiojiweza kama vilema.

Asilimia 15 iliyobaki, kimsingi unaweza ukaipeleka kwenye shughuli za kidini kama wewe ni muumini. Huko ndiko kuna mafungu ya 10 ama sadaka.
Ieleweke hapa kuwa hili la mwisho ni kwa ajili ya wafanyabiashara au watu wenye imani za kidini, ingawaje mtu halazimiki kufanya hivyo.

Lakini kikubwa ninachoongelea hapa ni kwamba iwapo mtu ataifuata kanuni hii kwa umakini, yumkini baada ya kipindi cha mwaka mmoja hadi miaka mitano, atakuwa ni mtu aliye na mafanikio makubwa.