Karia nakupinga hili la wazawa na wageni

01Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Karia nakupinga hili la wazawa na wageni

RAUNDI ya 12 ya Ligi Kuu Tanzania Bara imemalizika jana kwa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Mbao FC uliofanyika jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Kwa sasa masikio na macho ya mashabiki wa Yanga, Simba na Singida United wanaelekeza kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi lililoanza wiki iliyopita visiwani Zanzibar.

Lakini wakati ligi ikiwa imesimama kwenye raundi 11 kabla ya michezo ya raundi ya 12 haijafanyika, Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alifanya mkutano na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Katika mkutano huo alielezea mambo mengi ikiwa ni pamoja na tathmini ya miezi minne tangu aingie madarakani kama Rais, lakini pia katika maelezo yake aligusia kauli ambayo imekuwa ikijirudia kila wakati kuwa wachezaji wa kigeni wanaua wachezaji wazawa.

Kauli hii haijaanza leo, imekuwapo kwa muda mrefu tangu enzi ya uongozi wa Rais Leodgar Tenga.

Lakini kama wadau ni lazima tujiulize, je, hao wachezaji wa kigeni wanaokuja kucheza soka la kulipwa ndani wanaua vipi vipaji vya wachezaji wetu wa ndani?

Hii hoja haina mashiko na haipaswi kuzungumziwa, ikumbukwe Ligi Kuu ina timu 16 na kwa kanuni za TFF timu inaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 30 na kati ya hao wakigeni wasizidi saba.

Hivi wachezaji saba kwenye timu wanaweza wakaua vipaji vya wachezaji wetu wa ndani? Hapana... ukweli ni kuwa wachezaji wetu wa ndani hawajitambui, hawataki kujituma.

Hivi uwezo alionao Ibrahim Ajibu au Shiza Kichuya, ni wachezaji wangapi wa kigeni hawawafikii nyota hao? Mbona timu kama Mtibwa Sugar haina mchezaji yoyote wa kigeni na ina wachezaji wazawa tu, lakini hatuoni ikifanya vizuri sana.

Kutokuonekana au kuua vipaji vyao kwa wachezaji wetu wa ndani hatupaswi kusingizia uwapo wa wachezaji wa kigeni ambao si kila timu inayo.

Si hivyo tu, hata kufanya vibaya kwa timu yetu ya taifa, haiwezi kuwa sababu yake ni kwa kuwa tu timu zetu za Ligi Kuu zinawachezaji wa kigeni wanaopata nafasi sana ya kucheza.

Lazima tuwe wakweli, soka si mchezo wa kujificha, ni mchezo wa wazi na kila mtu anauona, mchezaji mzuri au mbaya anaonekana uwanjani.

Tuchukue mifano ya mastaa wetu wanaovuma sasa kama Kichuya, Mbaraka Yusuph au Aishi Manula, tujiulize hawa wametokea wapi? Wote hawa tumewajua au kuwasikia zaidi walipoanza kuchezea timu kubwa za Simba na Azam FC.

Wachezaji hawa hawakuja kwenye timu hizi ghafla tu, walianza kwenye timu za chini kabisa, uwezo wao, kujituma kwao kumewafanya kuonekana na leo hii hawakosekani kwenye vyombo vya habari hususan magazeti ya michezo.

Kikubwa kwa wachezaji wetu ni kujituma, hawa wachezaji tunaowaita wa kimataifa wanaokuja kwenye timu zetu, wengi wao wanauwezo unaokaribiana kabisa na wachezaji wa ndani, ila wazawa hawajitambui na hawataki kujituma.

Soka lina nidhamu yake, soka linahitaji kujituma, wachezaji wetu wavivu na ndio wanaotoa nafasi kuwapo kwa wachezaji wa nje ya nchi.

Timu ya Taifa inaweza kupata mafanikio kwa mikakati, na kuwa na wachezaji wanaojitambua na kujitua ndani ya uwanja.