Kasi ya Rais JPM inanionyesha nchi ya asali na maziwa

11May 2016
Theonest Bingora
Nipashe
Mjadala
Kasi ya Rais JPM inanionyesha nchi ya asali na maziwa

NI takribani miezi saba tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mpaka sasa amekwishafanya mambo mengi ambayo hakika anastahili pongezi ingawa safari yake bado ni ndefu.

Si jambo la kushangaza kusikia watu wakilalamika na kukosoa jitihada zozote zifanywazo na viongozi wetu katika masuala mbalimbali kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Nachomsihi Rais wetu achape kazi bila kujali kelele za watu maana ni vigumu kumridhisha kila binadamu.

Wakati anaanza kwa ziara zake za kushtukiza katika taasisi za serikali ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili na Wizara ya Fedha, wengi walisema ni nguvu ya soda, lakini kadiri siku zinavyozidi kusogea watu wanazidi kujenga imani kuwa hakuna maigizo juu ya ayafanyayo.

Kwa mda mfupi aliokaa Ikulu tumeshuhudia akiwasimamisha kazi watendaji mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine, walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hatimaye kuiingizia Serikali hasara.

Umakini wake huo na kasi yake vimechangia kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika sekta ya umma ambako watumishi wengi walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea pasipo kutambua wala kujali kuwa wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Mapambano yake dhidi ya wabadhirifu na wahujumu uchumi ni moja kati ya vitu vinavyonishawishi kuandika haya yote.
Mtu anapofanya vizuri hata kwa jambo dogo hakika hustahili pongezi ili apate nguvu ya kufanya mazuri zaidi na sio kumvunja moyo.

Naelewa vita anayopigana si nyepesi, lakini wananchi tukimuunga mkono kwa moyo mmoja ataishinda, kuna masuala mengi yanayolikabili taifa hili tajiri ambalo limefunikwa na giza la umasikini kwa miaka mingi kutokana na kugubikwa na viongozi wengi wala rushwa, mafisadi na wabadhirifu ambao kazi yao kubwa imekuwa ni kuchumia matumbo yao pekee.

Ni madudu mengi yamekwishaibuliwa na tingatinga letu ambayo ndio yamekuwa yakiitafuna nchi yetu na kusababisha umasikini mkubwa kwa wananchi wa tabaka la chini na utajiri kwa wale wa tabaka la juu.

Mikataba ya kinyonyaji na watumishi hewa ni mifano mizuri nayoweza kuitumia katika kujenga hoja yangu. Najaribu kufikiria namna malipo yaliyokwenda kwa watumishi hewa yalivyokosesha madawati shuleni au dawa katika hospitali za umma.

Inaskitisha kwa taifa lililojaa misitu wanafunzi wanakaa chini mpaka leo hii, kama pesa hizo zingeingizwa katika huduma za kijamii matatizo ya ovyo kama ukosefu wa dawa yasingetawala katika taifa hili lililobarikiwa kwa kupewa kila aina ya rasilimali, lakini kwa bahati mbaya likapewa viongozi wengi waliojaliwa vipaji vya udokozi.

Nachoamini kama kweli yote haya atayashughulikia ipasavyo kelele zitapungua na Mtanzania wa hali chini maisha yake yatabadilika, kuna baadhi ya watu walishaigeuza nchi hii kama yao kwa kuvunja sheria na kufanya kila watakacho kutoakana na vyeo vya umungu mtu walivyojipatia.

Lakini kwa muda huu mfupi tumeshuhudia watu hao hasa viongozi waliozoea kuagiza na kusubiri kuletewa taarifa ambazo wakati mwingine huwa hazina uhalisia ofisini kisha kutoa matamko wakitembelea sehemu mbalimbali na kuchukua hatua sahihi dhidi ya waliochini yao hasa wanaposhindwa kutekeleza ipasavyo majukumu waliyowapatia.

Bado nina imani sana na Rais wangu na nachowaomba Watanzania wenzangu tumwache afanye kazi yake huku tukizidi kumwombea ili aifikishe kwenye Tanzania ya asali na maziwa.

Kumbeza na kukejeli juhudi zake ni kumkatisha tamaa ingawa naamini atasimama imara na kuendelea kupambama kwa ajili ya wanyonge ambao ndio wanaoteseka siku zote katika taifa hili.

Kazi aliyonayo ni kubwa ukizingatia wingi wa changamoto zinazolikabili taifa hili, lakini napenda kumtia moyo kwamba hata Roma haikujengwa kwa siku moja. Tuwe na subira huku tukisimama imara katika kusapoti kwa vitendo yale ayafanyayo kwa manufaa yetu na kizazi kijacho.

Tusikae na kusubiri miujiza, tuchape kazi, tujiamini na kujali muda katika kila jambo hiyo ndio siri pekee ya mafanikio, kukaa na kusubiri tupiganiwe pasipo kujipigania siyo jambo la busara.

Huu ni muda wa kila mwananchi kusafiri na basi la ‘Haoa Kazi tu’ kwa kuweka pembeni na siasa, vyama, ukabila, udini ili tujenge taifa imara na bora kama Rais anavyosisitiza mara kwa mara katika hotuba zake akisema kuwa “Uchaguzi umekwisha, sasa ni wakati wa kuijenga Tanzania maana nilichaguliwa kuwatumikia watu wote pasipo kujali itikadi zao kisiasa wala kidini.”

Ni kweli, yapo mengi ya kujadili na kukosoa maana hakuna binadamu aliyekamilika hivyo yeye pia anaweza kosea kama binadamu mwingine hivyo tusitumie nafasi hiyo kutoa hukumu za chuki dhidi yake bali tutumie nafasi zetu kumwelekeza maana tunaamini Rais wetu ni msikivu ambaye anaendesha nchi hii kwa mujibu wa katiba na sheria.
“Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu”