Kaseja karudi Stars, Yosso mnakosea wapi?

29Jul 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kaseja karudi Stars, Yosso mnakosea wapi?

BAADA ya miaka sita kupita, hatimaye 'Tanzania One' wa zamani nchini, Juma Kaseja amerejea kwenye kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Na jana amedaka kwenye mechi ambayo Stars imecheza dhidi ya Kenya (Harambee Stars), katika mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Kurejea kwa Kaseja kwa mara nyingine tena kwenye kikosi cha Stars kumewashangaza mashabiki wengi wa soka.

Wanashangazwa kwa kipa mkongwe kama Kaseja ambaye alikuwa tayari taratibu ameshaanza kuwa kocha wa makipa, kabla ya kwenda kwenye soka la ufukweni.

Lakini ghafla akarejea kwa kasi akiwa na klabu ya KMC na kuiwezesha kushika nafasi ya nne, ikiiwezesha kutinga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hakuna ambaye haujui uwezo wa Kaseja. Kuna wakati aliitwa 'Tanzania One'. Aliwahi kuwaliza Zamalek nchini Misri alipopambana akiwa kwenye milingoti mitatu hadi kufanya mechi ya Ligi ya Mabingwa kwenda kwenye hatua ya mikwaju ya penalti mwaka 2003. Alipangua penalti mbili na kuiwezesha Simba kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, ikiivua ubingwa Zamalek.

Mshangao wa wengi ni kwamba baada ya miaka mingi kurejeshwa tena Taifa Stars, ikitegemewa kuwa uwezo wake utakuwa umeshuka na sasa kutakuwa na vijana wengi waliochipukia watachukua nafasi yake.

Alijiunga na Simba mwaka 2002 akitokea Moro United ya mkoani Morogoro. Fikiria tangu mwaka huo hadi sasa ni miaka 17.  Amerejea tena kwenye timu ya taifa.

Kijana aliyekuwa na mwaka mmoja wakati huo kwa sasa atakuwa na miaka 17 sasa. Kaseja bado yupo golini. Sababu ni nini?

Kwanza kabisa Kaseja ni mpenzi wa mazoezi. Anapenda kufanya sana mazoezi na hii inamweka fiti siku zote.

Kingine ni kwamba Kaseja hana mambo mengi nje ya uwanja. Ni mtu anayejitunza mno na hawajawahi kuwa na historia ya utovu wa nidhamu hasa akiwa nje ya uwanja.

Pamoja na kwamba kuna dhana kuwa makipa wanakaa kwenye soka kwa muda mrefu, lakini hapa Tanzania wengi wanakaa kwa muda mfupi na hata wanaokaa kwa muda mrefu hawawi kwenye kiwango cha juu kwa muda mrefu pia.

Jambo lingine la muhimu ni kwamba makipa wengi wa sasa Tanzania hawana viwango vya hali ya juu kama wale wa zamani.

Ukiondoa Aishi Manula, Benno Kakolanya na kidogo kwa sasa Metacha Mnacha na Aron Kalambo, wengine wote ni wa kawaida tu.

Nina uhakika kuwa Kaseja wa mwaka 2003 aliyeipeleka Simba kwenye makundi Ligi ya Mabingwa siyo huyu wa sasa.

Lakini kwa aina ya makipa tulionao Tanzania leo, Kaseja bado anaonekana ana uwezo mkubwa kwa sababu si wengi wenye uwezo wa kumpita yeye, au kuwa kama yeye zaidi ya hao wanne tu niliowaainisha.

Zamani Tanzania ilikuwa na makipa wengi mahiri, waliokuwa wakicheza kwa muda mrefu kiasi cha hata kocha wa timu ya taifa kuumiza kichwa.

Makipa vijana wa sasa inapaswa wajiulize wanakosea wapi? Hivi wanajisikiaje kama wao makipa vijana kabisa wanaodaka kwenye klabu mbalimbali za Ligi Kuu wameachwa na kurejeshwa kipa mkongwe? Kama ni kipaji wao nao si wanavyo?

Tatizo ni lile, kujituma na nidhamu. Kuanzia sasa wanapaswa walifanyie kazi suala hili, vinginevyo Kaseja anaweza kurejea tena kuwa 'Tanzania One' na wao wakiwa hapo hapo wanamuangalia.

Uwezo wao na kujituma ndiyo kutamfanya Kaseja atandike daluga. Kama anaona pamoja na ukongwe wake bado hawawezi kumfikia basi anaweza kukaa tena golini kwa miaka 10 tena ijayo.

Makipa vijana mnakosea wapi?