Kasoro TFF ya Karia hata ile ya Malinzi zilikuwapo

03Jun 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kasoro TFF ya Karia hata ile ya Malinzi zilikuwapo

BAADA ya Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, wadau wengi wakiwamo wachezaji wa zamani, makocha wamekuwa wakihojiwa jinsi walivyoiona ligi hiyo msimu huu.

Baadhi wameeleza mazuri na upungufu na kushauri jinsi gani ya kupunguza makosa msimu ujao. Lakini wapo ambao wanaponda kuwa hawajawahi kuona ligi mbovu kama hii iliyomalizika.

 

Sababu inaelezwa kuwa ni viporo vingi kwa Simba. Wengine wanadai Yanga ilipewa upendeleo maalum kwa kucheza mechi zaidi ya 10 kwenye uwanja wake wa nyumbani, Taifa bila kutoka mwanzoni mwa ligi. Wengine ni kwa sababu hakuna udhamini.

Ni kweli kila mtu ana maoni yake, lakini mara nyingi inashauriwa kuwa maoni yaendane na hoja, takwimu na rekodi hasa kwa watu wa michezo.

Binafsi, kwa maoni yangu wale wanaodai kuwa Ligi Kuu ya msimu huu ilikuwa mbovu zaidi kwa sababu wanazozisema, hawajalinganisha na hizo zilizopita na badala yake huenda wanazungumza kwa hisia zao ndani ya mioyo, kufuata mkumbo au vyote viwili.

Kuhusu suala ya viporo vya Simba ambavyo ndivyo vinalalamikiwa sana ni kwamba hata huko nyuma, yaani misimu mitatu minne hadi mitano hakujawahi kuchezwa ligi ambayo haikuwa na viporo.

Nadhani msimu huu viliongezeka kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kubadilika kwa Kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Hata TFF iliyopita chini ya Jamal Malinzi ilikuwa na viporo kwa timu ambazo zilikuwa zikishiriki michuano ya kimataifa hasa Yanga na Azam.

Nakumbuka kuna wakati hata Azam ilikuwa ikiomba kwenda nje ya nchi kwa ajili ya mechi za kirafiki, mechi zao zinaahirishwa, lakini ligi inaendelea na yenyewe ikawa na viporo, lakini ligi ilimalizika na hatukusikia sauti za ligi mbovu.

Hakukuwa na sababu yoyote ya maana ya Azam kwenda nje wakati kuna ratiba ya ligi. Sipati picha kama ndiyo ingekuwa sasa wakati wa Wallace Karia Azam ingepewa ruhusa hiyo na mechi zake kuwekwa viporo ingefunika vilivyo kwenye mitandao ya kijamii.

Kuhusu maamuzi tata ya waamuzi, hilo hata halipaswi kujadiliwa kwa sababu miaka nenda miaka rudi lipo kwenye Ligi Kuu, kiasi cha baadhi tulishawahi kuandika makala miaka ya nyuma kuwa imefika wakati kuleta baadhi ya waamuzi kutoka nje ya nchi kwenye baadhi ya mechi, lakini si utawala wa Malinzi wala wa Karia, hakuna kilichotekelezeka. Nashangaa msimu huu eti kuonekana kuwa limekuwa kubwa zaidi wakati matukio ni yale yale tu.

Kuhusu suala ya Kagera Sugar kuonekana kama imeshuka, lakini kumbe mahesabu yalikosewa, hili nalo linaonekana kama jambo la ajabu kabisa ambalo halijawahi kutokea kwenye historia ya soka na kuifanya TFF hii kuhesabika kuwa ni dhaifu, lakini misimu miwili nyuma kulikuwa na suala ambalo hadi leo bado ni kitendawili la Kagera Sugar dhidi ya Simba.

TFF iliyopita eti ilishindwa kujua kama mchezaji wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi ana kadi tatu za njano au la.

Baada ya Bodi ya Ligi kujiridhisha kuwa kadi ilikuwapo, TFF iliingilia kati, lakini haikusema kuwa ilikuwapo au la, badala yake iliwaita viongozi wa Kagera Sugar, mchezaji mwenyewe na waamuzi wote, wakawaweka karibuni wiki nzima Dar es Salaama kwa ajili ya kuitafuta kadi au kuwaliza.

Kilichoamuliwa ni matokeo ya mechi kuwa kama yalivyokuwa na haikusemwa rasmi kama ilikuwapo au la, badala yake ikatamkwa tu kuwa mchezaji huyo atatumikia adhabu yake ya kukosa mchezo kwenye mechi inayokuja. Hiki kilikuwa ni kituko cha mwaka kwa sababu mwamuzi wa kati anaweza kuthibitisha kama alimpa mchezaji au la. Lakini ligi iliendelea na ikaisha, hakukuwa maneno mengi kihivyo.

Kwa mifano hii tu michache, inaonyesha kuwa mapungufu ya TFF ya sasa yalikuwapo hata huko nyuma.

Binafsi, sipendi upungufu huo uwe unajirudi, lakini napinga wale wanaoonekana kutaka kuifanya TFF ya Karia ionekane ndiyo imeoza kuliko zilizopita na yote yanayotokea ni maajabu na hayajawahi kuonekana kwenye soka la Tanzania. Tunachotakiwa kushauri ni kuwaambia kuwa msimu ujao wajitahidi kupunguza upungufu uliojitokeza msimu huu.